Wananchi
wa Kata ya Nkololo katika Halmashauri ya
Wilaya ya Bariadi wametakiwa kutambua wajibu wao katika kuchangia ujenzi wa Vyumba
vya madarasa ili kupunguza tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa katika
shule za msingi na sekondari.
Wito
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati alipokuwa
akijibu kero mbalimbali za wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika
katika Kijiji cha Nkololo Kata ya Nkololo Wilayani Bariadi.
Mtaka amesema ni vema wananchi
wakahamasika kuchangia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa kama wanavyochangia
katika masuala mengine ili watoto wao wawe na mazingira mazuri ya kusomea.
“Kujenga vyumba vya
madarasa siyo wajibu wa walimu wetu ni wajibu wenu wenu wazazi, ni lazima
wananchi wa Nkololo mjenge vyumba vya madarasa kama mnavyojitoa katika mambo
mengine, najua hamuwezi kushindwa kutoa angalau mfuko mmoja wa saruji kila
kaya; Nkololo itajengwa na wana Nkololo wenyewe” amesema Mtaka.
Aidha, Mtaka ametoa
wito kwa wananchi hao kuzingatia suala la uzazi wa mpango kwa kuwa ongezeko
kubwa la watoto ndio linalopelekea idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganishwa na
vyumba vya madarasa.
“Mhe.Diwani nikuombe tengeneza
utaratibu hapa na watu wako, Nkololo ni moja ya centre(kituo) kubwa wachangie, wala
wasiseme tumechangia sana ni lazima wachangie; na kama hatutajirekebisha kwenye
kuzaana, tutachanga, tutachanga, tutachanga” amesema Mtaka.
Naye Afisa Elimu wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Doreen Rutahanamilwa amesema, Serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya elimu
vikiwemo vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo, hivyo wananchi wanao wajibu
kuunga mkono jitihada hizo ili kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.
Kuhusu kero ya uharibifu
wa mazao unaofanywa na wanyamapori hususani Tembo, ambayo ilitolewa na Luja
Masala Mkazi wa Kijiji cha Bubale, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, Serikali kupitia
watalaam wake wa Wanyamapori watakabiliana na tatizo hilo, hivyo akawataka
wananchi wasiache kulima na wazingatie ushauri wanaopewa na watalaam hao.
Akitoa ufafanuzi wa
kitaalam juu ya kero hiyo, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili, Ndg.Mazengo Sabaya
amesema, Halmashauri imekuwa ikipeleka askari wa Wanyamapori katika maeneo yanayovamiwa
na tembo na akawataka wananchi kuendelea kufuata ushauri wa kutumia uzio wa
pilipili katika mashamba yao ili kuwazuia tembo hao.
Katika suala la upatikanaji
wa mbegu bora, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka Serikali kupitia kwa
wakala wa mbegu ina mpango wa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora katika
bei wanayoweza kuimudu.
Katika hatua nyingine
Mtaka ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kuhakikisha inaweka
mipango ya ujenzi wa stendi, soko na barabara katika kituo cha Nkololo ambacho
ni moja vituo vikubwa vya kibiashara wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa ameanza
ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi katika Kata ya Nkololo na baadaye
atafanya ziara katika kata za Dutwa na Ngulyati ambapo atafanya mikutano ya
hadhara na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
0 comments:
Post a Comment