Na
Stella Kalinga
Serikali Mkoani Simiyu
imetangaza Kilimo cha Umwagiliaji kuwa kipaumbele cha mwaka 2017 hususani
kilimo cha Mpunga wilayani Busega.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Anthony Mtaka katika kikao maalum kilichofanyika jana kati ya
uongozi wa mkoa huo, uongozi wa wilaya ya Busega, Maafisa Watendaji wa Kata
pamoja na Maafisa Ugani wa Wilaya na wa Kata.
Mtaka amesema katika
kutekeleza azma ya Kilimo cha umwagiliaji kuwa kipaumbele mwaka 2017 wilayani
Busega , Serikali itawahahamasisha wananchi kulima mpunga na kuhakikisha kuwa
maji na miundombinu ya umwagiliaji inawafikia katika mashamba yao kwa kadri ya
utaratibu utakaowekwa.
Mtaka ameongeza kuwa kufuatia
kuwepo kwa taarifa ya kutokuwa na mvua za kutosha mwaka 2017 wananchi wamepata hofu ya mazao yao
kukauka , hivyo Serikali imekusudia kuwatoa wananchi hofu hiyo kwa
kuwahakikishia kuwa itawawezesha kupata maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya
kumwagilia mashamba yao.
Aidha, Mkuu huyo wa
Mkoa amesema Wilaya ya Busega ni wilaya ambayo wananchi wake wanaweza kulima
kwa kipindi cha mwaka mzima kwa kuwa ina uhakika wa maji, hivyo Serikali
imekusudia wananchi walime mpunga kwa misimu isiyopungua miwili kwa mwaka.
“Niko tayari kufanya
ziara kila kijini hapa Busega ili nizungumze na wananchi, niwatoe hofu ya waliyo
nayo juu ya mazao yao kukauka kutokana na kukosa mvua, maana Serikali itawapelekea
maji” amesema Mtaka.
Pamoja
na kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa maji Serikali ya Mkoa kwa
kushiriakiana na Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi itawasaidia wananchi kupata
mbegu bora ya mpunga ambayo itawawezesha kupata mavuno mengi na bora kuanzia gunia
35 hadi 40 za mpunga kwa heka moja.
Sambamba na hilo Mtaka
amesema katika kutekeleza mkakati wa Kilimo
cha Umwagiliaji kama Kipaumbele; wananchi, serikali na wadau wengine wa kilimo
kila mmoja atakuwa na wajibu na majukumu yake ili makakati huo utekelezwe kwa
tija, ambapo amesema yapo majukumu yatakayofanywa na wananchi, mengine
yatafanywa na Serikali (Halmashauri /Wizara ya Kilimo) , Viongozi na mengine
yatatekelezwa na wadau.
Naye Katibu Tawala wa
Mkoa huo, Ndg.Jumanne Sagini amesema Serikali ya Mkoa itaunda kikosi kazi cha
Wahandisi wa Kilimo na Umwagiliaji kutoka Halmashauri zote za Mkoa huo, ambao
watapaswa kuandaa mpango kazi na wajibu wa kila mdau katika utekelezaji wa
mradi huo, kabla ya Januari Mosi, 2017.
Sagini amesema Wataalam
hao kwa kushirikiana na watalaam wa Wilaya ya Busega watapaswa kukaa pamoja na
kuandaa mpango kazi utakaobainisha mipango ya muda mrefu na ya muda mfupi,
ambayo itapelekea kutekelezwa kwa mradi wa kilimo cha umwagiliaji kwa tija na matokeo chanya kwa wananchi.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Busega Mhe. Mickness Mahela akizungumza kwa
niaba ya Mwenyekiti, amesema madiwani
wote wa wilaya hiyo watatoa ushirikiano na kuhakikisha mpango huo wa kilimo cha
umwagiliaji unafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuwasaidia wananchi.
Mkuu wa Mkoa anatarajia
kuanza ziara ya siku sita wilayani Busega kuanzia Januari 03 hadi Januari 09,
2017 kwa lengo la kuzungumza na wananchi juu ya kilimo cha umwagiliaji kupitia
mikutano ya hadhara, ambapo ameagiza taarifa ya mikutano hiyo zitolewe katika
nyumba za ibada, kwenye mbao za matangazo za Vijiji na kata na gari la
matangazo litumike ili wananchi wote wapate taarifa.
0 comments:
Post a Comment