Na
Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe.Anthony Mtaka ametoa miezi mitatu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kujenga
machinjio katika Kata ya Nyashimo ambayo ni makao makuu ya wilaya hiyo.
Mtaka ameyasema hayo
katika mkutano wa Hadhara uliofanyika Kijiji cha Bulima kata ya Nyashimo kwa
lengo la kuhamasisha mpango wa Kilimo cha Umwagiliaji pamoja na kisikiliza kero
za Wananchi na kuwapatia ufumbuzi wakati wa ziara yake wilayani humo.
Akijibu kero
iliyowasilishwa na Deusdedit Mushungu mkazi wa Nyashimo ambaye alieleza kuwa
wananchi wamekuwa wakitozwa ushuru wakati machinjio hayakidhi viwango, Mtaka
amesema kwa kuwa Halmashauri inakusanya ushuru kutoka kwa wafanyabiashara wa
nyama inapaswa kuboresha huduma ya machinjio na itakaposhindwa isiwadai wafanyabiashara
hao ushuru.
“ Idara ya mifugo
hakikisheni mnajenga machinjio ya Nyashimo, nawapa miezi mitatu kuanzia sasa
mkishindwa nitafuta ushuru kwa wananchi kwa kuwa mtakuwa mmeshindwa kutimiza
wajibu wenu kama Halmashauri” alisema Mtaka.
Afisa Mifugo wa
Halmashauri ya Wilaya Busega, Ndg. Albert Francis amesema Halmashauri imetenga
eneo kwa ajili ya kujenga machinjio ya kisasa katika kijiji cha Nyang’anga kwa kuwa
yaliyopo kwa sasa yamejengwa karibu na makazi ya watu.
Aidha, Afisa Mifugo
huyo aliongeza kuwa machinjio hayo kwa mwaka 2015/2016 yalikadiriwa kuchangia
shilingi 300,000/= kwa mwezi katika mapato ya Halmashauri na mwaka 2016/2017 yamekadiriwa kuchangia
shilingi 600,000/= mapato ambayo
hayajafikia kutokana na idadi ndogo ya wachinjaji(wafanyabiashara wa nyama).
Wakati huo huo Mkuu
huyo wa Mkoa akijibu ombi la wananchi wengi wa Nyashimo la kuletewa chakula cha
bei nafuu ili kukabiliana na upungufu wa chakula inayotokana na baadhi ya mazao
kukaua mashambani kutokana kukosa mvua za kutosha, amesema Serikali italifanyia
kazi na kuona namna ya kuwasaidia.
Mtaka amesema ufumbuzi
wa kudumu wa tatizo la upungufu wa chakula ni wananchi wa Wilaya ya Busega kuhamasika na kuanza kutekeleza Mpango wa
Kilimo cha umwagiliaji unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mapema mwaka 2017
wilayani humo kama kipaumbele, kwa kuwa kuna uhakika wa maji ya Ziwa Victoria.
Mtaka amesema endapo
wananchi wataonesha utayari wa kutekeleza mpango huu Serikali kwa kushirikiana
na wadau wengine itafanya utaratibu wa
kuwawezesha kwenye miundombinu ya umwagiliaji na pembejeo za kilimo zikiwemo
mbegu bora na mbolea kwa kadri watakavyokubaliana.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
yuko katika ziara ya siku 6 wilayani Busega ambapo anazungumza na wananchi
kuelimisha na kuhamasisha kuhusu mpango wa kilimo cha umwagiliaji na kujibu
kero mbalimbali za wananchi wa wilaya hiyo.
0 comments:
Post a Comment