Thursday, March 29, 2018

SIMIYU, TANTRADE KUSHIRIKIANA KUANDAA MAONESHO YA WAKULIMA NANENANE KITAIFA MWAKA 2018Mkoa wa Simiyu na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania(TanTrade) wamesema watashirikiana kwa pamoja kuandaa Maonesho ya Kilimo NaneNane mwaka 2018 ambayo Kitaifa  yatafanyika Mkoa wa Simiyu.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bw. Edwin Rutageruka katika Mkutano wao na Waandishi wa Habari uliofanyika katika makao makuu ya Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.

Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa Mkoa utatoa dira ya kuyafanya Maonesho ya Kilimo NaneNane kuwa ni Maonesho ya Kilimo Biashara ili Watanzania wapate fursa ya kuona teknolojia mbalimbali kwenye eneo la kilimo, mifugo na uvuvi.

“Sisi kama Mkoa tungehitaji tutoe dira ya kuyafanya maonesho ya Wakulima NaneNane yawe ni maonesho ya Kilimo Biashara, mahali ambapo Watanzania watapata Fursa ya kuona teknolojia mbalimbali kwenye eneo la Kilimo, eneo la mifugo, eneo la uvuvi na yote haya yabebebwe na dhana ya Kilimo Biashara” alisema Mtaka

“Matarajio yetu kama mkoa kwa kushirikiana na TanTrade ni kuona kwamba tunaingiza Maonesho ya Kilimo NaneNane kuwa tukio ambalo litawakaribisha watu wenye teknolojia mbalimbali Kitaifa na Kimataifa kwenye kuwezesha mageuzi ya kilimo,uvuvi na ufugaji wa nchi kwa kuonesha ni kwa namna gani wanaweza kumfikia mkulima, mvuvi na mfugaji kwenye teknolojia ya kisasa ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi ili Maonesho ya Kilimo NaneNane yawekwe kwenye ramani ya dunia” alisisitiza  Mtaka

Aidha, Mtaka ameziomba Balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali kuyatangaza Maonesho haya kwa kuyatumia kukaribisha makampuni yenye teknolojia kuja kuonesha mkoani Simiyu na akatumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kwa makundi yote kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika eneo litakalofanyika Maonesho ya Kilimo Biashara ili uwekezaji huo uendane na viwango vya Kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Bw. Edwin Rutageruka ameeleza kuwa Mkoa wa Simiyu na TanTrade wamekubaliana kuwa na maonesho endelevu ya Kisekta katika Mkoa wa Simiyu

Rutageruka ameongeza kuwa TanTrade ni taasisi pekee iliyopewa jukumu la kusimamia masuala ya Maonesho ndani na nje ya nchi kisheria, hivyo kutokana na uzoefu wa uandaaji wa Maonesho mbalimbali,  kwa mwaka 2018 Maonesho ya Kilimo Biashara yatakuwa ni Maonesho bora kwasababu watawaandaa washiriki wote Kisekta,  kuweka miundo mbinu ya kisasa na kuyafanya Maonesho haya kuwa ya Kimataifa.

“Mkoa wa Simiyu una kiu ya kuona Maonesho ya Kilimo Biashara  yanakuwa ya kisasa  kama ilivyo Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ambayo kwa Afrika Mashariki ndiyo Maonesho yanayoongoza kwa ubora na Maonesho haya ya Kilimo tutayafikisha huko” aliongeza Bw Rutageruka.

Hivi karibu Serikali imetangaza Kanda Mpya ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima NaneNane  inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ambayo inatambulika kama Kanda ya Ziwa Mashariki na Maonesho hayo kwa kanda hiyo  yatakuwa yanafanyika Mkoani Simiyu.
 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari katika Makao Makuu  ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) jijini Dar es Salaam juu ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima NaneNane yanayotarajiwa kufanyika Kitaifa Mkoani humo mwaka 2018, (kulia) Mkurugenzi Mkuu Mamlaka hiyo, Bw. Edwin Rutageruka.

Tuesday, March 20, 2018

WAZIRI KABUDI AWATAKA WASAJILI WA VYETI VYA KUZALIWA MIKOA YA SIMIYU, MARA KUZINGATIA UMAKINI NA UZALENDO


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Prof. Palamagamba Kabudi amewataka wasajili wa vyeti vya kuzaliwa kupitia mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano  kwenye mikoa ya Simiyu na Mara, kufanya kazi hiyo kwa umakini na uzalendo mkubwa katika kuhakikisha wanawasajili watoto wenye sifa.

Waziri Kabudi ametoa rai hiyo Machi 20 wakati wa Uzinduzi wa  Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa, katika mikoa ya Simiyu na Mara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

 “Mikoa ya Mara na Simiyu ina muingiliano mkubwa sana na wananchi wa nchi jirani hivyo wasajili wawe makini na watangulize uzalendo wakati wa kutekeleza  mpango huu, tusisajili mtoto ambaye hahusiki na pale ambapo tuna mashaka kuwa mtoto huyo anaweza kuwa wa nchi za jirani, tutoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika ili hatua za kiusalama zichukuliwe” alisema Profesa Kabudi.

Amesema kuwa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano unafanyika bila malipo hivyo wasajili wasitumie kwa namna yoyote mpango huo kama fursa ya kujipatia fedha kwa udanganyifu.

Aidha, Waziri Kabudi ameahidi kutoa tuzo maalum kwa mkoa (kati ya Simiyu na Mara) utakaofikia asilimia 80 ya lengo  la usajili kwa kipindi cha miezi miwili tangu usajili ulipoanza  na wakati huo huo akawataka Viongozi wa Taasisi zote Umma kuvitambua vyeti vitakavyotolewa chini ya mpango huo kwa kuwa ni vyeti halali.

Mwenyekiti wa Bodi ya  Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA) Profe. Hamis Dihenga amesema kupitia mpango wa usajili na kutoa vyeti kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano,  RITA inakusudia kusajili jumla ya watoto 735, 545 katika mikoa ya Simiyu na Mara kwenye vituo 463 (Mara) na Vituo 324 (Simiyu).

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe.Annarose Nyamubi akiwasilisha taarifa ya Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe.Adam Malima amesema hadi sasa Mkoa huo umesajili jumla ya watoto 78, 625 na watahakikisha watoto wote wanaopaswa kusajiliwa wanasajiliwa ndani ya miezi miwili na baadaye kuendelea na usajili kwa watoto watakaozaliwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga, akitoa salamu za Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka amesisitiza wananchi kutambua umuhimu wa kuwasajili watoto wao ili waweze kutambulika, kupewa vyeti vya kuzaliwa na Serikali iweze kupata takwimu sahihi.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto (UNICEF) hapa nchini ambao ni miongoni mwa wafadhili wa mpango huu,  Bi. Maud Droogleever , amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wote wenye umri wa chini ya miaka  mitano wanasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Baadhi ya wananchi wa Mikoa ya Simiyu na Mara walioshirikia katika Uzinduzi wa Mpango huo wameishukuru Serikali kwa kuleta mpango huo kwa kuwa umewarahisishia huduma ya kupata vyeti vya kuzaliwa kwa kuwasogezea huduma hiyo katika Ofisi za kata tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(wa tatu kushoto) akizindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa,  kwa mikoa ya Simiyu na Mara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati) akionesha nakala ya cheti cha kuzaliwa kinachotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili na kutoa vyeti kuzaliwa  kwa  watoto wenye umri huo kwa mikoa ya Simiyu na Mara uliofanyika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akipewa maelezo juu ya mfumo unaotumika kukusanyia taarifa za usajili kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano chini ya mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto hao, katika mikoa ya Simiyu na Mara ambao aliouzindua Machi 20, katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akioneshwa cheti cha kuzaliwa kilichotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA), mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akimkabidhi mkazi wa Manispaa ya Musoma cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake mwenye umri wa chini ya miaka mitano,  mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA), Bi. Emmy Hudson akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, uliofanyika Uwanja wa Shule ya msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akitoa salama za Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka,  wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara,  katika Uwanja wa Shule ya Msingi  Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini hapa nchini (RITA) Prof. Hamis Dihenga akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara. 
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(wa tatu kulia) akifurahia burudani kutoka kwa kikundi cha ngoma ya asili kutoka Mkoani Mara, wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Wasanii wa Kikundi cha Ngoma ya Asili cha Wagoyangi kutoka Maswa mkoani Simiyu wakitoa burudani wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Dkt.Vicent Naano mara baada ya kuwasili Mkoani Mara kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara,katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera mara baada ya kuwasili Mkoani Mara kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt.Joseph Chilongani mara baada ya kuwasili Mkoani Mara kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi mara baada ya kuwasili Mkoani Mara kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi(kushoto) akisalimiana na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Mhandisi. Hatari Kapufi,  mara baada ya kuwasili Mkoani Mara kwa ajili ya kuzindua Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, Wilaya ya Musoma na baadhi ya viongozi wa RITA mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa ya Simiyu na Mara uliofanyika  katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (katikati kwa walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mikoa ya Simiyu na Mara, mashirika ya Kimataifa na Viongozi wa kitaifa mara baada ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa watoto wenye umri chini ya wa miaka mitano na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa mikoa hiyo uliofanyika  katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkendo Manispaa ya Musoma.

Thursday, March 8, 2018

WANAWAKE WATAKIWA KUWALINDA WATOTO WA KIKE DHIDI YA MIMBA ZA UTOTONI


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga ametoa wito kwa wanawake  wote Mkoani Simiyu kuwa mstari wa mbele katika kuwalinda watoto wa kike na kuhakikisha hawakatishwi masomo kwa sababu ya kupewa mimba wakiwa (katika umri mdogo) shuleni na badala yake wamalize masomo ili watimize ndoto zao.

Kiswaga ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka,  katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Kimkoa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mjini hapo.

Amesema Serikali ya awamu ya tano imetoa fursa kwa watoto wote kupata elimu bila malipo hivyo wazazi hususani wanawake (wakinamama) wanapaswa kutimiza wajibu wao katika kuhakikisha wanawasaidia watoto wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia mienendo yao na kuwaonya wanapoenda kinyume  ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Endapo mama kwenye familia atatimiza wajibu wake wa kumwangalia na kumwonya mtoto wa kike kuachana na vitendo vitakavyopelekea kupata mimba,  huyo mtoto atakuwa salama; kwa hiyo wakinamama timizeni wajibu wenu wa kuhakikisha mnawalinda watoto wa kike kama walivyofanya wazazi wetu zamani ili waweze kumaliza shule salama” alisema Kiswaga.

Ameongeza kuwa  wazazi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kuwafichua wanaume wote waliowapa mimba wanafunzi wa kike na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua badala ya kuwa upande wa wahalifu hao na kuwatetea.

Katika hatua nyingine Kiswaga ameziagiza Halmashauri zote mkoani Simiyu kuhakikisha kwamba zinatekeleza maagizo ya Serikali katika kutenga asilimia 10 kwa ajili ya wanawake na vijana na kuzitoa kama ilivyokusudiwa ili kuyasaidia makundi hayo kupata mitaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli mbalimbali  za kuwaingizia kipato.

Aidha, ametoa wito kwa wanawake wa Mkoa wa Simiyu kuunga mkono juhudi za Serikali Mkoani humo katika uanzishwaji wa viwanda vidogo ili kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa  Mkoa wa “Wilaya Moja Bidhaa Moja”, kwa lengo la kuwezesha kujitegemea kiuchumi na kuondokana na utegemezi kwa wanaume.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Simiyu Mariam Manyangu amewataka wanawake wa Mkoa huo kufanya kazi kwa bidii na  kujiamini katika majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu, Mwenyekiti wa Maandalizi ya Siku ya Wanawake mkoani SIMIYU, Mwl. Rachel Ernest amesema Wanawake Mkoani humo wanalaani vitendo vya baadhi ya watu katika jamii kuendelea kumtumia mtoto wa kike kama kitega uchumi kwa tamaa ya kupata  ng’ombe, hivyo kumkatisha masomo ili aolewe na kushindwa kutimiza  ndoto za maisha yake .

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2018 yameadhimishwa chini ya Kauli Mbiu isemayo “Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Tuelimishe Usawa wa kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini”,   ambapo wanawake mkoani Simiyu walianza maadhimisho hayo kwa kwenda kuwaona wagonjwa(wanawake na watoto) katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo sabuni na vinywaji.

Baadhi ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu wakiwa katika maandamano kuelekea Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu (Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi, Bi. Suzana Sabuni akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Baadhi ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu wakiwa katika maandamano kuelekea Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi.
Bi. Ruth Seni Mjasiriamali kutoka MCSEKA Group Company Mjini Bariadi,  wanaojishughulisha na utengenezaji wa sabuni aina zote akitoa maelezo juu ya bidhaa hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga(hayupo pichani)  alipotembelea banda lao maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (katikati) akizungumza na wajasiriamali wa Kikundi cha CHIKOMO cha Mjini Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea banda lao la maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Mjini hapo.


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (kushoto) akimsikiliza Mjasiriamali Bi. Wilielimina Edward mara baada ya kuona bidhaa alizozitengeneza  baada ya kutembelea banda lake la maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoani Simiyu yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Simiyu Mhe. Mariam Manyangu akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Msanii Elizabeth Maliganya akitoa burudani pamoja na wasanii wengine kutoka Simiyu Band wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoani Simiyu yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo Mkoani Simiyu yameadhmisha katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bibi. Rachel Ernest akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Maadhimisho hayo .

Wednesday, March 7, 2018

MAAFISA MICHEZO WATAKIWA KUWASAIDIA VIJANA KUFIKIRI MICHEZO KATIKA MTAZAMO WA AJIRA NA BIASHARA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewataka Maafisa Michezo na Walimu wa Michezo mkoani humo kuwasaidia Vijana wa Kitanzania kutoka kwenye nadharia ya kufikiri kuwa michezo ni afya, urafiki na  burudani tu ili waanze kufikiri michezo katika mtazamo wa biashara na ajira.

Mtaka ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga semina ya  kuwajengea uwezo Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni, kwa lengo la  kuchochea maendeleo ya Michezo Mkoani Simiyu,  ambayo yametolewa na Dkt. Angela Daalmann  na Anja Henke ambao ni  Wataalam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover Nchini Ujerumani.

“Tumeleta mafunzo haya tukiamini kuwa Maafisa Michezo wote ndani ya Mkoa wa Simiyu watakuwa na msaada mkubwa kwenye kuwaandaa vijana wa Kitanzania kutoka kwenye nadharia ya kusema michezo ni afya, michezo ni upendo, michezo ni burudani ; nataka Afisa Michezo akienda kwenye implementation(utekelezaji) vijana wa mkoa wa Simiyu waanze kujenga vichwani mwao kuwa michezo ni ajira, michezo ni biashara” alisema Mtaka.

“Katika Dunia ya leo michezo ni biashara kubwa na ni ajira kubwa ya dunia ndiyo maana hapa mmefundishwa kuhusu miradi, hili suala la michezo ni burudani, michezo ni afya,  michezo ni urafiki na upendo libaki kama jambo la pili” alisisitiza

Ameongeza kuwa Maafisa Michezo pamoja na walimu wa michezo Mkoani Simiyu kupitia michezo ya UMITASHUMTA  na UMISETA wanapaswa kuwatambua watoto/vijana wenye vipaji na kuwaandaa kibiashara ili wajue kuwa vipaji vyao ni ajira zao za baadaye.

Aidha, amesema Serikali mkoani humo imedhamiria kutangaza utalii na kukuza uchumi kupitia sanaa, michezo na utamaduni na akabainisha kuwa Mkoa umeanza kutekeleza hilo kupitia  uanzishwaji wa Tamasha kubwa la michezo na utamaduni maarufu kama “Simiyu Festival” ambalo linafanyika kila mwaka na kwa mwaka 2018 litafanyika mapema mwezi Julai.

Naye Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover Dkt. Angela Daalmann amesema kwamba wamehamasika kutoa mafunzo kwa maafisa, viongozi na walimu wa michezo mkoani Simiyu ikiwa ni mara ya pili sasa, kutokana na utayari wa viongozi na watalaam mkoani humo katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya michezo.

Afisa Michezo wa Mkoa wa Simiyu, Bw.Emmanuel Athanas amesema mafunzo hayo yataamsha ari na hamasa ya michezo kwa Maafisa Michezo na Walimu wa Michezo mkoani humo na kuwasaidia katika kuibua miradi mbalimbali itakayohusianishwa na michezo (sports projects)  sambamba na kuwatafuta wadau mbalimbali kuwezesha miradi hiyo.

Naye Afisa Michezo wilaya ya Meatu, Bw. Hassan Sengulo amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua namna sahihi ya kupata fedha kwa ajili ya uendeshaji wa michezo,  hivyo watayatumia kuwaelimisha Walimu wa Michezo na Viongozi wa Vyama na Vilabu  vya Michezo namna ya kutatua changamoto ya ukosefu wa fedha za kuendeshea michezo.

Semina hii ilijumuisha jumla ya washiriki 27 kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu na baadaye ikafuatiwa na Bonanza la michezo kwa wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi kushiriki mchezo wa riadha,  ambapo wanafunzi walipata nafasi ya kukimbia mbio za mita 100, mita 400 na mita 1500 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Somanda Mjini Bariadi.

MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza katika semina ya  Maafisa Michezo, Baadhi ya walimu wa michezo na Viongozi wa Vyama vya Michezo mkoani humo  iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani  Dkt. Angela Daalmann akizungumza na  Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni (hawapo pichani) mkoani Simiyu katika Semina iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni mkoani Simiyu wakimsikiliza Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann katika Semina iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni mkoani Simiyu wakimsikiliza Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann katika Semina iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) akiteta jambo na Mtalaam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann katika Semina ya Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni mkoani Simiyu iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wanafunzi wa kike kutoka Shule ya Msingi Somanda A na Somanda B wakishiriki  mbio za mita 100 katika Bonanza la Michezo lililofanyika katika viwanja vya shule hiyo Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wanafunzi wa kiume kutoka Shule ya Msingi Somanda A na Somanda B wakishiriki mbio za mita 400 katika Bonanza la Michezo lililofanyika katika viwanja vya shule hiyo Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda B wakitoa burudani ya ngoma ya asili ya kabila la Wasukuma katika Bonanza la Michezo lililofanyika katika viwanja vya shule hiyo Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa tatu kulia mbele) akiwa katika picha ya pamoja washiriki wa Semina kuwajengea uwezo Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo shuleni mkoani humo pamoja na Dkt. Angela Daalmann  na Anja Henke ambao ni  Wataalam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover Nchini Ujerumani.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa Michezo kutoka Jimbo la Hannover nchini Ujerumani Dkt. Angela Daalmann(wa pili kushoto) na Anja Henke(kulia) mara baada ya kukamilika kwa semina kwa Viongozi, Maafisa na walimu wa Michezo mkoani humo (kushoto ) Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera.
Afisa Michezo wa Mkoa wa Simiyu, Bw.Emmanuel  Athanas akifafanua jambo katika semina ya  kuwajengea uwezo Maafisa Michezo, Viongozi wa Vyama na Vilabu vya Michezo, makocha na walimu wa michezo mkoani humo iliyofanyika Machi 06, 2018 Mjini Bariadi.

Friday, March 2, 2018

HATUJAWAKATAA WADAU WA AFYA TUNATAMBUA MCHANGO WAO, TUNAOMBA WAZINGATIE VIPAUMBELE VYA KITAIFA-RC MTAKA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali Mkoani humo haijawakataa wadau wa Afya kutoka katika Mashirika mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa wanaofanya kazi mbalimbali  katika  kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye Sekta ya Afya , bali inatambua mchango wao na inawaomba kufanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa kwenye Sekta ya Afya.

Mtaka ameyasema hayo katika mazungumzo maalum na waandishi wa Habari wakati alipokuwa akifafanua kauli aliyoitoa katika kikao kilichofanyika Februari 25 na 26 Mjini Bariadi kati ya Viongozi wa Mkoa huo na Wadau Afya mkoani humo ya kuwataka kuelekeza zaidi fedha zao katika kujibu mahitaji ya wananchi kwenye Afya badala ya semina na mafunzo kwa watumishi.

Amesema Serikali inatambua mchango wa Mashirika na wadau wa Afya Mkoani humo kutokana na mambo waliyoyafanya kuunga mkono Serikali kutatatua changamoto mbalimbali za Sekta ya Afya, ikiwa ni pamoja na kutoa magari, kujenga majengo ya upasuaji katika baadhi ya Vituo vya Afya na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.

Ameongeza kuwa pamoja na michango hiyo Mashirika mengi yanayofanya kazi Mkoani Simiyu katika Sekta ya Afya yameonekana kujikita zaidi katika kutoa fedha nyingi kwa ajili ya semina na mafunzo kwa watumishi wa Afya , badala ya kusaidia katika kutatua changamoto ambazo ni vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa pia katika Sekta ya Afya.

Aidha. Mtaka amebainisha kuwa Vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa  katika Sekta ya Afya ni pamoja na Ujenzi wa Miundombinu ya Afya ambayo ni majengo ya zahanati, vituo vya afya, vyumba vya upasuaji, hospitali), Vifaa pamoja na vifaa tiba,  ambapo alieleza kuwa Mkoa huo una upungufu wa Hospitali ya Mkoa, Hospitali mbili za Wilaya, Vituo vya Afya 112 na Zahanati 291.

“Tumepitia bajeti za mashirika haya 11 kwa ujumla wake mwaka 2018 yatatumia zaidi ya shilingi bilioni 21, hizi ni fedha nyingi ambazo kama zitafanya kazi inayoonekana huduma za Afya ndani ya mkoa zitaimarika, changamoto kubwa ambayo mimi kama mkuu wa mkoa na viongozi wenzangu tumeiona ni fedha nyingi kati ya hizo kuelekezwa kwenye mafunzo ya watumishi wa afya” alisema.

“Kwanza nimeyaomba mashirika yanayofanya kazi za Sekta ya Afya ndani ya Mkoa  kila moja kuonesha kazi wanazofanya, pili natoa wito kwa mashirika haya kuelekeza fedha nyingi kwenye kuongeza idadi ya vituo vya afya, zahanati, vifaa na vifaa tiba ili tunapojenga uwezo kwa watumishi wetu wa Afya wawe na mahali pa kwenda kufanyia kazi mafunzo wanayopata” alisisitiza Mtaka

Ameongeza kuwa Ofisi yake imeandika barua Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili Viongozi kutoka Wizara hizo mbili wakutanishwe pamoja na Viongozi wa Wizara ya Afya na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa lengo la kujadili na kuchambua tija ya fedha za wadau/mashirika hayo kwenye Sekta ya  Afya.

Mmoja wa wadau hao  Mwakilishi kutoka Shirika la Mkapa Foundation Bi.Adeline Saguti akichangia hoja katika kikao chao na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu alisema Wadau wa Afya Mkoani humo wameahidi kushirikiana na Mkoa huo  kufanyia kazi maeneo yenye uhitaji katika Sekta ya Afya.

Wadau wa Afya (mashirika ya ndani na nje ya nchi) wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu ni pamoja na AMREF, AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, Red Cross, ICAP, TAMA, INTRAHELTH, WORD VISION na BORESHA AFYA.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake Machi O2, 2018 Mjini Bariadi

Thursday, March 1, 2018

RC MTAKA AWATAKA WANANCHI, VIONGOZI SIMIYU KUTOA USHIRIKIANO UTAFITI WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi na Viongozi Mkoani humo kutoa ushirikiano kwa wadadisi na wataalam wa Takwimu katika utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi unaoendelea hapa nchini ili kuwezesha upatikanaji wa  takwimu halisi na sahihi Mkoani humo.

Mtaka ameyasema hayo katika Mkutano wake na   waandishi wa habari, wataalam wa Takwimu na Viongozi wa madhehebu ya dini uliofanyika Februari 28 Mjini Bariadi.

Amesema Utafiti huo utatoa makadirio ya uchumi jumla(macroeconomic), hususani matumizi ya kaya kwa ajili ya Pato la Taifa (Gross Domestic Product-GDP), kupata mwenendo wa matumizi ya moja kwa moja ya kaya  ili kuwezesha uchambuzi wa hali ya soko na kupata taarifa za umilikaji wa vifaa vya kudumu pamoja na nyenzo za uzalishaji wa kipato.

Amesema kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2015 kila mwananchi anawajibika kushiriki katika utafiti kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu rasmi ambazo zitatumika kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.

“ Lengo mama la utafiti huu ni kujua hali ya kipato kwa kaya zetu asije mtu akapotosha kuwa watafiti wana agenda nyingine, ndiyo maana nimeona viongozi wa Dini nao walifahamu hili ili wasaidie kuwaeleza kwa ufasaha waumini wao; Serikali inahitaji takwimu sahihi ili ipange bajeti  na kuweka mipango ya maendeleo, niwaombe wananchi na viongozi tutoe  ushirikiano” alisema Mtaka.

Aidha, amemuagiza Meneja wa Takwimu mkoani humo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ushiriki wao katika utafiti huu hususani kaya zilizochaguliwa na akamtaka yeye na wataalam wa Takwimu wa Mkoa huo kufanya mikutano katika minada na magulio pamoja na maeneo ya yenye idadi kubwa ya watu yakiwemo ya Makao Makuu ya Wilaya na miji midogo(centers) ili kujenga uelewa kwa wananchi.

Meneja wa Takwimu Mkoa wa Simiyu, Nestory Mazinza amesema tangu utafiti huu uanzae Desemba Mosi 2017 jumla ya kaya 102 zimeshafanyiwa utafiti kati ya 408 zinazotarajiwa kufikiwa mpaka kumalizika kwa zoezi hilo mwezi Novemba  2018.

Naye Bi.Joyce Luhende Mdadisi kutoka Wilaya ya Meatu amesema wanapofanya utafiti huu wanakutana na changamoto mbalimbali na kubwa ikiwa ni baadhi ya wanakaya kuogopa kutoa taarifa zinazohitajika wakati wakihojiwa hali inayopelekea kukosekana kwa taarifa sahihi.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Dini, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikiristo Tanzania(CCT) Mkoa wa Simiyu, Mchungaji Martine Samson Nketo amesema kupitia ibada  watasaidia kuwahamasisha wananchi kushiriki katika utafiti huu na kuwaeleza umuhimu wake katika mipango ya maendeleo inayopangwa na Serikali.

  Kaya zilizochaguliwa k kufanyiwa utafiti huu zinatoka katika maeneo 34 (Vijiji/Mitaa) kwenye Wilaya zote tano za Mkoa wa Simiyu yaliyopo katika kata za Nkindwabiye, Nyangokolwa, Sakwe, Nyakabindi, Dutwa, Matongo,Gilya, Sima,Mwamtani, Mwaswale, Mwamapalala, Nhobora, Zagayu, Kinang’eli, Mwanhuzi, Mwandoya, Sakasaka, Mwabuma, Lubiga, Ng’oboko, Busilili, Seng’wa, Masela, Mwamashimba, Buchambi, Badi, Nyalikungu, Kiloleli,Kalemela, Mkula na Ngasamo.

MWISHO


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika Ofisini kwake Mjini Bariadi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Donatus Weginah akifafanua jambo katika kikao cha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Meneja wa Takwimu, Mkoa wa Simiyu, Ndg.Nestory Mazinza akifanyiwa mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kati yake na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mmoja wa Wadadisi akifanyiwa mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wadadisi na Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao kati yake na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa Takwimu, Mkoa wa Simiyu, Ndg.Nestory Mazinza(wa pili kulia) na baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini mara baada ya kumalizika kwa kikao  kati yake na waandishi wa Habari, Viongozi wa Madhebu ya Dini na Wataalam wa Takwimu kilichofanyika Mjini Bariadi.

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!