Tuesday, October 8, 2019

TRC YAAHIDI KUWARAHISISHIA WACHAMBUZI WA PAMBA USAFIRISHAJI WA MAROBOTA

Mkurugenzi wa shirika la reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa amesema kuwa shirika hilo limejipanga kuhakikisha linarahisiha huduma za usafirishaji wa marobota ya pamba kwa njia ya reli  lengo likiwa kuwapunguzia gharama wenye viwanda vya kuchambua pamba.


Kadogosa amesema hayo  mara baada ya kutembelea viwanda vya kuchambua pamba vya Alliance kilichopo kata ya Kasoli na NGS katika wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Pamoja na kupunguza gharama ameongeza kuwa njia hiyo ni salama na ya uhakika hata kipindi cha mvua mzigo unafika kwa urahisi bila matatizo ya aina yoyote huku akiongeza kuwa shirika la reli litaweka miundombinu itakayowarahisishia usafirishaji huo.

"Tumejipanga kuweka miundombinu itayowasaidia mizigo yakiwemo marobota ya pamba kusafirishwa kwa urahisi bila usumbufu wowote niwaombe wafanyabiashara watumie fursa hii ya reli kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaingizia vipato hivyo kubadilisha maisha yao," alisema Kadogosa

Katika hatua nyingine  aliongeza kuwa ni vyema jamii ione umuhimu wa kujenga viwanda vya nyama ili iwe iweze kusafirishwa nyama badala ya Mifugo ambapo mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa yenye mifugo mingi nchini  .

Awali akimkaribisha mkurugenzi huyo mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kumekuwepo na  changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara hususan katika usafirishaji wa robota za pamba kwani wanalazimika kutumia magari jambo linalopelekea kusafirisha mizigo michache kwa gharama kubwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe.  Enock Yakobo amewasisitiza wafanyabiashara hao kuona haja ya kutumia reli kwani huduma hiyo imesogezwa karibu na itawasaidia kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya gharama za  usafirishaji na potevu wa robota za pamba.

Aliongezea kuwa ni vyema  ujenzi wa eneo la kuhifadhia marobota ya pamba eneo la Malampaka ukazingatiwa huku akiongeza  kuwa ujio wa usafirishaji wa  kupitia njia ya reli utawarahisishia na kuwapunguzia gharama wenye viwanda vya kuchambua pamba.

Ibrahimu Kadudu ni mrajisi mkoa wa Simiyu amesema kuwa makisio ya mkoa ilikuwa kuzalisha kilogramu milioni 180 na hadi kufikia septemba 22 2019, jumla ya pamba kilogramu milioni 148,836,601 zilikusanywa kwenye vyama vya ushirika ,pamba iliyosafirishwa ni kilogramu milioni 116,391,208, iliyolipiwa kati ya pamba iliyosafirishwa ni kilogramu  milioni 85,166,453 , kilogramu milioni 31,106,816 zilisafirishwa bila kulipiwa huku kiasi kilogramu milioni 32,445,393 zikiwa bado kwenye maghala na kwa baadhi ya wakulima.

Kwa upande wake meneja wa kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance ambaye pia ni katibu wa wanunuzi nchini Boaz Ogolla alisema kuwa uzalishaji umeongezeka ambapo umesababisha uhitaji mkubwa wa magari ya kusafirishia marobota ya pamba huku akitolea mfano kiwanda cha ni Alliance.

“ Kiwanda hiki kinazalisha robota 400 kwa siku na zinazosafirishwa kwa siku ni robota 200 hivyo ujio wa usafirishaji kwa njia ya reli utamaliza changamoto hiyo maana behewa moja lina uwezo wa kubeba maroboto 90 tofauti na gari lina uwezo wa kubeba marobota 25,” alisema Ogola.

Sambamba na hayo ameongeza kuwa usafirishaji huo utawapunguzia gharama ambazo sio za lazima na kuwa awali changamoto ya usafirishaji iliwalazimu kulipia mizigo kwa gharama kubwa ambapo kupitia reli watasafirisha kwa gharama nafuu hivyo kutawawezesha na wao kupata faida kwenye biashara zao.
MWISHO


Mkurugenzi wa Alliance Ginneries Limited Bw. Boaz Ogola(kulia) akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa(katikati) na viongozi wengine wa Mkoa wa Simiyu, wakati alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kasoli wilayani Bariadi,  Oktoba 05, 2019  kwa lengo la kujionea uzalishaji wa robota za pamba ambazo shirika hilo linatarajia kusafirisha,

Mkurugenzi wa kiwanda cha kuchambua pamba cha NGS, Njalu Silanga (wa tatu kulia akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa(wan ne kulia) na viongozi wengine wa Mkoa wa Simiyu, wakati alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mjini Bariadi   Oktoba 05, 2019  kwa lengo la kujionea uzalishaji wa rmarobota ya pamba ambayo shirika hilo linatarajia kusafirisha.

Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa akizungumza na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu nawa Kiwanda cha  Alliance Ginneries Limited kabla ya kuanza kukagua hali ya uzalishaji wa robota za pamba kiwandani hapo, Oktoba 05, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa katika Kiwanda cha  Alliance Ginneries Limited yenye lengo la kujionea hali ya uzalishaji wa marobota ya pamba kiwandani hapo, Oktoba 05, 2019.
Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakiangalia namna marobota yanayozalishwa katika Kiwanda cha  Alliance Ginneries Limited wakati wa ziara ya kuona hali ya uzalishaji wa marobota ya pamba kiwandani hapo, Oktoba 05, 2019.
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtakawakipewa maelezo  na Mkurugenzi wa Alliance Ginneries Limited Bw. Boaz Ogola juu ya namna pamba inavyochakatwa wakati wa ziara ya kuona hali ya uzalishaji wa marobota ya pamba kiwandani hapo, Oktoba 05, 2019.
Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakitoka katika moja ya maghala ya Kiwanda cha kuchambua pamba cha NGS  wakati wa ziara ya kuona hali ya uzalishaji wa marobota ya pamba kiwandani hapo, Oktoba 05, 2019.
Mkurugenzi wa Alliance Ginneries Limited Bw. Boaz Ogola(kushoto) akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini(TRC), Bw.Masanja Kadogosa(katikati) na viongozi wengine wa Mkoa wa Simiyu, wakati alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kasoli wilayani Bariadi,  Oktoba 05, 2019  kwa lengo la kujionea uzalishaji wa robota za pamba ambazo shirika hilo linatarajia kusafirisha, 

0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!