Shirika la Hifadhi za Taifa leo limekabidhi mchango wa Shilingi Milioni 50
kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule tatu za vipaji maalumu katika mkoa wa
Simiyu za Simiyu Ufundi , Simiyu Wavulana na Simiyu Wasichana .
Mchango huo umekabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi kwa Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka.
Fedha hizi zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa shule maalum ya sekondari ya
ufundi mkoani Simiyu ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya mkoa katika kuimarisha
sekta ya elimu ambapo pia mkoa umepanga kujenga shule nyingine maalum mbili za
sekondari za wasichana na wavulana.
Kwa pamoja Mhe Mtaka aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo
Kiswaga wameihakikishia TANAPA kuwa fedha hizo zitatumika kama zilivyokusudiwa
na wakaahidi kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umuhimu wa wananchi
kuheshimu sekta ya uhifadhi kwa kuwa ina manufaa makubwa kwao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi aliahidi kuendelea
kuwaunga mkono wana Simiyu kwa kuwa mkoa huo umekuwa mstari wa mbele katika
kusimamia sheria za hifadhi hususan Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kuzuia
uingizaji wa mifugo pamoja na majangili.
Shule ya Ufundi ya Simiyu inatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi Milioni
350 hadi itakapokamilika na wadau mbalimbali wameombwa kuunga mkono jitihada
hizo za Simiyu.
0 comments:
Post a Comment