Wananchi
Mkoani Simiyu wamehimizwa kwenda kushuhudia mashindano ya Baiskeli na Ngoma za
Asili yatakayofanyika kesho Jumapili katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari Mratibu wa Mashindano hayo yanayotambulika kama Simiyu
Jambo Festival ambayo yanadhaminiwa na Kampuni ya Jambo Food Products,
Ndg.Kulwa Mtebe amesema washiriki wa mbio za baiskeli kutoka mikoa mbalimbali
wameshawasili Mjini Bariadi na wamejiandaa vizuri kwa ajili mashindano.
Aidha, amesema Mgeni
Rasmi katika tukio hilo(Simiyu Jambo Festival) la Kihistoria Mkoani Simiyu
ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Tulia
Ackson ameshawasili Mkoani kwa ajili ya mashindano hayo.
Mkuu wa Usalama
Barabarani Mkoa wa Simiyu, Edson Mwakihaba amesema Jeshi la Polisi Kikosi cha
Usalama Barabarani limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba watumiaji wa
barabara wanazingatia sheria za usalama barabarani na askari watakuwepo katika
vituo vyote ambavyo washiriki wa mbio za baiskeli watapita.
Rais wa Chama cha
Baiskeli Taifa Godfrey Mhagama amesema Chama hicho kupitia kamati yake ya
Ufundi kitakahikisha kanuni na taratibu za mchezo wa mbio za baiskeli
zinasimamiwa na kufuatwa katika mashindano hayo.
Mhagama ameongeza kuwa Wachezaji
wahakikishe wanacheza katika viwango vinavyotakiwa kwa kuwa vigezo vyote vitavyozingatiwa
ikiwa ni pamoja na kasi ya mchezaji na muda anaoutumia katika kukamilisha mbio kwa
umbali uliopangwa, ambayo pia itakuwa ni njia ya kupata wachezaji wanaoweza
kuwakilisha Taifa katika Mashindano ya Olimpiki.
Kwa upande wake Meneja
Masoko wa Kampuni ya Jambo Food Products Anthony Paul amewahakikishia washiriki
kuwa zawadi zote zilizopangwa kwa washindi katika makundi yote matatu (wanaume,
wanawake, walemavu) ziko tayari ambayo ni pikipiki itakayotolewa kwa mshindi wa
kwanza(wanaume) na fedha taslimu zaidi ya shilingi Milioni nane zitakazotolewa
kwa washindi wengine.
Naye Emmanuel Mollel
mshiriki wa mashindano ya mbio za Baiskeli kutoka mkoa wa Arusha amesema
washiri kutoka katika mkoa huo wamejipanga kikamilifu na kiushindani
kuhakikisha wanapata ushindi.
Tatu Malulu mshiriki wa
mbio za Kilometa 80 kutoka katika Mkoa wa Mwanza amesema amekuwa akifanya
mazoezi siku zote ambayo yamemuimarisha hivyo akathibitisha kuwa kutokana na
maandalizi hayo anatarajia ushindi na ametoa wito kwa Wachezaji kujenga
utamaduni wa kufanya mazoezi siku zote maana ndio siri ya kufanikiwa kwao.
Zaidi ya washiriki 160 kutoka
katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita na Arusha wanatarajia
kushiriki mashindano hayo ambayo yatagawanyika katika makundi matatu; wanaume
Kilometa 200, wanawake Kilometa 80 na Watu wenye Uemavu Kilometa 05.
0 comments:
Post a Comment