Friday, April 29, 2022
RC Kafulila akaribisha Eid kwa mshindano ya kusoma Quran na Iftar
Mhe. Kafulila Awapongeza Walimu na Wanafunzi Waliofanya Vizuri Katika Mitihani ya Taifa 2021, Aongeza Kiasi cha Zawadi za Ufaulu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ametumia kiasi cha Tsh.59,040,000/- (Milioni hamsini na tisa na arobaini elfu tu) kama zawadi na motisha kwa walimu, wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya mwaka 2021.
Hafla ya kukabidhi zawadi hizo imefanyika hivi karibuni katika ukumbi wa shule ya Sekondari Kusekwa iliyopo mjini Bariadi.
Zawadi hizo ambazo zilikuwa katika kategoria mbili. Kategoria ya kwanza ilihusisha zawadi kwa Mtihani wa darasa saba ambapo ndani yake kulikuwa na makundi manne ambayo yalipewa zawadi.Kundi la kwanza la zawadi lilienda kwa shule iliyoingia kumi bora kitaifa- katika shule za Serikali ambapo shule ya Msingi Mwanhegele iliyopo Wilayani Maswa imepokea zawadi ya Tsh.2,000,000/- (milioni mbili).
Kundi la pili la zawadi zimetolewa kwa wanafunzi watano walioingia kumi bora kitaifa ambapo kila mmoja wao alipokea fedha taslim kiasi cha Tsh.1,000,000/-(milioni moja). Kundi la tatu la zawadi zilitolewa kwa walimu wawili waliofanya vizuri zaidi kitaifa katika masomo ya Hisabati, Stadi za Kazi na Maarifa ya Jamii ambapo kila mmoja wao alipokea zawadi ya fedha taslim kiasi cha Tsh.300,000/-.
Kundi la nne la zawadi zilizotolewa kwa Walimu 36 waliofaulisha masomo yao kwa GPA nzuri zaidi Kimkoa pamoja na Walimu Wakuu wao kwa niaba ya shule zao. Katika kundi zilitolewa zawadi zenye jumla ya Tsh. 4,500,000/= na kufanya thamani ya zawadi zote zilizotolewa kwa ufaulu wa darasa la saba kufikia kiasi cha Tsh. 12,100,000/=(Milioni kumi na mbili na laki moja tu).
Kategoria ya pili ya zawadi zilizotolewa na Mhe.Kafulila zilielekezwa kwa ufaulu wa Mtihani wa kidato cha Nne,ambapo napo kulikuwa na makundi manne yaliyopokea zawadi hizo. Kundi la kwanza la zawadi lilielekezwa kwa kwa Shule iliyoingia Kumi Bora Kitaifa katika shule za Serikali ambapo shule ya sekondari Ng'hoboko iliyopo Wilayani Meatu ilipokea kiasi cha Tsh.3,000,000/-.
Kundi la pili la zawadi zilienda kwa Wanafunzi waliofaulu Mtihani kwa kupata daraja la kwanza alama 7 (Division One - Point kwa 7 Shule za Serikali),ambapo jumla ya wanafunzi 6 walipokea zawadi ya Tsh. 1,000,000/- kila mmoja. Kundi la tatu la zawadi zilielekezwa kwa Walimu waliofaulisha masomo yao kwa GPA nzuri zaidi ambapo jumla ya walimu 34 pamoja na Wakuu wao wa Shule 34 kwa niaba ya walimu walipokea kiasi cha Tsh. 9,200,000/=.
Kundi la nne katika kategoria hii, ilikuwa zawadi zilizotolewa kwa waalimu 958 waliofaulisha masomo yao kwa Daraja "A" ambapo kila mmoja wao alipata zawadi ya Tsh. 30,000/- kwa kila A moja na kufanya jumla ya Tsh.28,740,000/-.Jumla ya fedha zilizotumika kutoa zawadi zote kwenye kategoria ya Mitihani ya kidato cha nne ni Tsh. 46,940,000/=
Pamoja na zawadi tajwa hapo juu Mhe. Kafulila ametoa zawadi nyinginezo zikiwemo Vyeti vya Pongezi na Ngao kwa Shule, Kata na Halmashauri zilizofanya vizuri Kimkoa kwa Mtihani wa Darasa la Nne, Darasa la Saba, Kidato cha Pili na Kidato cha Nne pamoja na Vyeti vya Pongezi kwa Wadau mbalimbali wa Elimu kutokana na Mchango wao wakiwemo Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Aidha ili kuongeza hamasa kwa walimu katika kuchapa kazi kwa bidii na maarifa Mhe. Kafulila amesema lengo la mwaka huu 2022 ni kupata alama ''A'' 2000 na kila Mwalimu atakayepata A atalipwa kiasi cha Tsh. 50,000/- kwa kila ''A'' badala ya Tsh.30,000/- kama ilivyo sasa.
Mhe. Kafulila amewapongeza walimu wote wa mkoa wa Simiyu kwa kuchapa kazi licha ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo zikiwemo ukosefu wa nyumba za walimu na miundombinu isiyo rafiki.Mwisho.