Wednesday, January 18, 2017

KAMATI YA ULINZI NA USALAMA MKOA WA SIMIYU YAKUTANA NA UONGOZI WA TBA JIJINI DAR ES SALAAM

Na Stella Kalinga
Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa wa Simiyu ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni  Mkuu wa mkoa huo Mhe.Anthony Mtaka  imekutana na kufanya kikao na uongozi wa Wakala wa Majengo (TBA) leo jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimefanyika kutekeleza la agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli alilolitoa wakati wa Ziara yake Mkoani Simiyu la kuitaka kukutana na TBA ili kuona utaratibu wa kujenga Hospitali ya Mkoa kwa gharama ya shilingi bilioni 10 badala ya shilingi  Bilioni 46 za awali.

Mtendaji  Mkuu wa Wakala wa Majengo(TBA), Elius A. Mwakalinga  amesema baada ya kupata taarifa ya gharama ya shilingi bilioni 46 za ujenzi wa Hospitali zilizoandaliwa na TBA Mkoa wa Simiyu ambazo hazikuungwa mkono na Mhe.Rais,  ameunda timu ya wataalam itakayochunguza gharama hiyo , wakati huo wote Meneja wa TBA Mkoa wa Simiyu,QS.Michael Semfuko atarejeshwa kwanza makao makuu kupisha uchunguzi huo.

Mwakalinga amesema baada ya timu hiyo kuhakiki gharama za awali itatumwa timu nyingine itakayopitia upya michoro ya hospitali na kuandaa utaratibu wa kujenga hospitali hiyo kulingana  na fedha alizoahidi kutoa Mhe.Rais.

Mtendaji huyo  Mkuu wa TBA ametoa wito kwa Taasisi za Umma kuitumia TBA katika ujenzi wa Majengo yao kwa kuwa inawataalamu wengi wenye sifa  na inajenga kwa gharama nafuu ikilinganishwa na wakandarasi wengine.

Katika kikao hicho Mkuu wa mkoa amesema Uongozi wa mkoa unamshukuru Mhe.Rais kwa ahadi yake ya kutoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mkoa na akaomba Wakala wa Majengo kujenga hospitali hiyo  kwa viwango vinavyotakiwa ndani ya muda utakaopangwa ili iwe mfano kwa mikoa mingine ambayo bado haijajenga Hospitali za Mikoa.

“Kama mmeweza kujenga mabweni 20 kwa shilingi bilioni 10 ndani ya miezi sita naamini mnaweza kujenga hospitali yetu ya mkoa ndani muda mfupi pia;tunataka kabla mate ya Mhe.Rais hayajakauka  tumuombe aje azindue Hospitali ya mkoa wa Simiyu na mmenihakikishia mtaweza” amesema Mtaka.

Aidha, Mtaka ametoa wito kwa Mtendaji mkuu wa TBA na wataalam pamoja na kujenga majengo ya Taasisi za Serikali kwa gharama nafuu,  wasiogope kujenga nyumba za watumishi kwa gharama nafuu hususani katika maeneo ya pembezoni ili watumishi waweze kununua nyumba hizo.

Mtaka ameongeza kuwa kuna baadhi ya mashirika na Taasisi nyingine za umma zimekuwa zikitangaza kuwa zinajenga nyumba  za gharama nafuu lakini watumishi wengi ambao ndio walegwa hawamudu gharama za nyumba hizo.

“  Msiogope kujenga nyumba za watumishi katika Halmashauri, kuna wastaafu na watumishi wengi wa umma wanaweza kupanga na kununua nyumba hizo, TBA jipambanueni kama Taasisi pekee ya Serikali inayojenga majengo ya Serikali,nyumba za watumishi kwa viwango bora na gharama nafuu”amesema Mtaka.

Sanjali na hilo Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa wake unajipambanua kuwa mkoa kiongozi katika kuzalisha bidhaa zote ambazo malighafi yake yanapatikana hapa nchini chini ya Kauli mbiu yake ya Wilaya moja Bidhaa Moja”


Pamoja na kikao hicho Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu imepata fursa ya kutembelea na kuona mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyumba za watumishi ambazo zinajengwa na Wakala wa Majengo(TBA) katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi na Watendaji wa Wakala wa Majengo (TBA) pamoja na Wajumbe wa Kamati yake ya Ulinzi na Usalama katika kikao kilichofanyika Makao makuu ya TBA jijini Dar es Salaam leo
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Bw. Elius A.Mwakalinga akizungumza na viongozi na Watendaji wa Wakala wa Majengo (TBA) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Simiyu katika kikao kilichofanyika Makao makuu ya TBA jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya Wataalam na Watendaji wa TBA makao makuu, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Simiyu,Wataalamu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani)  katika kikao kilichofanyika Makao makuu ya TBA jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Makao makuu ya TBA jijini Dar es Salaam leo.

Baadhi ya Wataalam na Watendaji wa TBA makao makuu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Makao makuu ya TBA jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya Wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Makao makuu ya TBA jijini Dar es Salaam leo, kutoka kushoto Kaimu Mganga Mkuu,Oscar Tenganamba,Mhandisi Mkuu wa Ujenzi,Deusdedit Mshuga na Mchumi, Proaches Tumain.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Bw. Elius A.Mwakalinga akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Simiyu walipotembelea na kuona ujenzi wa mabweni 20  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyojengwa na TBA kwa gharama ya shilingi bilioni 10. 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Bw. Elius A.Mwakalinga akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Simiyu walipotembelea na kuona ujenzi wa mabweni 20  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyojengwa na TBA kwa gharama ya shilingi bilioni 10.

Baadhi ya mafundi wakiendelea na ujenzi wa mabweni 20  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyojengwa na TBA kwa gharama ya shilingi bilioni 10.
Mtendeji Mkuu wa Wakala wa Majengo (TBA), Bw. Elius A.Mwakalinga akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Simiyu walipotembelea na kuona ujenzi wa nyumba za watumishi zilizojengwa na TBA kwa ajili ya kuwauzia watumishi wa umma.
Baadhi ya nyumba zilizojengwa na TBA kwa ajili ya kuwauzia watumishi wa umma





0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!