Wanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi mkoani Simiyu wameomba viongozi wa mkoa na wadau wote wa elimu kuwa kambi za kitaaluma ziwe endelevu kwa kuwa zina matokeo chanya kwa katika ufaulu wa wanafunzi na ili mkoa uendelee kufanya vizuri katika mitihani yote ya Kitaifa.
Ombi
hilo limetolewa tarehe 14 Aprili 2021 wakati wanafunzi hao walipopokea msaada
wa chakula, shajala na taulo za kike kutoka Benki ya TPB vyote vikiwa na
thamani ya shilingi 4,550,000/= ambavyo vimetolewa kwa jili ya wanafunzi wa
kambi za kitaaluma kwa kidato cha sita mkoani hapa.
“Tunaomba
kambi hizi ziwe endelevu maana zina mchango chanya kwenye ufaulu wa masomo
yetu, miaka ya nyuma tulikuwa tukishika nafasi za mwisho kabisa lakini sasa
hivi tumekuwa wa tatu Kitaifa; pia tuwaahidi tu kwamba kidato cha sita mwaka
huu hatutawaangusa tutashika nafasi ya
kwanza,” alisema Godfrey Andrew mwanafunzi wa kidato cha sita.
“Tunashukuru
kwa msaada huu wa vitu tulivyopewa lakini pia tunashukuru kwa jitihada za mkoa
kuanzisha kambi ambazo zimetusaidia kuongeza ufaulu wetu, pamoja na ufaulu
kambi hizi zimesaidia wanafunzi wengi kumaliza masomo yao pasipo kukatishwa na
sababu za kijamii kwani muda mwingi wanakuwa shuleni,” Minza Kija mwanafunzi wa
kidato cha nne
Awali
akitoa taarifa ya elimu ya mkoa Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Ernest
Hinju amesema mkoa una mkakati wa taaluma wenye vipengele 12 na kimojawapo
kikiwa kambi za kitaaluma ambazo zimechangia kuuweka mkoa katika mikoa kumi
bora katika mitihani yote ya Kitaifa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya TPB, Bw. Henry Bwogi akikabidhi
msaada wa chakula, shajala na taulo za kike kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPB
Benki amesema benki imetoa msaada huo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za
Serikali katika elimu.
Aidha,
Bwogi ametoa rai kwa wanafunzi kujisomea kwa bidii ili waweze kufanya vizuri na
kufikia ndoto zao ikiwa ni njia moja wapo ya kuthamini juhudi za viongozi wa
Mkoa wa Simiyu na wadau mbalimbali katika elimu.
Akizungumza
kwa niaba ya uongozi wa Mkoa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Bw. Ekwabi Mujungu
ameishukuru Benki ya TPB kutoa msaada huo ambao umeonesha ni namna gani wadau
wa elimu wanatambua kazi inayofanywa na viongozi na wananchi wa mkoa wa Simiyu
katika sekta ya elimu ambapo amewahakikishia kuwa msaada huo utatumika kwa
malengo yaliyokusudiwa.
Vile vile Mujungu amewapongeza viongozi na watendaji
wa idara ya elimu mkoa wa Simiyu kwa jitihada wanazofanya katika elimu ambazo
zimechangia kuuweka mkoa wa Simiyu katika nafasi nzuri ya ufaulu kwa mitihani
yote ya Kitaifa, huku akiwataka wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze kufanya
vizuri na kufikia lengo la mkoa la kushika nafasi ya kwanza katika mitihani
yote.
MWISHO
Mkurugenzi wa Mikopo wa
Benki ya TPB , Bw. Henry Bwogi mwenye suti nyeusi) akikabidhi msaada wa taulo
za kike kwa uongozi wa Mkoa wa Simiyu, kwa ajili ya kambi za kitaaluma za
kidato cha sita na kidato cha nne, ambao ulikabidhiwa katika Shule ya Sekondari
ya Bariadi, tarehe 14 Aprili 2021.
Baadhi ya wanafunzi wa
shule ya sekondari Bariadi wakishangilia jambo wakati wa makabidhiano ya msaada
wa vyakula na mahitaji mengine muhimu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha
sita walio katika kambi za kitaaluma katika shule zao, msaada ambao umetolewa
na benki ya TPB tarehe 14 Aprili 2021.
Baadhi ya watendaji
katika idara ya elimu mkoa wa Simiyu na Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakishuhudia makabidhiano ya msaada wa
vyakula na mahitaji mengine muhimu kwa wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita
walio katika kambi za kitaaluma katika shule zao, msaada ambao umetolewa na
benki ya TPB tarehe 14 Aprili 2021.