Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani
Simiyu kuwasimamia watumishi wa Idara ya
Ardhi na kuhakikisha wanapima maeneo na
kutoa hati miliki kwa wananchi.
Mhe.Mabula
ameyasema hayo wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu ambayo imelenga kufuatilia utekelezaji
wa maelekezo mbalimbali aliyoyatoa wakati wa ziara yake Novemba 2017, mwenendo
wa ukusanyaji wa kodi za ardhi na kukagua
Jengo la Kanda ya Ardhi Simiyu itakayohudumia Mikoa ya Simiyu,Shinyanga na
Mara,
“Mtumishi
aliyeajiriwa kama surveyor (mpima ardhi) hana sababu za kukaa ofisini kuanzia
saa 1:30 asubuhi mpaka saa 9:30 alasiri wakati kazi zake nyingi ziko uwandani;
Mwisho atajikuta amepima viwanja 58 mwaka mzima, maana yake ni kwamba atakuwa hajajua
wajibu wake, wakurugenzi badilikeni katika kuwasimamia watumishi wa sekta ya
ardhi” amesema Mabula
Amesema ikiwa
Watumishi wa Idara ya Ardhi wakitimiza wajibu wao Ardhi ikapimwa, wananchi wakapewa
hati miliki ya maeneo yao ya viwanja na mashamba; migogoro itapungua, Serikali itakusanya
maduhuli kupitia kodi ya Ardhi na uendelezaji wa miji utafanyika katika mpango
mzuri
Pamoja na kupima
maeneo na kutoa hati miliki, Mhe.Naibu Waziri amesema Idara ya Ardhi inapaswa
kuhakikisha wananchi waliomilikishwa maeneo wanajenga kwa kuzingatia sheria
Namba 8 ya mwaka 2007 ya Mipango Miji, ili kuepukana na ujenzi holela
unaopelekea kuwa na miji isiyopangwa.
Aidha, Mhe.Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amesisitiza maeneo yote ya
Taasisi za Serikali yapimwe na kutolewa hati miliki ili kuyalinda na uvamizi.
Sanjali na hilo,
Mhe.Naibu Waziri amewataka wataalam wa Ardhi kukusanya maduhuli ya Serikali yatokanayo
na kodi za ardhi kwa kutumia mifumo ya Kielektroniki iliyowekwa katika
kufuatilia na kuhakikisha wananchi wote wanaostahli kulipa kodi ya ardhi
wanalipa kwa wakati.
Naibu Waziri
ameelekeza Kamati za Halmashauri zinazosimamia Ardhi zihakikishe zinaifanya
agenda ya Makusanyo ya maduhuli kuwa ya kudumu katika vikao vyao vya kila robo,
ili kila wanapokutana itolewe taarifa ya hali ya makusanyo, wananchi waliopewa
notisi na wale wanaotakiwa kupelekwa katika mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kwa
kushindwa kulipa kodi ya ardhi kwa wakati.
Akiwasilisha
taarifa ya Wilaya ya Bariadi Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe.Festo Kiswaga amesema Halmashauri
zote mbili zinazounda Wilaya ya Bariadi zinaendelea na kuhamasisha wananchi
kupima maeneo yao na kupata hati miliki ili kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya
Serikali kupitia kodi ya Ardhi, ambapo Halmashauri ya Wilaya Bariadi pekee kwa
mwaka 2017/2018 inatarajia kupima viwanja 2400 katika Vituo vya Kibiashara vya
Nkololo,Dutwa na Ngulyati.
Naye Kaimu
Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Kanda, Makwasa Biswalo amesema Mtalaam kutoka
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amefika Mkoani Simiyu kwa ajili
ya kutoa mafunzo ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi za Ardhi, kwa watumishi wa Halmashauri zote ambao
utawawezesha kutengeneza ankara (bill) ya makusanyo ya kodi na tozo zote.
Kwa upande wake
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameshukuru Wizara ya Ardhi kwa kuona
Umuhimu wa kuanzisha Kanda ya Ardhi ya Simiyu na akaomba Wizara ifanye
utaratibu wa kumleta Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Maswa kutokana na
aliyekuwepo kasimamishwa kazi, hali iliyopelekea mashauri mengi kutofanyiwa
kazi.
Msajili Msaidizi
wa Baraza la Ardhi Kanda ya Ziwa, Dorothy Moses amesema kuanzia mwezi Septemba
2017 atakuwepo Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Maswa ambaye atasikiliza kesi, ambapo pia ameleeza
kuwa Wizara ina mpango wa kuanzisha mabaraza mawili ya Ardhi na Nyumba katika
Wilaya ya Bariadi na Busega ambayo yataanzishwa muda wowote baada ya kupatikana
majengo kwa ajili ya Ofisi.
Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Angelina Mabula(Mb) yuko
katika ziara ya siku mbili Mkoani Simiyu ambapo akiwa Mjini Bariadi amefanya
kikao na Viongozi, wataalam wa Ardhi na
Watendaji wa Kata,Mitaa na Vijiji wa Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri
ya Wilaya Bariadi kilichofanyika Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment