Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka Wakuu wa Shule mkoani humo
kuongeza ubunifu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika shule zao.
Mtaka
ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wakuu wa
shule zote za Sekondari yaliyofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa Shule ya
Sekondari Bariadi
Amesema wakuu wa shule wanatakiwa kuwa wabunifu
hususani katika mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuwaandaa vizuri kitaaluma wanafunzi
ikiwa ni pamoja na mazoezi na mitihani ya kujipima ya mara kwa mara, zitasaidia
wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya ndani na kitaifa.
“Kiongozi lazima uwe mbunifu,
Mkiwa wabunifu kwenye shule watoto watafanya vizuri,mnapaswa kubuni mbinu na
mikakati mbalimbali kwenye majaribio ya darasani, mitihani ya kujipima na kubuni namna ya kuwapa motisha walimu wenu
wapende kazi na kujiona ni wanafamilia katika shule mlizopo” amesema Mtaka.
Aidha, amewataka wakuu
hao wa shule kujiwekea utaratibu wa kupita mara kwa mara madarasani kukagua kwa
lengo la kujiridhisha, ikiwa walimu wanatimiza wajibu wao wa kuwafundisha
wanafunzi kama inavyotakiwa badala ya kusubiri kuletewa taarifa.
Mkuu huyo wa Mkoa pia
amewaasa wakuu hao wa shule kuwa na uongozi shirikishi ambao unajali pande zote
kwa maana ya walimu, wanafunzi na wazazi ili waweze kujua kero na masuala
mbalimbali yasiyowaridhisha na waweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa
taratibu kuyapatia suluhu.
Vile vile Mtaka amesisitiza
wakuu wa shule kufanya vikao na wazazi kwa kuwa wazazi wanayo nafasi kubwa ya
kuchangia wanafunzi kufanya vizuri, hivyo akawataka wavitumie vikao kupata
maoni ya wazazi katika masuala mbalimbali ya kuboresha maendeleo ya wanafunzi kitaaluma.
Sanjali na hilo
amewataka Wakuu hao wa Shule kuzingatia sheria, kanuni , taratibu na kuchukua
hatua stahiki pale inapobidi ikiwa ni pamoja na kutowaruhusu wanafunzi
wajawazito au waliojifungua kuendelea na masomo.
Kwa upande wake Afisa
Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory amesema katika mafunzo hayo ya siku
mbili wakuu wa shule wameelimishwa juu ya sheria zote nne za Elimu, falsafa,nyaraka,kanuni
mbalimbali za Elimu na sera mpya ya Elimu.
Nestory amebainisha pia
kuwa wakuu wa shule hao wamepewa mafunzo
ya utunzaji wa nyaraka za Serikali, udhibiti wa vitendo vya rushwa, kusimamia
shule na taaluma pamoja na utunzaji wa takwimu sahihi ambapo amewataka wakuu wa
shule hao kutumia sheria zilizopo katika kusimamia shule kupitia mipango
thabiti itakayotoa matokeo chanya.
Naye Magebu Bugacha
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwantimba ameshukuru uongozi wa Mkoa kuona umuhimu
wa kuwaandalia wakuu wa shule mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo ambayo yatawasaidia
na kuwapa uzoefu katika kuendesha na kusimamia shule zao.
Akitoa shukrani kwa
niaba ya Maafisa Elimu wa Wilaya za Mkoa huo, Afisa Elimu wa Wilaya ya Meatu,
Mwl.Estomia Makyara amesema maelekezo yote ya Mkuu wa Mkoa aliyoyatoa wakati
akifunga mafunzo hayo kwa Wakuu wa shule yatatekelezwa kwa uadilifu, ili mkoa wa
Simiyu uwe ni miongoni mwa mikoa mitatu bora kwa ufaulu katika mitihani ya Kitaifa.
Jumla ya Wakuu wa shule
152 kutoka katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu wamepata mafunzo hayo ambayo yalilenga kuwajengea uwezo
katika usimamizi na uendeshaji wa shule za Sekondari.
0 comments:
Post a Comment