Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya amesema Serikali itahakikisha madeni yote ya Vyama vya ushirika vya Msingi(AMCOS), wakulima, ushuru wa Halmashauri na Vyama Vikuu vya Ushirika (UNIONS) kwa zao la pamba ambayo bado hayajalipwa yanalipwa kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mwaka 2020.
Kusaya ameyasema hayo Aprili 29, 2020 katika kikao alichofanya na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Simiyu na wanunuzi wa pamba ambacho kimefanyika Mjini Bariadi wakati akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Simiyu.
“Serikali inayatambua madeni yote kwenye zao la pamba AMCOS na Vyama Vikuu vya Ushirika vinadai, Halmashauri zetu nazo zinadai ushuru lakini pia hata kwenye mfuko wa pembejeo; ni lengo la serikali na jitihada zinazofanywa na wizara ya Kilimo na wizara nyingine kwa kuwa hili ni suala mtambuka, kuhakikisha madeni yote yanamalizika kabla hatujaanza msimu mpya ,” alisema Kusaya.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Vyama vya msingi havijalipwa, wakulima 7000 hawajalipwa na Halmashauri, hazijalipwa ushuru wa pamba takribanishilingi bilioni 3.5, ambapo amebainisha kuwa mapato ya ndani ya Halmashauri yanategemea ushuru wa pamba kwa asilimia 70 hivyo madeni hayo yameathiri shughuli za uendeshaji wa Halmashauri.
“ Wakulima wetu 7000 bado wanadai fadha za kilo milioni 2.6, AMCOS zinadai shilingi bilioni 3.5, Chama chetu Kikuu cha Ushirika kinadai milioni 729, Halmashauri zetu zinadai bilioni 3.5 ni vema jambo hili likafanyiwa kazi na (maeneo hayo) viungo vyote hivi kwenye zao la pamba vikaunganishwa vizuri ili kuwe na ufanisi katika msimu ujao,” alisema Mtaka.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini, Bwana Boazi Ogolla akitoa taarifa kwa niaba ya wanunuzi amesema wanunuzi wanaiomba Serikali kutekeleza ahadi yake ya kulipa fidia ya hasara waliyopata wanunuzi mara baada ya kununua pamba kwa bei elekezi ya shilingi 1200 ambayo ilikuwa juu zaidi ya bei ya soko la dunia.
Ogolla amesema kushindwa kulipwa fidia hiyo kumesababisha wanunuzi kushindwa kulipa ushuru wa pamba kwa Halmashauri, vyama vya ushirika, madeni ya wakulima, malipo ya mchango wa mfuko wa pembejeo, madeni ya watoa huduma na benki(wakopeshaji).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo ameitaka serikali kutimiza ahadi hiyo ya kuhakikisha madeni yote yanalipwa kabla ya msimu kuanza ili msimu mpya usiwe na vikwazo vyovyote.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Musabila Kusaya amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Kilimo linalojengwa viwanja vya Nane nane Nyakabindi Bariadi, Simiyu na kumtaka mkandarasi ambaye ni Suma JKT kuhakikisha ujenzi unakamilika kabla ya Mei 30, 2020.
Ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka jana 2019 na lilitakiwa kukamilika machi 30 na hadi sasa limefikia asilimia 70 ya ujenzi huku changamoto ikitajwa kuwa ni mabadiliko ya mchoro.
MWISHO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya akiangalia mafuta yanayozalishwa kutokana na mbegu za pamba katika Kiwanda cha kuchambua pamba cha NGS kilichopo wilayani Bariadi wakati wa ziara yake ya siku moja Aprili 29, 2020.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya
(mwenye suti ya bluu) na viongozi wengine wakiondoa mara baada ya kukagua maendeleo
ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Kilimo linalojengwa katika Uwanja wa Nanenane Nyakabindi
Mjini Bariadi wakati wa ziara yake ya siku moja Aprili 29, 2020.
Mmoja wa Wafanyakazi katika kiwanda cha Alliance
Ginnery akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald
Kusaya(katikati) kuhusu namna mbegu za pamba zinavyochakatwa katika kiwanda
hicho kilichopo Bariadi, Aprili 29, 2020 wakati wa ziara yake ya siku moja
mkoani Simiyu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa
wa Simiyu, Bw. Mayunga George akichangia hoja katika kikao cha Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Kusaya wakati wa zaira yake ya siku moja mkoani
Simiyu, Aprili 29, 2020.