Na Stella Kalinga,
Serikali Mkoani
Simiyu imewashauri wakulima wote wilayani Busega wenye mashamba yaliyo karibu na ziwa Victoria kuorodhesha
jumla ya ekari za mashamba waliyonayo ili waweze kusajiliwa na kuingizwa katika
mpango wa kilimo cha umwagiliaji
kinachotarajiwa kuanza mapema mwaka huu.
Ushauri huo umetolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka katika ziara yake maalum ya kuwatembelea
wananchi wa vijiji vilivyopo kandokando ya ziwa
Victoria Wilayani Busega, ambapo ameanza na vijiji vya Nyamikoma na
Nyakaboja kata ya Kabita.
Mtaka alisema endapo
wakulima watakuwa tayari kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa kufuata ushauri wa kitaalamu na kutumia mbegu bora
watapata mazao mengi yatakayokubalika katika soko la ndani na nje ya Mkoa ikiwa
sambamba na na kujikwamua kiuchumi.
Alieleza kuwa lengo la serikali ya Mkoa ni kuhakikisha
dhana ya mapinduzi ya kilimo kwa mfumo wa umwagiliaji inatekelezwa kwa vitendo
kwa kuwapatia elimu ya kitaalamu wakulima ili waweze kuzalisha mazao bora na
mengi yanayotosheleza soko la ndani ya nchi na kupunguza uagiziaji mazao nje ya
Mkoa.
“Tumekuja kama
mkoa kuzungumza na wananchi ili wale watakaokuwa tayari waanze kutekeleza. Ni
lazima tufanye maamuzi ya kufanya mapinduzi ya kilimo kama watu tulio kandokando
ya ziwa Victoria ili uwepo ziwa utunufaishe” amesema Mtaka.
Aidha alifafanua kuwa
kilimo hicho katika maeneo ya Wilaya ya Busega kitahusisha mazao ya Mpunga, mboga mboga, mahindi na
mazao jamii ya mikunde, hivyo wakulima kwa kushirikiana na Serikali wanatakiwa
kuendelea kubuni mbinu mbalimbali za
uzalilishaji mazao hayo kwa wingi ili kwenda sambamba na fursa ya masoko ya
ndani na nje ya nchi hasa kwa mazao ya mikunde.
Mtaka ameongeza kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi imetoa fedha katika Taasisi
za fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo, hivyo akawashauri wananchi kujiunga
katika vikundi ili iwe rahisi kuwatambua na kuwawezesha kwa pembejeo na
miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji
kulingana na makubaliano yatakayowekwa.
Hata hivyo Mkuu huyo
wa Mkoa amewasihi vijana nchini kujiajiri wenyewe kupitia kilimo hicho kwa
lengo la kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira badala ya kukimbilia
mijini wakati fursa za kujiajiri zipo nyingi vijijini.
Kwa upande wake
Mkulima wa kilimo cha mpunga Charles Malombo kutoka katika kijiji cha Nyakaboja alisema licha ya serikali kuwa na
mpango mzuri kwa kuwapatia matumaini makubwa ya mafanikio katika kilimo cha
umwagiliaji bado wanahitaji msaada wa kitaalamu utakaowasaidia kutumia
teknolojia ya kisasa katika umwagiliaji maji ya ziwa Victoria ili waweze kupata mazao mengi zaidi ya
wanayopata kwa sasa.
Naye Samuel Chochomo
ambaye ni Mkulima wa mazao mbali mbali ya Mboga mboga alikiri kilimo hicho
ndicho kitakachowatoa wakulima na wananchi katika janga la njaa
Alieleza kuwa kilimo cha kutumia teknolojia ya umwagiliaji maji ni kizuri
na hakitegemei msimu wa mvua, wakulima wanaweza
kulima wakati wote kama wakiwa na miundombinu
mizuri ya upatikanaji wa maji kutoka Ziwani na mipira imara ya kusambazia maji.
Wilaya ya Busega ni wilaya pekee Mkoani Simiyu iliyo na maji ya uhakika ya Ziwa Victoria na ina eneo la takribani ekari 7200 zinazofaa kwa kilimo ch umwagiliaji.
0 comments:
Post a Comment