Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC)
imeanza kutoa mafunzo ya siku tano ya Utawala na Uongozi wa Michezo Mkoani
Simiyu, ambayo yamelenga kuleta tija katika kusimamia na kuendeleza Michezo.
Mafunzo hayo
yanawahusisha Maafisa Michezo Mkoa na Wilaya, Viongozi wa Vyama mbalimbali vya
Michezo na walimu wa michezo kutoka
katika baadhi ya shule za msingi na sekondari mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa
Mafunzo hayo Ndg.Suleiman Jabir amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwasaidia
Maafisa Michezo, viongozi wa vyama vya michezo ngazi ya mkoa na wilaya sambamba
na walimu wa michezo kupata mafunzo ya kiufundi katika kusimamia na kuendeleza
michezo, ambayo hutolewa katika mikoa yote hapa nchini, chini ya usimamizi wa
Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC).
Akizungumzia ushiriki
wa wanawake Ndg. Jabir amesema Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imehakikisha
kuwa wanawake wanashiriki kwa asilimia 40 katika mafunzo hayo ikiwa ni utekelezaji
wa agizo la Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa la mwaka 2016 la kuwashirikisha
wanawake katika masuala muhimu ya kimichezo ikiwemo suala la uongozi.
Akifungua mafunzo hayo
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya
Itilima, Mhe.Benson Kilangi amesema, Utawala na uongozi wa michezo ulio bora ni
msingi wa kuongoza na kuendeleza michezo
kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu.
“Kamati ya Olimpiki imeandaa
mafunzo haya kwa wakati muafaka kwa sababu wanahitajika viongozi wenye taaluma
ya kisasa ya namna ya kuongoza michezo na wanamichezo,ambao watakwenda na wakati
kutenda kazi zao bila mgongano au vurugu “ amesema Kilangi.
Kilangi amewataka
washiriki kuhakikisha kuwa wanazingatia mafunzo watakayopata na kuwa mabalozi
wazuri katika maeneo yao, ili mafunzo hayo yasiishie tu katika Taasisi walizopo
bali elimu hiyo ifike hadi ngazi ya vijiji ambako ndiko kwenye wachezaji wengi.
Aidha, Mkuu huyo wa
Wilaya ametoa wito kwa washiriki kutumia mafunzo hayo kama chachu katika kufuata
taratibu zote za uendeshaji wa vilabu na vyama vya michezo katika mkoa wa
Simiyu ikiwa ni pamoja na kufuata katiba.
Ameongeza kuwa pamoja
na kuchukulia michezo kama burudani na sehemu ya kuimarisha afya, washiriki hao
wanapaswa kuwasaidia wachezaji kutumia michezo kama ajira inayoweza kuwaingizia
kipato.
Kwa upande wake Afisa
Michezo wa Mkoa, Ndg.Anthony Komba amesema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki
kusimamia michezo kwa weledi mkubwa, kuibua vipaji na pia yatasaidia vyama vya
michezo kusimamia vema vyama vyao, ikiwa ni pamoja na kufuata katiba hali
itakayowasaidia kuepuka migogoro katika vyama.
Mafunzo kwa Maafisa
Michezo, viongozi wa vyama vya michezo Mkoa na Wilaya pamoja na walimu wa
michezo kutoka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari Mkoani Simiyu, ambayo
yamefunguliwa rasmi leo, yanafanyika katika ukumbi wa BARIDECO mjini Bariadi na
yatahitimishwa siku ya Ijumaa tarehe 18/08/2017.
Mkuu wa Wilaya ya
Itilima, Mhe.Benson Kilangi(katikati) akizungumza na washiriki wa Mafunzo ya
Utawala na Uongozi wa Michezo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC)
wakati alipofungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony
Mtaka Mjini Bariadi.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo kutoka Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC)
Ndg.Suleiman Jabir akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo kutoka mkoani
Simiyu (hawapo pichani) ambayo yanafanyikwa kwa muda wa siku tano Mjini
Bariadi.
Afisa Michezo wa Mkoa
wa Simiyu,Ndg.Addo Komba (kushoto) akizungumza katika mafunzo ya Utawala na Uongozi
wa Michezo kwa maafisa michezo, viongozi wa vyama vya michezo na walimu wa
michezo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC)
Mkuu wa Wilaya ya
Itilima, Mhe.Benson Kilangi(wa tatu kulia walioketi) katika picha ya pamoja na maafisa
michezo, viongozi wa vyama vya michezo na walimu wa michezo wa Mkoa wa Simiyu, wanaoshiriki
wa Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo mjini Bariadi ambayo yameandaliwa
na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC); (wa pili kulia) Mkurugenzi Mkuu wa Mafunzo
Ndg.Suleiman Jabir
Baadhi ya washiriki wa
Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC)
wakifuatilia Hotuba ya Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson
Kilangi(hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo hayo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka mjini Bariadi.
Baadhi ya washiriki wa
Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC)
wakifuatilia Hotuba ya Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson
Kilangi(hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo hayo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka mjini Bariadi.
Mkurugenzi Mkuu wa
Mafunzo ya Ndg.Suleiman Jabir Utawala na Uongozi wa Michezo kutoka Kamati ya Olimpiki
Tanzania(TOC)(kulia) akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Itilima, mhe.Benson
Kilangi ambaye amefungua mafunzo hayo mjini Bariadi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, MheAnthony Mtaka.
0 comments:
Post a Comment