Na
Stella Kalinga
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe.Anthony Mtaka ameongoza harambee ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Gambosi
iliyopo Kata ya Gambosi wilayani Bariadi Mkoani humo.
Harambee hiyo
imefanyika kufuatia azma ya Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA)
Tanzania, Ndg.Mark Malekana kutaka kuunga mkono juhudi za wananchi wa kata
aliyozaliwa ya Gambosi katika ujenzi wa shule hiyo, kwa kuwa watoto wa kata
hiyo wamekuwa wakisoma katika shule ya sekondari Miswaki kata ya jirani ya
Mwasubuya.
Akitoa taarifa ya
ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Gambosi,
Longino Nasari amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kwa kushirikiana na
wananchi wameanza kwa kujenga vyumba vitatu vya maabara, jengo la utawala na
matundu 08 ya vyoo.
Askofu Malekana
amewataka wananchi wa Gambosi kushirikiana na Serikali kujenga shule na
miundombinu mingine ya Huduma za Jamii bila kujali tofauti zao za kiitikadi na
dini ili kuitengeneza Gambosi mpya ya tofauti na jinsi inavyodhaniwa na watu
kuwa ni mahali penye mambo ya kishirikina.
Aidha, Askofu Malekana
ametoa wito kwa wananchi wa Gambosi hususani vijana kufanya kazi kwa bidii ili
kuleta maendeleo katika eneo hilo na kubadili fikra na mtazamo wa watu wengi
juu ya eneo hilo.
“Maendeleo hayaji kwa
muujiza wala hayaji kwa bahati mbaya, acheni hadithi za kusema kama Mungu
kakupangia kufa maskini utakufa maskini, au kama ulipangiwa kuwa na tajiri
utakuwa hivyo, hapana Mungu hakupanga hivyo. Muachane kabisa na fikra hizo potofu
fanyeni kazi kwa bidii, mjenge Gambosi Mpya”
Pamoja na kuhimiza
maendeleo Askofu Malekana amewataka wananchi wa Gambosi kudumisha amani na
kuwatengenezea mazingira rafiki watumishi wanaopangwa kufanya kazi katika
eneo hilo ikiwa ni pamoja na kujenga
nyumba za kupangisha ili waone fahari kufanya kazi Gambosi.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka wananchi kuona umuhimu wa elimu na
kuwapeleka shule watoto wote wanaopaswa kwenda shule mapema mwezi Januari, 2017
shule zitakapofunguliwa.
Wakati huo huo Mtaka
amewataka wananchi kuvitumia vituo vya kutolea huduma za Afya pale wanapougua
badala ya kwenda kwa waganga wa jadi ili kupunguza vifo visivyo vya lazima
vinaivyoibua chuki na visasi vitokanavyo
na ramli chonganishi, ikiwa ni pamoja na ukataji wa mapanga kwa vikongwe kwa
imani za kishirikina.
“Tumieni
vituo vyetu vya huduma za Afya vilivyopo
ili mfanyiwe uchunguzi na kupewa tiba kwa gharama nafuu; wazee na watoto
chini ya miaka mitano wanatibiwa bure. Pamoja na unafuu huo unasikia mtu anampeleka
mtoto kwa mganga anachanjwa chale akifikishwa hospitali hana damu hana maji
anakufa, akifa mnaanza kutafuta mchawi, hiyo tabia iachwe kabisa” amesema Mtaka
Katika Harambee hiyo ya
ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi mifuko 604 ya saruji, nondo 100, bati 20,
misumari kilogramu 7, Madawati 80, Unga wa Ngano mfuko mmoja na mafuta ya kula
katoni 1 kwa ajili ya chakula cha mafundi, vitabu 18 na fedha taslimu vilipatikana,
vyote vikiwa na thamani ya shilingi 21,761,050, ikiwa ni michango ya Askofu wa
Kanisa la SDA Tanzania na wadau wake, Viongozi wa Serikali ya Mkoa na Wilaya,
Wafanyabiashara wa Bariadi na wananchi wa Gambosi.
Mkuu wa Mkoa amehimiza
fedha hizo zitumike kwa makusudi yaliyokusudiwa na ujenzi uendelee ili kufikia
mwaka 2018 shule hiyo ifunguliwe.
Paroko wa Parokia ya
Ngulyati wilayani Bariadi akizungumza na wananchi wa Gambosi (hawapo pichani)
wakati wa Harambee ya Ujenzi wa Shule ya
Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani Bariadi.
Mbunge wa Jimbo la
Itilima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Gambosi (hawapo pichani) kabla ya
kuchangia katika Harambee ya Ujenzi wa
Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi wilayani
Bariadi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Wilaya ya Bariadi, Mhe.Duka Mashaurimapya akipeana mkono na Askofu wa Kanisa
la Waadventista Wasabato (SDA), Ndg.Mark Malekana baada ya kuwasilisha mchango
wa Halmashauri hiyo wakati wa Harambee
ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha
Gambosi.
):- Mwenyekiti wa
Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu na Mbunge wa Itilima ,akipeana mkono na Diwani wa
Kata ya Gambosi Mhe. Bahame Kaliwa, baada ya kuwasilisha mchango wake wakati
wa Harambee ya Ujenzi wa Shule ya
Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijiji cha Gambosi.
Askofu wa Kanisa la
Waadventista Wasabato (SDA), Ndg.Mark Malekana akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka risiti
aliyopewa baada ya kununua mifuko 100 ya saruji
kwa ajili ya kuchangia Ujenzi wa
Shule ya Sekondari Gambosi.
Baadhi
ya wananchi wa Kijiji cha Gambosi wakienda kuchangia wakati wa Harambee ya Ujenzi
wa Shule ya Sekondari Gambosi iliyofanyika jana katika kijijini hapo
0 comments:
Post a Comment