Tuesday, October 8, 2019

DKT MWANJELWA ATOA NENO KAMBI ZA KITAALUMA SIMIYU

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa ametoa wito kwa wanafunzi wa kidato cha nne mkoani Simiyu ambao walipata  ufaulu hafifu katika mtihani wa utimilifu  (mock) walioko  kambi ya kitaaluma ,kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii ili waweze  kutimiza ndoto zao.

Dkt Mwanjelwa ametoa wito huo alipowatembelea wanafunzi hao katika kambi ya kitaaluma iliyopo chuo cha ualimu Bariadi mkoani hapa na kuwasisitiza walimu mbali na kuwafundisha masomo ya darasani pia  wawafundishe  namna ya kukabiliana na maisha baada ya kumaliza masomo ili ambao hawatabahatika kuendelea na masomo ya juu waweze kujiajri na kuajiri wengine.

Katika hatua nyingine Mwanjelwa amewataka wanafunzi kuitumia fursa ya uwepo wao kambini kufanya kile kilichowapeleka, watumie muda mwingi kujifunza na  wajiepusha na mahusiano ya kimapenzi ambayo yatawasababishia kushindwa kutimiza malengo yao ya baadaye.

“Maisha bila malengo sio maisha nini matarajio yako baada ya kusoma na endepo hutafaulu ujue namna ya kujiajiri, tumieni fursa ya kuwa hapa kuhakikisha mnasoma kwa bidii ishike sana elimu MUNGU hatakuacha, maisha lazima myatafute ,myatolee jasho, ” alisema Mwajelwa

“Wanafunzi wa kike jitunzeni lindeni utu wenu asitokee mtu akawadanganya mkashindwa kufikia ndoto zenu ninyi ni wa thamani kubwa kumbukeni mbali na mimba kuna magonjwa, ” aliongeza Dkt Mwanjelwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema kama mkoa  wataendelea kusimamia fedha  zote  zinazotolewa na serikali ya awamu ya tano  za elimu bila malipo ili ziweze kuleta matokeo chanya .

“Tunatamani kuona elimu bure inayotolewa na serikali inazaa matunda tutapambana kuhakikisha vituo vya kutolea elimu vinakuwa na mazingira bora na kama mlivyomuahidi kwa ziro hakuna na iwe hivyo, ”alisema Sagini

Awali  baadhi ya wanafunzi waliopo kambini hapo wamemshukuru mkuu wa mkoa huo  kwa kuanzisha kambi za kitaaluma ambazo wamesema zimewawezesha kuwa na uwelewa wa masomo mbalimbali kupitia walimu mahiri hatua iliyowatoa kwenye daraja sifuri mpaka daraja la 111 kupitia mitihani mbalimbali wanayopewa kambini hapo..

“Nilikuja kambini hapa nikiwa na division ziro tulivyofanya mtihani wa mock ufaulu uliongezaka na nikikapata division 111 awali nilikuwa sijui kuandika essay sasa hivi najua na  nina uwezo wa kuandika barua ya kuomba kazi ninachokuhakikishia mhe,pamoja na mkoa chini ya mkuu wetu wa mkoa hatutawaangusha alisema ” Pendo Aguda kutoka shule ya sekondari Old Maswa.

Akiwa kambini hapo Dkt. Mwanjelwa amekabidhi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga kilo elfu moja za unga wa mahindi, kilo mia tano za mchele na mafuta ndoo ishirini kwa ajili wanafunzi walioko kambini.
MWISHO
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu na wanafunzi wa kidato cha nne mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaaluma wakati alipowatembela kambini hapo Oktoba 5, 2019 


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa akikabidhi baadhi msaada wa chakula na mafuta kwa niaba ya  Mbunge wa Itilima Njalu Silanga kwa wanafunzi wa kidato cha nne walio katika kambi ya kitaaluma wakati alipowatembelea, Oktoba 05, 2019.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne walio katika kambi ya kitaaluma  Chuo cha Ualimu Bariadi wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa alipowatembelea Oktoba 05, 2019.



Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Mary Mwanjelwa akizungumza na wanafunzi wa kidato cha nne mkoani Simiyu walio katika kambi ya kitaalumakatika Chuo cha Ualimu Bariadi  wakati alipowatembela kambini hapo Oktoba 5, 2019

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!