Na
Stella Kalinga
Serikali Mkoani Simiyu
imeagiza Shule zote za Serikali Mkoani humo kuhakikisha kuwa ifikapo Januari 09
mwaka 2017 zinatumia Chaki zinazotengenezwa Wilayani Maswa.
Agizo hilo limetolewa
na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka wakati wa ziara yake
aliyoifanya wilayani Maswa kwa lengo la
kukagua ujenzi wa Miundombinu ya shule ikiwa
ni pamoja na vyumba vya madarasa.
“Kuanzia Januari 09
mwakani shule zitakapofunguliwa Wakuu wa Shule, Walimu wakuu na Wazabuni wanaofanya
kazi na shule za Serikali wahakikishe wananunua chaki zinazotengenezwa
na Vijana wa Wilaya ya Maswa. Haya ni maelekezo na hayajadiliki”, alisema
Mtaka.
Mtaka amewataka
Wananchi Mkoani Simiyu kujenga utamaduni wa kupenda na kuthamini vitu au bidhaa
zinazozalishwa hapa nchini.
Mkuu huyo wa mkoa
ameongeza kuwa Maono ya Serikali ya Mkoa ni kuzalisha bidhaa zote ambazo
malighafi yake yanapatikana hapa nchini na kubadili mtazamo na fikra za
Watanzania walio wengi wanaoamini kuwa
bidhaa bora ni zile zinazotengenezwa nje ya nchi.
Mtaka amewataka
Viongozi wa Kisiasa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Watendaji wa Serikali
katika ngazi zote, ili waweze kufikia azma ya Mkoa wa Simiyu kuwa Mkoa kiongozi kwa kutekeleza kwa Vitendo
Ilani ya Chama cha Mapinduzi , ikiwa ni pamoja na kuifikia Tanzania ya Viwanda
kwa kuanzisha viwanda vidogo hususani vya kuyaongezea thamani mazao yanayozaliswa
mkoani humo.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Kikundi cha Vijana wanaozalisha Chaki cha Maswa Family, Kelvin Steven
amesema kikundi hicho kimeongeza
uzalishaji ambapo kimekuwa kikizalisha katoni 200 kwa siku, wakati mahitaji halisi ya Mkoa wa
Simiyu ni katoni 700 kwa mwezi, hivyo kutokana na uzalishaji kuongezeka wanaendelea kutafuta soko nje ya Mkoa.
Naye Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.Dkt.Fredrick Sagamiko amewataka Wakuu wa Shule
na Walimu wakuu wote wilayani humo kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa la kununua
chaki zinazotengenezwa na Kikundi cha Vijana (Maswa Family) shule zitakapofunguliwa
Januari 09,2016.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa
amewataka wazazi wote wenye watoto wanaotakiwa kwenda shule mwakani wahakikishe
wanawapeleka na watakaokaidi watakuwa vibarua wa Serikali ambao watafanya usafi
katika taasisi za umma ikiwa ni pamoja na shule,hospitali,vituo vya afya,
zahanati, vituo vya polisi, masoko na vituo vya mabasi.
Mtaka ameongeza kuwa
wazazi wawe waaangalifu na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika kipindi
hiki cha sikukuu ili waweze kuwaandalia watoto wao mahitaji yote muhimu ya
shule.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
amefanya ziara ya siku moja Wilayani Maswa ambapo ametoa jumla ya mifuko 200 ya
saruji ikiwa ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa kuunga mkono juhudi za Serikali
na wananchi wa Maswa katika ujenzi wa miundombinu ya shule hususani vyumba vya
madarasa
0 comments:
Post a Comment