Na Stella Kalinga
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka ametoa tamko la Mapinduzi ya Elimu na
mwelekeo wa Elimu mwaka 2017 kama kipaumbele cha kwanza kwa mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa tamko hilo katika
kikao maalum cha viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika mjini Bariadi kwa lengo la kujadili dira ya maendeleo ya Mkoa huo.
Tamko
hilo linamtaka kila Mwalimu Mkuu, Mtendaji wa Kijiji, Mtendaji wa Kata
kuhakikisha ifikapo tarehe 05 Januari, 2017 awe amebandika majina yote ya
watoto wanaoanza awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza tarehe 09
Januari, 2017.
Mtaka
amesema tangu Serikali ya awamu ya tano ilipotangaza elimu bila malipo Mkoa wa
Simiyu umepokea takribani kiasi cha shilingi 2,841,356,000/= kwa wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari, hali iliyowapunguzia mzigo wazazi.
Mtaka
amesema wajibu wa wazazi ni kuhakikisha kila mtoto anapelekwa shule tarehe 09
Januari, 2017 shule zitakapofunguliwa, ambapo amesema wazazi wote ambao
hawatawapeleka watoto wao shule watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja
na kuwa vibarua wa kudumu watakaofanya usafi katika Taasisi za Umma.
“Wazazi
wote ambao hawatawapeleka watoto shule wajiandae kuwa vibarua wa kudumu wa
Serikali, hao ndiyo watakaosafisha masoko, vituo vya polisi, hospitali, vituo
vya afya wengine watadeki hata madarasa na maeneo mengine ya Serikali. Nimeamua
kuongea mbele yenu viongozi ili ujumbe huu muwafikishie wananchi, lakini pia nimekuwa
nikizungumza na wananchi kila ninapofanya mikutano ya hadhara”, amesema Mtaka.
Pamoja
na tamko hilo ameelekeza mambo muhimu yaliyoamuriwa kupitia vikao ya kisheria
na kimaamuzi kama Vikao vya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC),Kamati za Ushauri
za Wilaya(DCC), Mabaraza ya Madiwani, Vikao vya Maendeleo ya kata (WDC) na
mikutano ya vijiji yatekelezwe ambayo ni kukamilisha madawati Desemba
2016,kukamilisha ujenzi wa madarasa ifikapo Januari 30, 2017.
Maelekezo
mengine ni pamoja viongozi wote kugawana na kusimamia madarasa yote ya mtihani (darasa
la nne, darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na kidato cha sita), Shule
zote kutumia chaki za Maswa, Madarasa ya Mitihani kufanya mazoezi ya kila siku
asubuhi saa 1:30 2:00 asubuhi, na kuwepo
kwa makambi ya kielimu kwa shule, kata, Wilaya na Mkoa katika siku za mwisho za
juma, mapumziko ya kati na mwisho wa mihula.
Naye
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu,Ndg.Jumanne Sagini amewataka Watendaji wote
Serikali kuhakiksha kuwa wanafanyia kazi maelekezo yanayotolewa na viongozi wa
mkoa huo ili kutekeleza dira ya maendeleo ya Mkoa kwa kuzingatia sheria, kanuni
na taratibu.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa amesema katika utekelezaji wa Kauli mbiu ya Mkoa huo ya “Wilaya
Moja Bidhaa Moja”baada ya wilaya ya Maswa kuzalisha chaki, Wilaya ya Meatu
kusindika maziwa Mkoa umejipanga kuanzisha kilimo cha Umwagiliaji wilayani
Busega mwaka 2017.
Mtaka
amesema Katibu Tawala Mkoa ameunda kikosi kazi cha Wahandisi wa kilimo
watakaosaidiana na watalaam wa Busega kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa
kilimo cha Umwagiliaji hususani kilimo cha mpunga kwa misimu miwili au zaidi ili wananchi wa Busega
wanufaike kwa kuwa na maji ya Ziwa Victoria.
Pamoja
na kilimo cha umwagiliaji Mtaka amewataka wananchi wa Mkoa wa Simiyu kulima
mazao yanayokomaa muda mfupi na yanayostahimili ukame kama mtama, muhogo na
viazi kutokana na taarifa kuwa mwaka 2017 hautakuwa na mvua za kutosha.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Lamadi wilayani Busega, Mhe.Laurent Bija amesema ili
wilaya hiyo iweze kuzalisha chakula cha kutosha mkoa mzima na ziada kwa ajili
ya kuuza kupitia mradi wa kilimo cha
umwagiliaji, mkoa unapaswa kuwa na mpango mkakati wa kudumu kwa lengo la
kuufanya mradi huo kuwa endelevu.
Naye
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu,Mhe.Gimbi Masaba ametoa wito kwa viongozi
wa mkoa huo kuwajibika ipasavyo katika shughuli za maendeleo ya wananchi bila
kujali tofauti zao za kisiasa.
Kikao
cha Viongozi na Wadau wa Maendeleo Mkoani Simiyu kimewahusisha Viongozi wa
Serikali Ngazi ya Mkoa, Wilaya,Wabunge, Madiwani, Watendaji wa Sekretarieti ya
Mkoa na Halmashauri, Viongozi wa CCM ngazi ya Mkoa na wilaya,viongozi wa Vyama
vingine vya siasa na wadau wengine.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza na viongozi na wadau wa maendeleo wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao cha kujadili dira ya maendeleo ya Mkoa mwaka 2017. |
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza na viongozi na wadau wa maendeleo wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao cha kujadili dira ya maendeleo ya Mkoa mwaka 2017. |
Katibu Mkuu wa CCM Mkoa
wa Simiyu, Joyce Masunga (wa pili
kulia) akizungumza katika kikao cha
Viongozi na Wadau wa Maendeleo wa Mkoa huo kilichofanyika jana ukumbi wa
Bariadi Alliance mjini Bariadi.
|
Diwani wa Kata ya Lamadi, Mhe.Laurent Bija akichangia katika kikao cha viongozi na wadau wa Maendeleo ya Mkoa wa Simiyu katika kikao kilichofanyika jana ukumbi wa Bariadi Alliance mjini Bariadi |
Diwani wa Kata ya
Lingeka wilayani Meatu akichangia hoja katika kikao cha viongozi na wadau wa Maendeleo ya
Mkoa wa Simiyu katika kikao kilichofanyika jana ukumbi wa Bariadi Alliance
mjini Bariadi.
|
Baadhi
ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu walioshiriki kikao cha viongozi na wadau wa
Maendeleo ya Mkoa huo kilichofanyika jana ukumbi wa Bariadi Alliance mjini Bariadi. |
0 comments:
Post a Comment