Na
Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka amewaongoza Watumishi wa Umma mkoani humo kutekeleza
agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Samia Suluhu
Hassan, la kufanya mazoezi kwa lengo la kukabiliana
na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari,shinikizo la damu, saratani
na magonjwa ya moyo.
Mazoezi hayo na michezo mbalimbali iliyowahusisha watumishi
kutoka Serikali kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na baadhi ya Taasisi nyingine
za Serikali yamefanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuanzia
saa kumi na mbili hadi saa 3:45 asubuhi.
Akifungua mazoezi hayo Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu amewataka watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kutekeleza
agizo la Mhe.Makamu wa Rais na kujenga
tabia ya kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.
Mtaka amesema Serikali
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ina mkakati wa kukarabati uwanja wa
Halmshauri ya Mji wa Bariadi na kuhakikisha kuwa viwanja vya michezo yote
ikiwepo mpira wa wavu, mpira wa kikapu, mpira wa pete, mpira wa miguu vinatengenezwa
vizuri ili watu wapate mahali pa kufanya mazoezi na kucheza michezo hiyo.
Mtaka ameongeza kuwa uwanja
wa Shule ya Msingi Somanda umeshatengenezwa na kuwekewa mahitaji yote muhimu
kwa ajili ya mchezo wa riadha, hivyo watumishi na wananchi wanaopenda mchezo wa
riadha watatumia uwanja huo.
Aidha, Mkuu huyo wa
mkoa ammetoa wito kwa Maafisa michezo na
Maafisa utamaduni Mkoani humo kuwa na mipango kazi itakayowawezesha kuhamasisha
na kusimamia uendeshaji wa shughuli za michezo ili uwe endelevu katika Mkoa.
“ Maafisa michezo na
Maafisa utamaduni msiishie kuaandaa michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA tu,
andaeni mipango kazi itakayoendeleza michezo; Afisa Michezo na Utamaduni Mji wa
Bariadi utumie uwanja huu kuandaa mabonanza ya michezo mbalimbali na burudani kutoka
vikundi vya ngoma vinavyotambulisha utamaduni wa huku, nina uhakika wananchi watapenda
kuona mambo hayo” amesema Mtaka.
Naye Katibu Tawala Mkoa
ametoa wito kwa watumishi wa Taasisi za Serikali ambazo hazikushiriki kufanya
mazoezi ya wiki ya pili ya mwezi huu kuungana pamoja na watumishi wengine wiki
ya pili ya mwezi Februari.
Michezo iliyochezwa leo baada ya kumaliza
mazoezi ni pamoja na mpira wa miguu(wanaume), kuvuta kamba(wanaume na wanawake),
kufukuza kuku(wanaume na wanawake na mbio za mita 100 kwa wanaume na wanawake.
Katika mpira wa miguu
timu ya watumishi wa Serikali kuu na Timu ya Watumishi wa Mamlaka za Serikali zimetoka
sare ya bila kufungana, kuvuta kamba wanaume Timu ya Sekretarieti ya mkoa
iliibuka kidedea dhidi ya Timu ya Halmashauri ya Wilaya na Mji Bariadi, wakati
kwa wanawake Timu ya Halmashauri iliiburuza timu ya Sektarieti ya Mkoa.
Katika mchezo wa kufukuza
kuku wanawake na wanaume, watumishi wa
Sekretarieti ya Mkoa waliwashinda watumishi wa Halmashauri ya mji Bariadi na Halmashauri
ya Wilaya ya Bariadi.
0 comments:
Post a Comment