Na Stella Kalinga
Serikali Mkoani Simiyu imedhamiria kwa mwaka 2017
kutatua na kuondoa migogoro yote ya ardhi ambayo imekuwa
ikijitokeza mara kwa mara kwa wananchi wa mkoa huo.
Akitoa ufafanuzi wa namna ya kutatua kero hiyo wakati wa mkutano
wake na wananchi wa jimbo la Meatu ,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony
Mtaka alisema kuwa amechoshwa kusikia na kuona migogoro ya ardhi inayojitokeza
ndani ya mkoa wake, hivyo mwaka 2017 ndio utakuwa mwisho wa kero hizo.
Mtaka amesema kuwa kamwe hawezi kukubali kuona migogoro hiyo
inaendelea hivyo wananchi na watendaji wa idara ya ardhi wanapaswa kila mmoja
ajue utaratibu sahihi wa utoaji na ununuaji wa ardhi ili kuepusha sintofahamu
zinazojitokeza.
“ mwaka huu wa 2017 ni mwaka ambao mimi mkuu wa Mkoa wa Simiyu
nimeamua kusimamia ,kusikiliza na kutatua kero zote za ardhi…nataka ndani ya
kipindi hichi ifikie mahali migogoro ya ardhi kwa mkoa wa Simiyu inakuwa sio
kipaumbele chetu…Mtaka.
Aidha, Mtaka alieleza kuwa anataka watendaji wa idara ya ardhi kuhakikisha
wanafanya kazi zao kwa umakini na kuweka kumbukumbu za kimaandishi katika kila
mgogoro unaotatuliwa kwani kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakiibua mgogoro hiyo
upya pindi kunapotokea mabadiliko ya viongozi katika maeneo yao.
Sambamba na hilo pia amewataka wananchi wote wa mkoa wa Simiyu kutovamia
maeneo ya Taasisi za Serikali na endapo wapo ambao wako ndani ya maeneo hayo
waondoke mara moja kabla serikali haijawachukulia hatua za kisheria ikiwa ni
pamoja na kubomolewa kwa nyumba zao.
Hata hivyo katika kikao hicho kulibainika kuwepo na tatizo la
watendaji wa ardhi kutoa umiliki wa kiwanja kimoja kwa zaidi watu wawili hali
ambayo inasababisha mgongano mkubwa baina ya wananchi hao, ambapo wananchi wote
walioonekana kupata tatizo hilo waliahidiwa kupewa viwanja mbadala na
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
Michael Stephano mkazi wa Meatu amesema kuwa amefurahishwa sana na mfumo wa
mkuu wa Mkoa kusikiliza kero za wananchi , kwani kwa kufanya hivyo wananchi
watapata haki zao stahiki ambazo hapo awali walikuwa hawazipati.
“tunamshukuru sana mkuu wa Mkoa wetu…kitendo anachokifanya kwa kweli
kimetupa nguvu ya kujua wapi tunapata haki zetu pale tunapoona tumeibiwa haki
hiyo…sambamba na hilo ametusaidia mwongozo na kutatua kero za ardhi na
ninaamini mpaka kuisha mwaka huu kero nyingi zitakuwa zimeisha…Alisema
Stephano.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum mkoa
wa Simiyu, Mhe.Leah Komanya amewataka Watumishi wa Idara ya ardhi kuzingatia
sheria na taratibu kila wanapotwaa, kuuza, kuthamini au kupima ardhi kwa sababu kitendo cha kutofuata sheria na
taratibu kwa watumishi hao kimekuwa chanzo cha migogoro mingi ya ardhi.
Wakti huo huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka amemtaka Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Ndg.Fabian Manoza kuchunguza tuhuma
zilizotolewa na wananchi dhidi ya viongozi wa Vijiji na Vitongoji juu ya
kutumia maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa yajulikanayo kama HASHI (Hifadhi Ardhi
Shinyanga) kwa manufaa yao, na watakaobainika wachukuliwe hatua.
Mtaka amesema kwa kuwa wilaya hiyo inatarajia kuanzisha mradi wa ufuagaji
bora wa ng’ombe wa kisasa, maeneo yote ya HASHI yatumike kupanda majani ya
malisho kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji kupata malisho hasa wakati wa kiangazi.
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Meatu kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kituo cha Mabasi cha Mjini Mwanhuzi kwa
lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
0 comments:
Post a Comment