Na Stella Kalinga
Mkoa wa Simiyu leo umezindua mradi wa Kupima na Kutibu (Test
and Treat) Wale watakaobainika kuwa na Virusi vya Ukimwi bila kujali wingi wa
CD4.
Mradi huo ambao unaendeshwa na Shirika lisilo la Kiserikali
la CUAMM umezinduliwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi ambaye amemwakilisha
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki
Mjini Bariadi na kushuhudiwa na viongozi wa serikali, viongozi wa dini,
wataalam wa Afya ngazi ya Mkoa na wilaya na wadau wa Afya kutoka mashirika
mbalimbali yasiyo ya Kiserikali.
Akisoma Hotuba ya Uzinduzi wa Mradi huo kwa Niaba
ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi,
Mhe.Festo Kiswaga ametoa wito kwa wananchi Mkoani humo kujitokeza kwa wingi kupima na kujua hali zao,
na kwa wale watakaobainika kuwa na maambukizi kuanza dawa mara moja kama
wataalamu watakavyoelekeza.
Akitoa shukrani
kwa Shirika la CUAMM amesema Serikali ya Mkoa iko tayari kuhamasisha na kuweka
mazingira mazuri ya uwekezaji katika idara ya Afya kwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji
watakaofuata sheria, uwekezaji wenye tija na kusisitiza kuwa wadau watakaotaka
kushirikiana na Mkoa huo katika maeneo tofauti ilikiwemo eneo la mapambano
dhidi ya UKIMWI kujadiliana kwanza ili kuzingatia vipaumbele vya Mkoa.
Aidha, ameuagiza uongozi wa idara ya afya
Mkoa kuhakikisha mipango ya wadau wote wanaofanya kazi na Mkoa wa Simiyu inaingizwa katika mipango ya Idara hiyo (Comprehensive
Regional Health plan/CCHP) ili kujua mchango wa wadau hao na kutokubali mipango
isiyo na tija kwa wananchi.
“Mtakumbuka kuwa jukumu
la kudhibiti UKIMWI si la Serikali
peke yake bali ni la jamii kwa ujumla wakiwepo wadau mbalimbali, tukishirikiana
kwa pamoja tunaweza kufikia malengo ya sifuri tatu, yaani maambukizi mapya
sifuri, unyanyapaa kwa waathirika wa VVU sifuri na Vifo vitokanavyo na UKIMWI
sifuri” amesema.
Akitoa taarifa ya mradi wa Pima na Kutibu(Test and
Treat) ambao unatekelezwa katika Mikoa ya Simiyu na Shinyanga, Mwakilishi wa
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Shinyanga, Liberatus Sangu, Paroko wa
Parokia ya Bariadi Padre Kizito Nyanga Victor, amesema Mradi
huu unatarajiwa kutoa ushauri nasaha na kupima ,jumla ya wakazi 300,000 Simiyu sambamba na utoaji wa matibabu ya watoto wadogo 20,000 ikiwa ni moja ya mkakati wa kupunguza kasi ya maambukizi ya asilimia 3.1 kimkoa.
Kizito amesema kuwa makusudio ya mradi huo ni kuweka vituo vya upimaji
,kuimarisha maabara na vitendanishi ,kupima usugu wa VVU ,wingi wa VVU katika mwili ambapo wao kama Kanisa kwa
kushirikiana na mashirika mbalimbali wanaungana na Serikali katika mapambano
dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.
Kwa upande wake Professa Samuel Kaluvya kutoka Chuo
Kikuu cha Tiba Bugando, ambaye ndiye Mshauri Mkuu wa Mradi huu amesema kuwa Malengo ya Shirika la Ukimwi Dunia katika nchi zote asilimia
90 ya watu wanaoishi naVVU waweze kutambulika kwa kupimwa na kuweza
kuunganishwa na mfumo wa kutoa dawa na asilimia 90 ya watu wanaotumia dawa za kufubaza VVU wahakikishe
wanatumia dawa hizo ipasavyo kwa maisha yao yote .
Mradi wa Pima na Kutibu (Test and Treat) Mkoani
Simiyu utaanza kutekelezwa katika vituo viwili vya kutolea huduma za Afya Mwamapalala (wilayani Itilima) na Songambele
(wilayani Bariadi) na baadaye vituo nane na hatimaye utatekelezwa katika wilaya
zote.
Mwakilishi
wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Shinyanga, Liberatus Sangu, Paroko wa
Parokia ya Bariadi Padre Kizito Nyanga Victor akizungumza na
viongozi, wataalam wa Afya na wadau mbalimbali wa afya kabla ya Uzinduzi wa
Mradi wa Pima na Kutibu VVU (Test and Treat) Mjini Bariadi, ambao unatekelezwa
na Shirika la CUAMM kwa kushirikiana na Serikali.