Takribani
wanafunzi 1003 wa Kidato cha sita kutoka shule za Sekondri 11 zenye kidato cha
tano na sita Mkoani Simiyu, wamepiga kambi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana
Maswa na Shule ya Sekondari Binza, ikiwa
ni sehemu ya maandalizi ya Mtihani wa Taifa ambao unatarajia kufanyika mapema
mwezi Mei mwaka huu.
Akifungua
kambi hiyo leo katika Shule ya Sekondari
ya Wasichana Maswa wilayani Maswa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka
amesema ili mkoa huo uweze kushindana na kufanya mageuzi katika Uchumi ni
lazima kuwekeza katika elimu.
“Kama
wanafunzi wetu wanakaa makambi ya michezo ngazi ya kata, wilaya, mkoa na Taifa
kwa nini wanafunzi hao hao wasikae kambi
kwa ajili ya maendeleo ya taaluma; tukitaka kufanya mageuzi ya Mkoa huu ni
lazima tuweke nguvu kwenye elimu, maeneo yenye uchumi mzuri wamewekeza sana kwenye
elimu” alisema Mtaka.
Aidha,
Mtaka awataka wanafunzi wote wa kidato cha sita kuwasikiliza walimu watakaokuwa
wakiwafundisha na kuwaelekeza na akawataka kujiamini wakati wa mtihani wao wa
mwisho.
Afisa
Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory amesema Mkoa huo una mpango wa
kuondoa daraja la nne na sifuri katika matokeo ya Mitihani ya Taifa, hivyo wanayo matumaini makubwa kuwa, kupitia makambi
hayo ya kitaaluma Mkoa utaweza kufikia lengo hilo kwa matokeo ya kidato cha
sita mwaka 2018.
“
Tumeamua kuwaleta pamoja wanafunzi ili waweze kunyanyuka kama kundi moja la
mama mmoja (Simiyu) na kuweza kupandisha ufaulu, tumewaleta hapa ili kuweza kunyanyua
morali wa kazi kuwaleta pamoja anayeweza na asiyeweza ili tuweze kunyanyuka
pamoja kama kundi” alisema Mwl.Nestory.
Amesema katika siku 10 za kambi wanafunzi wa
kidato cha sita watapitishwa katika miiko ya watahiniwa wakati wa mitihani kwa
kuwa mkoa wa Simiyu unapinga suala la udanganyifu kwenye mitihani, watapitishwa
katika maswali na mada ambazo baada ya tathmini ilionekana hawakufanya vizuri
katika mtihani wa kanda na mtihani wa Mkoa.
Akizungumza
kwa niaba ya walimu mahiri 40 ambao watakuwa wakiwafundisha na kuwasaidia
wanafunzi hao, Mwl.Majaliwa Chibona wa
Shule ya Sekondari Mwandoya wilayani
Meatu amesema, wamejipanga kuwasaidia wanafunzi katika kuwapa mbinu na mikakati
mbalimbali itakayowasaidia kujiandaa na mitihani wao wa mwisho ili waweze
kufaulu.
Nao
baadhi ya wanafunzi wamesema kambi hiyo itawasaidia sana katika kuwajengea hali
ya kujiamini kwa kuwa watasaidiwa na walimu katika maeneo yote yanayoonekana
magumu kwao, watasaidiana wa kwa wao kupitia makundi na watapewa mbinu zitakazowasaidia
kujiandaa vema na hatimaye kufanya vizuri.
Baadhi
ya Wanafunzi wa Kidato cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza
Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kambi
ya Kitaaluma kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha
Sita kutoka shule 11 za Mkoa huo wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa
wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Baadhi ya walimu mahiri 40 waliochaguliwa kufundisha na kuwaandaa wanafunzi wa
kidato cha sita (kutoka shule 11 mkoani Simiyu) na Mtihani wa Taifa
utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony
Mtaka (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma kwa wanafunzi
hao Aprili 03 wilayani Maswa.
Mkuu
wa Wilaya ya Maswa, Mhe.Dkt.Seif Shekalaghe akizungumza na wanafunzi wa Kidato
cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa wa Simiyu wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma
kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani humo.
Afisa
Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory akizungumza na wanafunzi wa Kidato
cha Sita kutoka shule 11 za Mkoa huo wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Kitaaluma
kwa wanafunzi hao Aprili 03 wilayani Maswa.
0 comments:
Post a Comment