Saturday, April 28, 2018

TANAPA YATOA SHILINGI MILIONI 50 KUSAIDIA UJENZI WA SHULE ZA VIPAJI MAALUM SIMIYU



Shirika la Hifadhi za Taifa leo limekabidhi mchango wa Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule tatu za vipaji maalumu katika mkoa wa Simiyu za Simiyu Ufundi , Simiyu Wavulana na Simiyu Wasichana .

Mchango huo umekabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka.

Fedha hizi zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa shule maalum ya sekondari ya ufundi mkoani Simiyu ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya mkoa katika kuimarisha sekta ya elimu ambapo pia mkoa umepanga kujenga shule nyingine maalum mbili za sekondari za wasichana na wavulana.

Kwa pamoja Mhe Mtaka aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga wameihakikishia TANAPA kuwa fedha hizo zitatumika kama zilivyokusudiwa na wakaahidi kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umuhimu wa wananchi kuheshimu sekta ya uhifadhi kwa kuwa ina manufaa makubwa kwao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi aliahidi kuendelea kuwaunga mkono wana Simiyu kwa kuwa mkoa huo umekuwa mstari wa mbele katika kusimamia sheria za hifadhi hususan Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kuzuia uingizaji wa mifugo pamoja na majangili.

Shule ya Ufundi ya Simiyu inatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi Milioni 350 hadi itakapokamilika na wadau mbalimbali wameombwa kuunga mkono jitihada hizo za Simiyu.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa( TANAPA) Allan Kijazi akikabidhi Hundi ya  Sh Mil 50 kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka kwa ajili ya kusaidia Ujenzi wa Shule za Vipaji Maalum katika mkoa huo ,wengine kushoto ni Meneja Mawasiliano wa Tanapa,Pascal Shelutete na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi ,Bw Festo  Kiswaga .

Wednesday, April 25, 2018

WANANCHI MKOANI SIMIYU WAJITOKEZA KWENYE UJENZI WA SHULE YA VIPAJI MAALUM



Wananchi wa Wilaya ya  Bariadi Mkoani Simiyu  kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga  wamejitokeza kwa wingi  kuchangia nguvu kazi , kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu
.
Wananchi hao wamejitokeza leo kwa wingi katika shule ya sekondari ya Simiyu kwa lengo la kuunga jitihada za Mkuu wa Mkoa wao Anthony Mtaka za kuhakikisha wanakuza na kurudisha heshima ya elimu Mkoani humo.

Wamesema  kuwa wameguswa na uamuzi wa Serikali wa kuona  umuhimu wa kuboresha mazingira rafiki ya kujifunzia wanafunzi na kujenga shule kubwa ya vipaji maalum ambayo itakuwa ni msaada na utambulisho wa  Mkoa wao.
Yohana Musa mkazi wa mji wa Bariadi amesema kuwa wamegusa sana na uamuzi wa Serikali ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wao wa Mkoa Anthony Mtaka wa kuwekeza katika elimu ambayo itawasaidia watoto wao kufikia malengo waliyojiwekea.
“chini ya uongozi wa mkuu wa Mkoa  pamoja na Mkuu wa Wilaya,Mkoa wetu utakuwa na shule bora itakayochukua idadi kubwa ya wanafunzi walio na vipaji maalum ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu…Alisema Musa.
Mwenyekiti wa mtaa wa mnara wa voda Songera Magenda amesema kuwa wananchi wake wamekuwa na muamko wa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ili kujenga Mkoa wao.
Magenda amesema kuwa kupitia nguvu kazi za wananchi wake ,ni matumaini yake kuwa ujenzi wa shule hiyo utaenda kwa kasi na kukamilika mapema mwaka huu ambapo ukikamilika utatoa fursa kwa wanafunzi wenye vipaji maalum wa Mkoa wa Simiyu kusoma hapo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga  amesema endapo shule hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 kwani inatarajiwa kuwa na mabweni 10 pamoja na vyumba vya madarasa visivyopungua 40.
Kiswaga amesema kuwa shule hiyo imeanza kujenga kwa jitihata za uongozi wa Mkoa ambao lengo kuu ni kuona Mkoa wa Simiyu nao unakuwa na shule kubwa,nzuri ya wanafunzi wa vipaji maalum kama ilivyo mikoa mingine.
Kiswaga pia ametoa wito kwa wanasimiyu wote wenye mapenzi mema na elimu ,waone umuhimu wa kujitolea na kuchangia ujenzi wa shule hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kusaidia kundi kubwa na wanafunzi kusoma shuleni hapo.
MWISHO
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Malambo Mjini Bariadi wakichimba msingi wa wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu ambayo inatarajiwa kuwa shule ya vipaji maalum ya mkoa wa Simiyu.
 

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Festo Kiswaga (mwenye koleo) akishirikiana na wananchi kwa Kata ya Malambo mjini Bariadi kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu ambayo inatarajiwa kuwa shule ya vipaji maalum ya mkoa wa Simiyu.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Festo Kiswaga (mwenye koleo) akishirikiana na wananchi kwa Kata ya Malambo mjini Bariadi kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu ambayo inatarajiwa kuwa shule ya vipaji maalum ya mkoa wa Simiyu.

 

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!