Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kabita Wilayani Busega wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Fogofogo. |
Na Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe. Anthony Mtaka amewashauri wananchi wa Mkoa huo kuzingatia uzazi wa mpango
ili wawe na idadi ya watoto watakaoweza kuwahudumia vizuri kwa kuwapatia mahitaji
yote muhimu.
Mtaka ameyasema hayo
jana alipozungumza na wananchi wa Kata ya Kabita Wilayani Busega Mkoani humo
kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Shule ya Msingi Fogofogo, kabla ya kuwakabidhi wananchi hao mifuko 100
ya saruji ikiwa ni kuwaunga mkono katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli
hiyo kufuatia taarifa ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Fogofogo, Nyabunyili
Tolokoko kuonesha kuwa shule hiyo ina upungufu wa vyumba 21 vya madarasa
kutokana na shule hiyo kuwa na idadi
ya wanafunzi zaidi 1600.
Mtaka amesema Serikali
imekuwa ikitoa elimu bila malipo kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wananchi kwa
kutoa michango isiyo ya lazima, lakini kama watakuwa na watoto wengi watakaoshindwa
kuwapa huduma na mahitaji muhimu hawataona unafuu na umuhimu wa elimu bure kwa
kuwa bado watakuwa na mzigo mzito.
“Ndugu zangu tuunge
mkono kampeni ya Serikali ya Uzazi wa Mpango na Nyota ya Kijani, itatusaidia
kupata watoto tutakaowasomesha, tutakaowalisha na kuwahudumia vizuri. Serikali yetu inatoa
elimu bure lakini fikiria mzazi kama mwakani utakuwa na watano, hata kama
hutatoa ada na michango mingine utakuwa na mzigo kuwahudumia watoto hao ili
kuhakikisha wanapata mahitaji yote muhimu” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka ametoa
wito kwa wananchi, viongozi wa dini na
mashirika ya yasiyo ya kiserikali kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa
miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na vyumba vya madarasa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Vumi Magoti amewataka wananchi
wa Wiaya hiyo kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kadri itakavyokuwa
imepangwa na Kamati za Maendeleo za Vijiji na Kata ili kukabiliana na upungufu uliopo
kwa sasa.
Wakati huo huo Mkuu huyo
wa Mkoa amewataka wanachi kulima mazao yanayostahilimili ukame hususani mihogo,viazi na mtama na yale
yanayokomaa kwa muda mfupi kwa kuwa hakutakuwa na mvua za kutosha, ambapo
amesisitiza kila mtu ahakikishe analima ili apate chakula kwa sababu chakula
cha msaada hakitakuwepo.
Sanjari na hilo
amewataka wananchi kulima pamba na mazao ya mikunde hususani dengu , mbaazi,
choroko na mbaazi ambayo Serikali imewahakikishia wananchi soko
la uhakika kutoka nchini India.
Mtaka ameongeza kuwa
Viongozi wa wilaya ya Busega wahakikishe wanawasaidia na kuwasimamia wananchi
katika kufanya shughuli za kilimo cha umwagiliaji na ufugajii wa samaki kwa
kutumia vizmba kutokana na uwepo wa Ziwa victoria.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
alifanya ziara wilayani Busega jana, ambapo alizungumza na wananchi na kuchangia
mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa madarasa katika shule
ya Msingi Fogofogo na Shule ya Sekondari Kabita zote za kata ya Kabita wilayani
humo.
0 comments:
Post a Comment