Halmashauri ya Wilaya
ya Maswa Mkoani Simiyu imetekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli la kutengeneza
madawati kwa asilimia 75, ambapo hadi kufikia Mei 31mwaka huu, imetengeneza madawati
19,655 kati ya 26,261 yanayohitajika kwa
shule za msingi na meza 10,943 kati ya 9,359 zinazohitajika na viti 10,810 kati
ya 9,359 vinavyohitajika na kufanya kuwa na ziada ya meza 1,432 na viti 1,277
kwa shule za sekondari.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe.
Rosemary Kirigini wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya utekelezaji wa agizo
hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka alipofanya ziara
kuona namna agizo hilo linavyotekelezwa wilayani humo.
Mhe. Kirigini alisema
wamefikia hatua hiyo kutokana na kuwashirikisha wadau mbalimbali, kunua mbao na
kutumia mafundi ambao ni wanafunzi wa Chuo cha Ufundi
cha Binza, ambao wamekuwa wakitengeneza madawati 500 hadi 1000 kwa siku, kwa
gharama ya shilingi 21,625/= kwa dawati moja.
Akipokea taarifa ya
wilaya ya Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu mhe. Anthony J. Mtaka ameupongeza
uongozi wa wilaya ya Maswa kwa hatua waliyofikia na ubunifu walioutumia katika
kutafuta mbao na kuwatumia mafundi kutoka Chuo cha Ufundi cha Binza, hali
iliyosaidia kupunguza gharama na akazitaka wilaya nyingine kutumia uzoefu wa
Maswa ili zikamilishe agizo la Mhe. Rais kwa wakati uliopangwa.
“Hiki chuo ni cha
Serikali, wakipewa mbao wanatengeneza dawati moja kwa shilingi 21,625 kama
alivyotuambia DC,kwa nini wilaya zote za mkoa huu wasione umuhimu wa kuwatumia
hawa vijana wa chuo hiki kuwafanyia kazi yao. Watu wanatengeneza dawati moja
kwa shilingi 70,000/= sasa si bora tukatumia chuo chetu hiki ili tupunguze
gharama na kumuwezesha Mkuu wa chuo akapata fedha zitakazomsaidia kuendesha
chuo badala ya kutegemea ruzuku ya serikali?” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amepiga
marufuku tabia ya kutumia viti,meza na madawati ya wanafunzi katika shughuli
nyingine kama mikutano ya hadhara kwa kuwa kuhamisha madawati au viti kutoka
sehemu moja kwenda nyingine kunachangia uharibifu.
Wakati huo huo Mtaka
amewataka Maafisa Elimu kuweka mikakati ya kitaaluma ili kuwafanya kuongeza
ufaulu kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kufanya mitihani ya
majaribio ya mara kwa mara kwa madarasa ya mitihani na kuanzisha na kuzisimamia
klabu za masomo mbalimbali mashuleni
Kwa upande wake Katibu
Tawala Mkoa, Jumanne A. Sagini amesema Halmashauri ione umuhimu wa kupima
maeneo yote ya shule ili yatambuliwe yasivamiwe na wananchi kwa kufanya
shughuli nyingine kinyume na utaratibu.
Halmashauri ya Wilaya
ya Maswa ina jumla ya shule za Msingi 121 zenye wanafunzi 78,783 na shule za sekondari 40 kati ya hizo 36 ni za Serikali ambazo zina
jumla ya wanafunzi 9359.