Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu wamekubali kuunga mkono
Serikali katika Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkoa wa Simiyu inayotarajiwa
kuanza kujengwa mwezi Juni mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa na Wafanyabiashara hao katika kikao chao na
Mkuu wa Mkoa kilichofanyika jana Mjini Bariadi, ambacho kilifanyika kwa
lengo la kuzungumzia fursa za biashara na uwekezaji zilizopo mkoani humo,
changamoto zinazowakabili na utatuzi wake.
Awali akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony
Mtaka amesema Serikali mkoani humo imekusudia kuwa na shule kubwa itakayoweza
kuchukua wanafunzi 1000 ambayo itakayopatikana kwa kujenga upya shule ya
Sekondari Simiyu (Kidato cha kwanza hadi cha Nne), ambapo aliahidi kuwa ofisi
yake itatoa fedha kiasi na akawaomba wafanyabiasha wazawa kuchangia Ujenzi wa
shule hiyo kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa.
Amesema pamoja na kujenga
upya Shule ya Sekondari Simiyu, katika shule hiyo kutajengwa mabweni kwa ajili
ya wanafunzi wa kike ili wanafunzi wote wa kike wasome wakiwa wanafunzi wa bweni(boarding).
Ameongeza kuwa shule hiyo itakuwa ikichukua wanafunzi
watakaofanya vizuri kutoka katika wilaya nyingine ili waandaliwe vema na
kuimarisha shule za Kidato cha Tano na Sita na kuwa katika uwezo wa kushindana
na wenzao kutoka mikoa mingine.
Aidha, amesema mara baada ya kukamilisha kuimarisha Shule ya
Sekondari ya Simiyu Mkoa huo umedhamiria kuwa na Shule ya Sekondari ya
Wasichana Simiyu na Shule ya Sekondari ya Wavulana Simiyu, ambazo zitapatikana kwa Kujenga Upya au
kubadili zilizopo kwa kibali maalumu cha Wizara yenye dhamana na Elimu, ili
kuwa na shule mbili za mkoa moja ya wasichana na nyingine ya wavulana.
"Hatuwezi kuwa Makao Makuu ya Mkoa ambayo elimu yote
inaishia Shule za Kata, ni lazima tutengeneze shule ambayo watoto wetu
wakifanya vizuri katika wilaya zetu wanakuja kusoma hapa; hatuwaweza kushindana
na kufanya mambo yote mazuri tuliyojadili hapa ya viwanda na mengine kama
hatutaelimisha watu wetu" alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu Bw. Njalu
Silanga amesema Wafanyabiashara wako tayari kuunga mkono juhudi za Serikali
katika ujenzi wa Shule ya Mkoa jambo ambalo litakuwa mwendelezo wa kile
kilichowahi kufanyika miaka iliyopita ambapo wafanyabiashara hao walijenga
shule ya Sekondari Biashara na kuikabidhi kwa Serikali.
“Sisi wana Simiyu tunapenda maendeleo, tumewahi
kukusanywa kama hivi leo tukakubaliana tukajenga Shule ya Sekondari Biashara
tukaikabidhi Serikali, pia wapo watu hapa kwenye maeneo yao wamejenga madarasa
tena ya viwango wakaikabidhi Serikali, kujenga Shule ya Sekondari ya Mkoa
inawezekana” alisema Njalu.
Wakati
huo huo wafanyabiashara hao wameahidi kuwashirikisha Wafanyabiashara wengine
ambao ni wazaliwa wa Mkoa wa Simiyu wanaofanya biashara zao katika mikoa
mingine ili washirikiane katika kufanikisha Ujenzi wa Shule ya Sekondari Mkoa
wa Simiyu.
Baadhi ya
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao chao na Mkuu huyo wa Mkoa
kilichofanyika jana Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyabiashara Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu
Silanga akizungumza katika kikao cha Wafanyabiashara wa Mkoa huo na Mkuu wa
Mkoa huo katika Kikao kilichofanyika jana Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Wafanyabiashara wa Mkoa huo katika kikao
kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya
Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao chao na Mkuu huyo wa Mkoa
kilichofanyika jana Mjini Bariadi.
0 comments:
Post a Comment