Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amefungua
Mashindano ya Mbio za Baiskeli na Ngoma za Asili Mjini Bariadi(Simiyu Jambo
Festival) ambayo yamehudhuriwa na Maelfu ya Wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mashindano
hayo ya mbio za baiskeli yamehusisha kilometa 200 wanaume, kilomita 80 wanawake
ambapo pia walemavu waliweza kushindania
katika umbali wa kilomita tano.
Akizungumza
baada ya kufungua mashindano hayo Dkt.Tulia pamoja na kuupongeza Mkoa wa Simiyu
kuandaa mashindano hayo amesema, ipo michezo nchini haijapewa kipaumbele lakini
ikitumiwa vizuri inaweza kutoa ajira ukiwemo mchezo wa mbio za baiskeli; ambapo
ametoa wito kwa viongozi wa mikoa mingine pia kuwekeza katika michezo
mbalimbali ili kuwasaidia wananchi kupata kipato.
“Lililofanyika
Simiyu ni jambo jema sasa hivi watu watakuwa wanajua kuwa wakijifua vizuri
kwenye baiskeli na ngoma za jadi wanakuja kushiriki mashindano ya Baiskeli na ngoma Simiyu, nitoe wito kwa viongozi wengine
kufikiria mambo mengine yanayoweza kuwasaidia wananchi katika maeneo yao kupata
ajira na kujipatia kipato” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka amesema mkakati wa mkoa huo ni kurasimisha tamaduni zote na kuhusianisha
na shughuli za Utalii ndani ya mkoa huo.
“Position(Nafasi) ya
Mkoa wa Simiyu kwenye nchi ni kukuza tamaduni na sanaa zetu kama moja ya eneo
litakalotuunganisha na sekta ya Utalii, tumezungukwa na mapori ya akiba na mbuga
za wanyama, tungehitaji watalii wanapokuja kwenye maeneo hayo wapate ladha ya
tofauti kiwemo utamaduni wa Mtanzania”
Mtaka ameongeza kuwa
wasanii wote watatambuliwa na baadae kujengewa uwezo kupitia watalaam wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam(Kitivo cha sanaa),Chuo cha Sanaa Bagamoyo na vyuo vya michezo ili waweze
kufanya kazi zao kibiashara na kuimarisha uchumi wao.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo Food Products,Mhe.Salum Khamis ambaye
ndio Mdhamini wa mashindano ya Baiskeli na ngoma za Asili (Simiyu Jambo
Festival) amesema ataendelea kudhamini mashindano kama hayo Mkoani Simiyu ili
kuwawezesha wananchi kuinua kipato kupitia vipaji vyao.
Naye mshindi wa kwanza mbio za kilometa 80
(wanawake) Raulensia Luzuba kutoka Mwanza ameomba mashirika na makampuni mbalimbali
kuwadhamini ili waweze kujengewa uwezo
na kuandaliwa kushiriki katika mashindano ya Kimataifa.
Masunga Duba mshindi wa
mbio za kilometa 200(wanaume)kutoka Simiyu amesema pamoja na wafadhili kudhamini
mashindano wawasaidie pia wachezaji
kupata baiskeli za kisasa zitakazowasaidia kwenda kwa kasi inayotakiwa.
Mashindano ya baiskeli
Mkoani Simiyu yameshirikisha wachezaji kutoka mikoa ya Simiyu, Mwanza,
Shinyanga,Arusha na Mbeya, ambapo ushindi kwa upande wa wanaume umechukuliwa na
Hamisi Hussein(Arusha) ambaye amejishindia pikipiki, wa pili ni Masunga
Duba(Simiyu) kitita cha shilingi 1,000,000/= wa tatu Richard Laizer(Arusha) .shilingi
500,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne mpaka wa 15.
Kwa upande wa wanawake
mshindi wa kwanza Raulensia Luzuba
kutoka Mwanza amejipatia shilingi 500,000/=, mshindi wa pili Tatu
Malulu(Mwanza) shilingi 400,000/= na wa tatu ni Vumilia Mwinamila(Simiyu)
shilingi 300,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne mpaka wa
10.
Walemavu mshindi wa
kwanza Emmanuel Mtemi amejipatia shilingi 200,000/= wa pili Masunga Sendama
shilingi 150,000/= na wa tatu Saguda Sospeter shilingi 100,000/=wote kutoka
mkoa wa Simiyu na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne na wa tano.
0 comments:
Post a Comment