Na Stella Kalinga
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhia kununua na kutumia chaki zinazotengenezwa na Vijana wa Maswa Family
kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya
ya Maswa Mkoani Simiyu ili zitumike
katika shule zake Msingi na Sekondari.
Kauli
ya hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe.Riziki Pembe Juma alipotembelea kiwanda cha
kutengeneza chaki na kujionea namna vijana wa Maswa Family wanavyojishughulisha
na utengenezaji wa chaki hizo wilayani humo.
Ziara hiyo ya Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Amali wa Zanzibar Mkoani Simiyu, imefanyika kufuatia ahadi
ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt.Ali Mohamed
Shein aliyoitoa wakati wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 ya
kumtuma Waziri huyo Mkoani Simiyu kuona namna uzalishaji wa chaki unavyofanyika
na kuweka utaratibu wa Zanzibar inavyoweza kununua chaki hizo.
Mhe.Riziki amewataka kuendesha
kiwanda hicho kwa ubunifu na kukifanya kuwa endelevu ili kuendana na kasi ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli katika
kutekeleza kwa vitendo sera ya Tanzania ya Viwanda.
Aidha, Mhe. Riziki ameihakikishia
Serikali mkoani Simiyu kuwa Wizara yake itashirikiana na Mkoa huo katika
masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya elimu na akaahidi kuwa wizara yake pia
itakuwa balozi wa Chaki za Maswa visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema suala la ushirikiano wa kibiashara
uliofanyika juu ya Chaki za Maswa (MASWA CHALKS) kati ya Mkoa wa Simiyu na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ni jambo la
kihistoria, la kipekee ambalo limeonesha kuwa Serikali ya Zanzibar inathamini na
kuunga mkono juhudi za mkoa huo katika kuinua uchumi wake na Taifa kwa ujumla.
“ Tunamshukuru sana Rais
wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein kwa heshima aliyotupa viongozi na
wananchi wa mkoa wa Simiyu, kwa kutekeleza ahadi yake ya kumtuma Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali kuja kuona utengenezaji wa chaki Maswa na kuweka makubaliano
ya matumizi ya chaki hizo Zanzibar naahidi hatutamuangusha, tutatekeleza jambo
hili kwa ushirikiano mkubwa” amesema Mtaka.
Mtaka amesema pamoja na
kutengeneza Chaki wilayani Maswa, kusindika maziwa Wilayani Meatu mkoa huo
umejipanga kuzalisha bidhaa zote ambazo malighafi yake inapatikana hapa nchini
na kuyaongezea thamani mazao yote katika wilaya zote za Mkoa huo chini ya Kauli
Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja”.
Mtaka amewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kupenda na
kuthamini bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuachana na dhana kuwa bidhaa
bora ni zile zinazotoka nje ya nchi chini ya Kauli Mbiu “Buy Tanzania Watanzania tupende
vya Kwetu”
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa, Ndg.Peter
Bunyongoli amesema Ziara ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu ni
ishara ya umoja ambao ni njia mojawapo ya kudumisha Muungano, ambapo
aliwashauri viongozi wenye dhamana katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuenzi Muungano huo.
Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Mhe.Riziki Pembe Juma
amefanya ziara ya siku moja Mkoani Simiyu ambapo alitembelea kiwanda cha chaki
Maswa na kufungua nyumba ya walimu moja ambayo wataishi watu sita (six in one)
kwa wakati mmoja , vyumba vya madarasa viwili na choo cha walimu matundu mawili
(02) ya vyoo katika Shule ya Sekondari ya Jija.
0 comments:
Post a Comment