Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina ameongeza muda wa mwezi mmoja kwa
Halmashauri hapa nchini kukamilisha zoezi la upigaji chapa mifugo na kuwataka
watendaji wote wa Serikali wanaohusika kuhakikisha mifugo yote inapigwa chapa.
Waziri
Mpina ameyasema hayo leo wakati wa kuhitimisha zoezi la upigaji chapa Kitaifa
katika Kijiji cha Migato wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, zoezi ambalo lilianza
rasmi Kitaifa mwezi Desemba, 2016 na kupangwa kukamilika Desemba 31, 2017.
“Kwa
kuwa hadi sasa zoezi hili limetekelezwa kwa asilimia 38.5 kutokana na sababu
mbalimbali, Mimi Luhaga Mpina Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa Mamlaka niliyopewa chini
ya sheria ya Utambuzi, Usajili na ufuatiliaji wa mifugo ya mwaka 2010 na kanuni
yake, ninaongeza muda wa kupiga chapa mifugo kutoka tarehe 01/01/ 2018 hadi 31/01/2018”alisititiza.
Mpina amesema miongoni mwa
changamoto zilizopelekea Halmashauri nyingi kushindwa kutekeleza zoezi hilo kwa
asilimia 100 ni baadhi ya halmashauri kutokutenga fedha kwa ajili ya zoezi
hilo, kubaini mifugo kutoka nje ya nchi, baadhi ya wafugaji kushindwa kutaja
idadi halisi ya mifugo yao na baadhi ya Halmashauri kuwatoza wafugaji zaidi ya
shilingi 500 ambayo ndiyo bei elekezi, ambapo ameagiza wafugaji hao waliotozwa
zaidi ya shilingi 500 warejeshewe fedha zao.
Ameongeza kuwa hadi kufikia
Desemba 31, 2017 Halmashauri 30 hapa
nchini hazijapiga kabisa chapa mifugo, halmashauri 23 zimeendesha zoezi hilo
chini ya asilimia 10 na akaongeza kuwa orodha ya majina ya viongozi wa wilaya
hizo walioshindwa kutekeleza agizo hilo la Serikali ameyawasilisha kwa Waziri
Mkuu wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa.
“Halmashauri 30 ambazo hazijapiga
chapa kabisa hata ng’ombe mmoja na zile 23 ambazo zimepiga chini ya asilimia 10
majina ya viongozi wote na Halmashauri
husika nimekabidhi orodha hiyo kwa Waziri Mkuu, hatuwezi kuendekeza ukaidi wa
maagizo ya Viongozi Wakuu wa Nchi” alisema Mpina.
Akiwasilisha taarifa ya zoezi la
Upigaji Chapa katika Mkoa wa Simiyu, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa,
Ndg.Elias Kasuka amesema zoezi hilo mkoani humo lilianza rasmi mwezi Aprili
2017 ambapo hadi sasa ng’ombe zaidi ya 764, 933 wameshapigwa chapa kati ya ng’ombe
1,500,000.
Akitoa maoni yake baada ya
kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo, Paulo Mabula mfugaji kutoka Migato
Itilima amesema wafugaji wamelipokea kwa furaha agizo la Waziri wa Mifugo na Uvuvi
kuongeza siku za kwa ajili ya kupiga chapa kwani litawasaidia wafugaji ambao
bado hawajakamilisha ili kuondokana na changamoto ya wizi wa mifugo.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya
Itilima, Mhe.Mahamoud Mabula amemuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Luhaga
Mpina kuwasaidia wafugaji wa Wilaya hiyo na maeneo mengine ya Mkoa huo kufanya
vikao vya ujirani mwema na wale wa mikoa jirani ili kujadiliana namna ya
kuondoa changamoto ya wizi wa mifugo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Itilima Mhe.Benson Kilangi amesema viongozi na wataalam wa wilaya hiyo wamekuwa
wakiwahamasisha wafugaji kupanga matumizi bora ya ardhi ili waweze kutenga
maeneo kwa ajili ya malisho na kuyawekea miundombinu muhimu kwa ajili ya mifugo
ikiwemo maji, majosho pamoja malisho.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga
Mpina(wa pili kushoto) akipiga chapa ng’ombe katika hitimisho la zoezi la
upigaji chapa mifugo Kitaifa katika Kijiji cha Migato, Wilaya ya Itilima Mkoani
Simiyu.
Vijana wa Skauti wilaya ya Itilima wakimvisha skafu
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina alipowasili wilayani
humo kwa ajili ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo kitaifa, mkoani
Simiyu.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga
Mpina akisalimiana na Afisa Mifugo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Ally
Mzee mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kuhitimisha zoezi la
upigaji chapa mifugo Kitaifa, lililofanyika katika kijiji cha Migato wilayani
Itilima.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi (wa
tatu kushoto) akipiga chapa ng’ombe katika hitimisho la zoezi la upigaji chapa
mifugo Kitaifa katika Kijiji cha Migato, Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu ambalo
limehitimishwa na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Daudi
Nyalamu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Migato na vijiji jirani mara baada ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa
lililofanyika kijijini hapo leo.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Luhaga Mpina akizungumza na wananchi wa Kijiji cha
Migato na vijiji jirani mara baada ya
kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa lililofanyika kijijini hapo
leo.
Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe.Njalu Silanga
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Migato na vijiji jirani mara baada ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa
lililofanyika kijijini hapo leo.
Ndg.Paulo Mabula akitoa maoni yake mara baada ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina kuhitimisha zoezi la upigaji chapa Kitaifa katika
Kijiji cha Migato wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akisalimiana na Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa
wa Simiyu, Ndg.Elias Kasuka mara baada ya kuwasili Mkoani humo kwa ajili ya
kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo Kitaifa, lililofanyika katika kijiji
cha Migato wilayani Itilima.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga
Mpina akipokelewa na Viongozi wa Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu mara baada ya
kuwasili wilayani humo kwa ajili ya kuhitimisha zoezi la upigaji chapa mifugo
Kitaifa, lililofanyika katika kijiji cha Migato wilayani Itilima.