Na
Stella Kalinga
Benki ya NMB imesema
iko tayari kutoa mkopo kwa ajili ya kufanikisha kutekelezaji wa mradi wa Kilimo
cha Umwagiliaji unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu katika wilaya ya Busega
Mkoani Simiyu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa
Idara ya Kilimo Biashara wa Benki wa Benki ya NMB, Bw. Saif Ahmed katika kikao
Maalum kilichofanyika Makao makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam kati ya
Uongozi wa Benki hiyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu
ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Anthony Mtaka.
Mtaka amesema kwa kuwa
wilaya ya Busega ina maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria serikali imedhamiria
kukifanya kilimo cha umwagiliaji kuwa kipaumbele kwa mwaka 2017 ambapo
itawasaidia wakulima katika upatikanaji wa miundombinu ya maji na pembejeo za
kilimo.
Mtaka ameongeza kuwa
kutokana na Benki ya NMB kuwa na fedha za kusaidia shughuli za kilimo kupitia Dirisha
la Kilimo, uongozi wa mkoa wa Simiyu
unaomba Benki hiyo kuona namna itakavyosaidia mafanikio ya utekelezaji wa mradi
wa kilimo cha umwagiliaji.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo imekusudia kuwatoa wananchi
katika fikra za kulima kwa ajili ya chakula pekee na kuboresha kilimo kwa kulima kibiashara.
“Tunataka kutengeneza ‘model’
yetu katika kilimo cha umwagiliaji ili wananchi wetu walime kibiashara, wenzetu
kwenye maeneo mengine wanafanya na wamefanikiwa na sisi tufanye, kwa kuwa
tumedhamiria tutafanya” alisema Mtaka.
Akizungumza na viongozi
wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa Benki ya NMB Bw. Saif Ahmed benki iko tayari kuunga mkono
juhudi za mkoa wa Simiyu katika kilimo cha umwagiliaji Busega Mkoani humo,
ambapo amependekeza mradi huo ukatekelezwa kwa ushirika kati ya Benki
hiyo,Serikali na wananchi.
Naye Meneja Mwandamizi
Idara ya biashara za Serikali wa NMB Makao Makuu, Suzan Shuma Nguya, amesema
Benki hiyo itaunga mkono juhudi za Serikali ya Mkoa wa Simiyu katika
Utekelezaji wa mradi huo, wakiamini kuwa utakuwa mfano na kuwapa fursa kusaidia
utekelezaji wa miradi kama hiyo katika Halmashauri nyingine hapa nchini.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Busega Mhe.Vumi Magoti amesema atashirikiana na
viongozi wengine kuwahamasisha wananchi kuchimba mitaro itakayopelekea maji
mashambani kama sehemu ya moja ya mchango wao katika utekelezaji wa mradi wa
kilimo cha umwagiliaji.
Mkuu wa Mkoa na wajumbe
wote wa kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa wameahidi kuwaunga mkono wananchi
katika uchimbaji wa mitaro mara utekelezaji wa shughuli hiyo utakapoanza.
Katibu Tawala Mkoa wa
Simiyu,Ndg.Jumanne Sagini ameuomba uongozi wa NMB kuwaruhusu wataalam wao kushirikiana
na wataalam wa Mkoa huo katika ukamilishaji
wa andiko na utekelezaji wa mradi huo ili kuwasaidia wananchi wa Busega na
Simiyu kwa ujumla kuwa na usalama wa chakula na kujipatia fedha kwa kilimo
biashara.
0 comments:
Post a Comment