Na Stella Kalinga
Halmashauri
wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu imeandaa mpango
mkakati wa kuboresha kilimo cha pamba , mahindi na mtama kwa lengo la kuwawezesha
wakulima kuzalisha mazao mengi na yenye ubora kwa kufuata kanuni za kilimo
bora.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg.Fabian Manoza alipozungumza
na wananchi wa Kata ya Mwanhuzi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika jana, katika
kituo cha mabasi cha mjini Mwanhuzi,, wakati wa Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka wilayani humo.
Manoza
amesema wakulima wengi wamekuwa wakizalisha pamba kwa kutofauata kanuni za
kilimo bora hali inayopelekea kupata mavuno hafifu ya kilo 300 kwa heka moja
wakati endapo watalima kitaalam wanaweza kupata kuanzia kilo 1000 kwa heka
moja.
“Pamba
tunayozalisha sasa hivi, mkulima ukijitahidi unavuna kilo 300 kwa heka moja lakini
ikitunzwa vizuri, ukatumia mbegu nzuri unaweza
kupata kilo 1000. Sisi kama viongozi tuliopewa dhamana Lazima tuwapeleke
wakulima wetu huko, sasa tumeanza kwa kuanzisha mafunzo ya kilimo bora cha
pamba,kata zote vijiji vyote mafunzo ambayo yataenda sambamba na matumizi ya mbegu bora ya
UKM08, tuachane na matumizi ya mbegu
za kienyeji.”, alisema Manoza.
Manoza
amesema Halmashauri yake imekusudia kufikia mwaka 2019 wakulima wote wilayani
humo watumie mbegu bora za pamba na kutumia mbinu za kisasa za kilimo ili wafikie
azma ya kuzalisha kilo 1000 kwa heka.
Mkurugenzi
huyo ameongeza kuwa kuanzia tarehe 19 Disemba,2016 yeye pamoja na wakuu wote wa
idara wataenda vijijini kwa ajili ya kufungua mashamba darasa ya pamba, mahindi
na mtama, hivyo akaagiza Maafisa Watendaji wa kata zote wafike Ofisini kwake
kwa ajili ya kuchukua mbegu za mashamba darasa hayo.
Kwa
upande wa kilimo cha mahindi Mkurugenzi huyo amesema kwa kuwa Jimbo la Kisesa
limekuwa likipata mvua za kutosha ikilinganishwa na jimbo la Meatu, wamekusudia
kuwasaidia wananchi wa Kisesa kulima mahindi kwa kufuata mbinu za kisasa ili
wapate chakula cha kutosha na ziada, kwa ajili ya biashara.
Manoza
amesema kwa kuwa Jimbo la Meatu limekuwa likipata mvua kidogo Halmashauri
imesaini mkataba na Mwekezaji Saimon Group ambaye atafanya kilimo cha mkataba
na wakulima, ambapo atatoa mbegu bora za
mtama na kutoa mikopo kwa wakulima kwa asilimia 100 ili kuwawezesha kutekeleza
kilimo cha mtama.
Kufuatia
kuwepo kwa mkakati huo ifikapo Disemba 2017 Halmashauri imekusudia kuyaongezea thamani mazao ya
mahindi na mtama kwa kujenga kiwanda cha kuchakata unga wa mahindi katika kata ya
Mwandoya (Jimbo la Kisesa) na Kiwanda cha kuchakata unga wa mtama katika kata
ya Jija (Jimbo la Kisesa) ambao utauzwa ndani na nje ya Simiyu.
Akiunga
mkono mkakati huo wa kilimo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka
amewahimiza wananchi kulima pamba kwa kuwa Serikali mkoani humo kwa
kushirikiana na wadau wengine imejipanga kuanza kujenga viwanda vya bidhaa za
afya zitokanazo na pamba mwaka 2017, ambazo ni pamba za hospitali, bandeji,
pamba za masikio, pampasi za watoto na
pedi za wanawake, hali itakayoliongezea thamani zao la pamba, kwa kuwa
litahitajika kwa wingi.
Aidha, Mtaka amewataka wananchi kutunza
akiba ya chakula waliyonayo pamoja na kulima mazao yanayostahimili ukame na yale
yanayokomaa kwa muda mfupi kwa kuwa, kwa
mujibu wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini mwaka 2017 hautakuwa na mvua za kutosha na hakutakuwa
na chakula cha msaada.
Naye
Mkuu wa wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt.Joseph Chilongani amesema Serikali wilayani
humo kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba imeichagua kata ya Mwabusalu kuwa kituo
cha kuzalisha mbegu bora, hivyo wananchi wategemee kupata mbegu bora
itakayowazesha kupata mavuno bora.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, amefanya ziara wilayani Meatu kukagua maendeleo ya ujenzi wa
miundombinu ya elimu hususani ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambapo ameunga mkono
juhudi za Serikali na wananchi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuchangia
mifuko 120 ya saruji.
Katika
ziara hiyo pia amezungumza na wananchi
wa wilaya hiyo kupitia mkutano wa hadhara ambapo alipata fursa ya kusikiliza
kero mbalimbali kutoka kwa wananchi, ambapo kero nyingi ziliigusa Idara ya
Ardhi. Baada ya Mkuu wa Mkoa kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na Idara ya
Ardhi, alitoa siku 14 kwa wananchi kupeleka kero zao kwa Mkuu wa Wilaya na
akaahidi kufanya mkutano wa hadhara tena kwa tarehe itakayopangwa na Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya, akiwa na timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Mkoa ili kutatua kero
za wananchi hao.
Baadhi ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa ushirikiano wa Serikali na Wananchi katika Shule ya Msingi Mshikamano wilayani Meatu. |
0 comments:
Post a Comment