Na
Stella Kalinga
Taasisi ya Benjamin
Mkapa Foundation imekabidhi Serikali jumla ya Nyumba 28 kati ya 48
zinazotarajiwa kujengwa kwa ajili ya watumishi wa Idara ya Afya na Majengo
Mawili ya Upasuaji kwa ajili ya huduma za akina mama wajawazito Mkoani Simiyu.
Akipokea na kufungua
Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya cha Ngulyati Wilayani Bariadi na Nyumba
za Watumishi katika Hospitali ya Mkula wilayani Busega, Waziri wa Afya,Maendeleo
ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto , Mhe.Ummy Mwalimu ameishukuru Taasisi hiyo
kwa kuuunga mkono Serikali katika uboreshaji wa huduma za Afya, hasa katika
ujenzi wa miundombinu ya Afya.
Mhe.Waziri amesema
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuboresha huduma za Afya kwa kuongeza
kiwango cha upatikanaji wa dawa na vifaa
tiba, miundombinu ya Afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali, Vituo vya
Afya, Zahanati na Majengo ya Upasuaji, hivyo upatikanaji wa majengo hayo
utasaidia wananchi wa maeneo husika kupata huduma zinazotakiwa.
Mhe.Waziri ameongeza
kuwa Serikali imeanza kwa kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa
kuongeza bajeti, ambapo kwa Mwaka 2015
zilitengwa jumla ya shilingi bilioni 31 na mwaka 2016 zimetengwa shilingi
bilioni 51.
Amesema Serikali kwa
kushirikiana na wadau wengine imejipanga kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa
Mkoani Simiyu, hivyo pindi kiwanda hicho kitakapokamilika dawa za Vituo
Mbalimbali vya kutolea huduma za Afya zitanunuliwa Simiyu.
Aidha, Mhe.Ummy Mwalimu
ameutaka Uongozi wa Mkoa uhakikishe unasimamia ukusanyaji wa mapato katika
Vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, ili sehemu ya mapato hayo itumike kununulia
dawa na vifaa tiba kwa lengo la kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma
bora za afya.
Katika kukabiliana na
tatizo la vifo vya akina mama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua,
Mhe.Ummy Mwalimu amewataka akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya
kutolea huduma za Afya, ikiwa ni pamoja na kituo cha Afya cha Ngulyati mahali
ambapo Jengo la Upasuaji na wodi kwa ajili ya akina mama wajawazito vimejengwa.
Sanjari na hilo
Mhe.Ummy Mwalimu akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Ngulyati wilayani
Bariadi na Mkula wilayani Busega, amewahakikishia kuwa Wizara yake italeta
watumishi wa idara ya afya ili kukabiliana na upungufu uliopo na akazitaka
Halmashauri zote mkoani Simiyu kutengeneza mazingira mazuri ambayo yatawapa
motisha watumishi watakaoletwa na kuendelea kubaki Simiyu.
Akizungumza wakati wa
makabidhiano ya nyumba za watumishi na majengo ya Upasuaji, Afisa Mtendaji Mkuu
wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Dkt.Hellen Mkondya Senkoro
amesema, Taasisi hiyo imekamilisha
majengo hayo yote na akaiomba Serikali kuweka miundombinu iliyosalia kama maji,
vifaa vya kutolea huduma na watumishi ili wananchi waweze kunufaika na miradi
hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameishukuru Taasisi ya Mkapa Foundation na
akaahidi kuwa Serikali itajitahidi kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa
katika miradi ya Benjamin Mkapa Foundation ili itekelezwe kwa tija na manufaa
kwa wananchi.
Aidha,Mkuu huyo wa Mkoa
amemshukuru Waziri wa Afya,Maendeleo yaJamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy
Mwalimu kwa kutoa magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) nane(08) kwa Vituo vya
Afya,Hospitali za Wilaya na Hosptali Teule ya Mkoa kwa ajili ya kusaidia kutoa
huduma.
Wakati huo huo Mbunge
wa Busega,Mhe.Dkt.Raphael Chegeni amemshukuru Mhe Waziri kwa jitihada
zinazoendelea kufanyika katika kuboresha huduma za Afya Mkoani Simiyu na
akamuomba aupe kipaumbele Mkoa wa Simiyu, hususani Wilaya za Busega na Itilima
ambazo ni mpya kila Wizara yake inapogawa rasilimali au miundombinu mingine ya
Afya.
Wilaya za Mkoa wa Simiyu zilizonufaika na
Mradi wa Ujenzi wa Majengo ya Upasuaji sambamba na wodi ya wazazi Bariadi na
Busega ambayo yamejengwa kwa thamani ya shilingi milioni 435, kwa upande wa Nyumba
za Watumishi wilaya ya Busega (Nyumba 10),Itilima (Nyumba 10) na Bariadi ni
Nyumba 08 ambazo zimegharimu jumla ya shilingi bilioni 1.47.
0 comments:
Post a Comment