Friday, August 17, 2018

KIWANDA CHA USHONAJI KUAJIRI VIJANA NA WANAWAKE SIMIYU


Kukamilika kwa kiwanda cha ushonaji  katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi kutasaidia kuongeza ajira, ujuzi na vipato vya wananchi wa Simiyu hususani  wanawake na vijana.

Kiwanda hicho kinakadiriwa kujengwa kwa fedha kiasi cha shilingi milioni 85 hadi kukamilika kwake ambapo itatoa pia fursa kwa wakazi wa mji wa Bariadi na Mkoa mzima kwenda kujifunza ushonaji na ubunifu wa mitindo mbalimbali ya nguo ambayo baadae wataweza kujiajiri na kujiongezea kipato.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho  mbele ya kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Ndg. Charles Kabeho  kabla ya kuweka jiwe la msingi kiwanda hicho ,Mhandisi  wa Halmashauri ya Mji Samwel Msolini amesema Halmashauri ilipokea msaada wa vyerehani 50,  kutoka Serikali ya Jamhuri ya China, vyerehani 25 vikiwa vya umeme na vingine 25 ni vya kawaida.

Ameongeza kuwa baada ya kupokea msaada huo Halmashauri imeamua kuanzisha Kiwanda hicho ili kuviwezesha kutumika na hatimaye Halmashauri ipate mapato, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi kupata huduma za mavazi yenye kiwango.
  
“”Lengo la Ujenzi wa Kiwanda cha Ushonaji ni kwa ajili ya kushona nguo kwa mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na nguo zinazovaliwa  kwenye sherehe mbalimbali, sare za shule na maeneo ya kazi, mradi huu ukikamilika utaongeza mapato ya Halmashauri, kutoa ajira kwa wananchi na wananchi watapata huduma ya mavazi” alisema Msolini..

Aidha,  akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hiki, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho amefurahishwa sana na akapongeza Halmashauri kwa kubuni mradi huo ambao amesema utakuwa na manufaa kwa wananchi na Halmashauri.

“Kiwanda hiki  kitawasaidia wajasiriamali wanaojihusisha na masuala ya ushonaji  kupata kipato, kitawasaidia wananchi kujiajiri wenyewe, lakini pia Halmashauri nayo itapata mapato” alisema Charles Kabeho..

Angello Michael mkazi wa mji wa Bariadi alisema kiwanda hicho kitasaidia vijana na wanawake wengi ambao hawana kazi za kufanya na kubadilisha maisha na vipato vyao kwa baadaye.

Katika hatua nyingine Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018 amewapongeza Wananchi na Viongozi katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwa namna walivyoshirikiana katika ujenzi wa Miundombinu ya Elimu katika Shule ya msingi Kilulu na akatoa wito wananchi kwenda kujifunza ujenzi wa majengo mazuri yenye kiwango kwa gharama nafuu.

Aidha Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri Mji wa Bariadi,  pamoja na kuweka Jiwe la Msingi la kiwanda cha ushonaji, umepitia miradi mingine katika Sekta ya Elimu, Afya, Mazingira, Sekta Binafsi  na Ujenzi.

MWISHO
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akiweka jiwe la Msingi la Jengo/Kiwanda cha Ushonaji Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Agosti 16, 2018. 
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani katika makabidhiano Kijiji cha Gambasingu Wilayani Itilima, Agosti 16, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga(kulia), Katibu Tawala Mkoa(kushoto) wakiwa pamoja na baadhi ya Wakimbiza Mwenge Kitaifa mwaka 2018 na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu John mara baada ya Mwenge wa uhuru kuona msitu wa asili na mradi wa maji.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akifungua mabomba ya maji ili kujiridha kama ni kweli yanatoka, kabla ya Kufungua mradi wa maji wa Gitoya Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Agosti 16, Bariadi.
Askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia(FFU) na baadhi ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, wakielekea eneo la Mradi wa kufungua madarasa matatu katika Shule ya Msingi Kilulu Mjini Bariadi, Agosti 16, 2018.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akizungumza na viongozi na wananchi wa Bariadi Mjini mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la Jengo/Kiwanda cha Ushonaji Mjini Bariadi, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Agosti 16, 2018. 
Mfanyabiashara wa Mjini Bariadi, Bw. John Sabu na akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo( wa pili kushoto), kuweka Jiwe la Msingi la Hoteli yake ya SweetDream,(kulia)ni mtoto wao.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeyo akiweka jiwe la Msingi katika Hoteli ya Sweet Dreams ya Mjini Bariadi inayomilikiwa na Mfanyabiashara John Sabu, wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Mjini Bariadi, Agosti 16, 2018. 


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!