Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga ametoa wito kwa wanawake wote Mkoani Simiyu kuwa mstari wa mbele
katika kuwalinda watoto wa kike na kuhakikisha hawakatishwi masomo kwa sababu
ya kupewa mimba wakiwa (katika umri mdogo) shuleni na badala yake wamalize
masomo ili watimize ndoto zao.
Kiswaga ameyasema
hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu kwa niaba
ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani, yaliyofanyika Kimkoa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi
Mjini hapo.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano imetoa fursa kwa watoto wote kupata elimu bila malipo
hivyo wazazi hususani wanawake (wakinamama) wanapaswa kutimiza wajibu wao
katika kuhakikisha wanawasaidia watoto wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia
mienendo yao na kuwaonya wanapoenda kinyume ili waweze kutimiza ndoto zao.
“Endapo
mama kwenye familia atatimiza wajibu wake wa kumwangalia na kumwonya mtoto wa
kike kuachana na vitendo vitakavyopelekea kupata mimba, huyo mtoto atakuwa salama; kwa hiyo wakinamama
timizeni wajibu wenu wa kuhakikisha mnawalinda watoto wa kike kama walivyofanya
wazazi wetu zamani ili waweze kumaliza shule salama” alisema Kiswaga.
Ameongeza
kuwa wazazi wanapaswa kutoa ushirikiano
kwa Serikali katika kuwafichua wanaume wote waliowapa mimba wanafunzi wa kike
na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua
badala ya kuwa upande wa wahalifu hao na kuwatetea.
Katika
hatua nyingine Kiswaga ameziagiza Halmashauri zote mkoani Simiyu kuhakikisha
kwamba zinatekeleza maagizo ya Serikali katika kutenga asilimia 10 kwa ajili ya
wanawake na vijana na kuzitoa kama ilivyokusudiwa ili kuyasaidia makundi hayo
kupata mitaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato.
Aidha,
ametoa wito kwa wanawake wa Mkoa wa Simiyu kuunga mkono juhudi za Serikali Mkoani
humo katika uanzishwaji wa viwanda vidogo ili kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa
Mkoa wa “Wilaya Moja Bidhaa Moja”, kwa
lengo la kuwezesha kujitegemea kiuchumi na kuondokana na utegemezi kwa wanaume.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mwenyekiti wa
Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Simiyu Mariam Manyangu amewataka wanawake wa Mkoa
huo kufanya kazi kwa bidii na kujiamini
katika majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu, Mwenyekiti wa
Maandalizi ya Siku ya Wanawake mkoani SIMIYU, Mwl. Rachel Ernest amesema
Wanawake Mkoani humo wanalaani vitendo vya baadhi ya watu katika jamii
kuendelea kumtumia mtoto wa kike kama kitega uchumi kwa tamaa ya kupata
ng’ombe, hivyo kumkatisha masomo ili aolewe na kushindwa kutimiza ndoto
za maisha yake .
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa
mwaka 2018 yameadhimishwa chini ya Kauli Mbiu isemayo “Kuelekea Uchumi wa Viwanda,
Tuelimishe Usawa wa kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini”, ambapo wanawake mkoani Simiyu walianza
maadhimisho hayo kwa kwenda kuwaona wagonjwa(wanawake na watoto) katika Hospitali
Teule ya Mkoa wa Simiyu na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo sabuni na vinywaji.
Baadhi ya wanawake wa
Mkoa wa Simiyu wakiwa katika maandamano kuelekea Uwanja wa Halmashauri ya Mji
wa Bariadi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa
Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu (Akimwakilisha
Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani, yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji
wa Bariadi.
Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi, Bi. Suzana Sabuni akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi, Bi. Suzana Sabuni akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Baadhi ya wanawake wa
Mkoa wa Simiyu wakiwa katika maandamano kuelekea Uwanja wa Halmashauri ya Mji
wa Bariadi katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa
Mjini Bariadi.
Bi. Ruth Seni Mjasiriamali
kutoka MCSEKA Group Company Mjini Bariadi, wanaojishughulisha na utengenezaji wa sabuni
aina zote akitoa maelezo juu ya bidhaa hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga(hayupo
pichani) alipotembelea banda lao maonesho wakati
wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (katikati) akizungumza na wajasiriamali wa Kikundi
cha CHIKOMO cha Mjini Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea banda lao la maonesho wakati
wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Mjini hapo.
Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga (kushoto) akimsikiliza Mjasiriamali Bi. Wilielimina
Edward mara baada ya kuona bidhaa alizozitengeneza baada ya kutembelea banda lake la maonesho
wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoani Simiyu yaliyofanyika
Kimkoa Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa
Simiyu Mhe. Mariam Manyangu akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Simiyu, katika
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika Kimkoa Mjini Bariadi
katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Msanii Elizabeth
Maliganya akitoa burudani pamoja na wasanii wengine kutoka Simiyu Band wakati
wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoani Simiyu yaliyofanyika Kimkoa
Mjini Bariadi.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo Mkoani Simiyu
yameadhmisha katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bibi. Rachel Ernest akisoma
risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Maadhimisho hayo .
0 comments:
Post a Comment