Na
Stella Kalinga
Mkoa wa Simiyu umejipanga kuhakikisha
hakuna maambukizi mapya ya VVU ifikapo mwaka 2020, kwa kuwaanzishia dawa za
kufubaza VVU wote watakaopimwa na kubainika kuwa na VVU bila kujali wingi wa
CD4 kama mwongozo mpya unavyoeleza.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Dkt. Mageda Kihulya wakati akitoa taarifa ya hali ya
maambukizi ya VVU na Ukimwi katika Uzinduzi wa Kampeni ya Huduma Jumuishi za
kuzuia maambukizi ya VVU uliofanyika kimkoa katika viwanja vya Sabasaba Mjini
Bariadi.
Dkt Mageda amesema hadi kufikia Septemba
2016 Mkoa umesajili wateja 40,426 kwenye huduma za tiba na matunzo (CTC) na
kati ya hao 34,838 tayari walikuwa wameanzishiwa dawa za ARV sawa na
asilimia 86,huku wagonjwa wanaoendelea na dawa za kufubaza VVU ni 18,246 sawa
na asilimia 52.
Dkt. Mageda ameongeza kuwa katika kipindi
cha Januari hadi Desemba 2015 wananchi wapatao 262,862 walipata huduma ya
ushauri nasaha na upimaji na kati yao 8,631 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU
sawa na asilimia 3.3 chini ya kiwango cha maambukizi cha kitaifa ambacho ni
asilimia 5.1.
Aidha, akina mama wajawazito wapatao
92,964 katika kipindi cha Januari- Desemba 2015, waliohudhuria kliniki
walipimwa kujua hali ya afya zao ikiwa ni kutekeleza mpango kabambe wa
kuzuia maambukizi yaVVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kati yao akinamama
1,459 waligundulika kuwa na virusi sawa na 1.6%.
Sanjari na hilo Mganga Mkuu huyo wa Mkoa
ameanisha mikakati ya kuzuia maambukizi mapya ya VVU ifikapo 2020 Mkoani Simiyu, kuwa ni pamoja na kutoa huduma
za ushauri nasaha na upimaji kuwawezesha watu kujua hali
zao na kujikinga na kukinga wenzao wasipate maambukizi mapya, sambamba
na kuwaanzishia dawa za kufubaza virusi wale wote watakaopimwa na kubainika na VVU
bila kujali wingi wa CD4 kama mwongozo mpya unavyoeleza.
Mikakati mingine ni na kupima na kuanzisha dawa za
kufubaza VVU kwa akinamama wote wajawazito na wanao nyonyesha
watakaobanika na VVU, kutoa huduma ya tohara ya
hiari kwa wanaume na kuwafanyia uchunguzi wa Kifua Kikuu na kuwatibu
mara kwa mara watakaobainika kuwa na Kifua Kikuu kwani ni moja ya
magonjwa nyemelezi yanayoua watu wengi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Anthony Mtaka, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, amesema
kuwa Kampeni ya Huduma Jumuishi za kuzuia Maambukizi ya VVU itatekelezwa
hadi Juni 2017, ambapo inalenga kufikia watu zaidi ya 6,000 katika wilaya zote
za mkoa huu, huku akitoa rai kwa wadau kufuata sera, miongozo na sheria za Nchi katika
kutoa huduma za VVU na Ukimwi wakati na baada ya kampeni hii.
Kwa upande
wake Meneja wa AMREF Tanzania Dkt. Amosi Nyirenda amesema Shirika hilo linafanya kazi
kwa kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI na amewaomba
wakazi wa Mkoa wa Simiyu kujenga utamaduni wa kupima ili kujua afya zao wanapobaini
wameathirika ni vema kuanza dawa mapema.
“Sisi kama AMREF
tunafanya kazi na Serikali kuhakikisha tunashirikiana katika mapambano maeneo yote, tunakwenda zaidi maeneo yenye uhitaji leo
tumezindua kampeni hii hapa na tutaendelea na kata 25 mpaka Desemba mwaka huu na mwaka ujao tutaenda
kata 18 za mkoa wa Simiyu tutashirikiana na timu ya mkoa kuanisha kata husika”
alisema Dkt.Nyirenda.
Uzinduzi wa Kampeni ya Huduma Jumuishi
za kuzuia Maambukizi ya VVU Mkoa wa Simiyu, umeenda sambamba na uchangiaji
wa damu kwa hiari, huduma za upimaji VVU, Toharakinga kwa wanaume, huduma za
kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, huduma za magonjwa
ya ngono na via vya uzazi, upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi na huduma za
ushauri wa lishe bora.
Kampeni hii inatekelezwa chini ya kauli
mbiu ya“PIMA AFYA YAKO UOKOE MAISHA YAKO NA YA WENZIO”
0 comments:
Post a Comment