Wednesday, March 30, 2016

UONGOZI MKOANI SIMIYU WABAINI WATUMISHI HEWA 33


Kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli la kuhakiki watumishi wa Umma nchini, Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umebaini watumishi hewa 33 na watoro 29 kati ya watumishi 13,174 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za Serikali kuu.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J.Mtaka (kulia) akizungumza na viongozi wa wilaya za Mkoa wa Simiyuwakati wa tathmini ya hali ya watumishi wa Mkoa wa Simiyu jana, katika ukumbi wa mikutano katika Ofisi yake, kutoka Kushoto wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Ponsiano Nyami, Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Mhe. Rosemary Kirigini na Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe. Erasto Sima.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana mara baada kikao cha kutathmini hali ya Watumishi katika Mkoa , Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony J. Mtaka alisema uwepo wa watumishi hewa na watoro umeisababishia Serikali hasara ya shilingi 320,993,683.69 .

Mtaka alisema mara baada ya kubaini uwepo wa watumishi  watoro, amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamisha mishahara ya watumishi hao  wakiwemo walimu ambao walikwenda masomoni bila ruhusa ya waajiri wao na wale ambao mashauri yao yapo kwa muda mrefu katika Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD) mpaka mashauri hayo yatakapopatiwa ufafanuzi.
 Kutokana na idadi ya watumishi wa kada ya ualimu kuwa kubwa katika watumishi hewa na watoro kuliko kada zingine, Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umeshauri Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD) kushughulikia kwa haraka mashauri ya walimu yanayopelekwa kutoka ngazi za Wilaya na Mikoa na kutoa ufafanuzi kwa wakati, ili kuondokana hasara ya kulipa mishahara hewa.

Aidha , Uongozi wa Mkoa umeshauri Ofisi ya HAZINA na Utumishi kuona namna ya kugatua madaraka kutoka Ofisi kuu kwenda Ofisi za kanda na mikoa, ili pale mtumishi anapotakiwa kusimamishiwa mshahara wake anapostaafu,kufariki au kufukuzwa kazi iwe rahisi kuwaondoa katika mfumo wa mishahara badala ya kusubiri Ofisi kuu Dar es Salaam kuwatoa kwenye mfumo wa mishahara.


Hali ya watumishi watoro katika Mkoa wa Simiyu inaongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu yenye watumishi watoro 18, hewa mmoja (01), ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi yenye watumishi watoro 11, hewa watano (05), huku Halmashauri ya Mji wa Bariadi ikiwa na watumishi hewa watano (05), Itilima sita (06), Busega wanne na Maswa 12 ambapo Halmashauri hizi nne (04) hazina watumishi watoro. 

Monday, March 28, 2016

MTAKA AHIMIZA UFUGAJI WA SAMAKI SIMIYUMkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony John Mtaka amehimiza wataalam wa uvuvi kuanzisha  mradi wa ufugaji wa samaki katika  mabwawa ili kuwahakikishia  wananchi wa mkoa wa Simiyu upatikanaji wa kitoweo pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa vijana.

Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo katika kikao alichofanya kati ya viongozi wa taasisi za serikali, binafsi, timu za menejimenti za Mamlaka za Serikali za Mitaa (CMT), viongozi wa dini, vyama vya siasa na wadau wengine wa maendeleo kilichofanyika mwanzoni wa wiki hii,  katika ukumbi wa K.K.K.T Bariadi.
Alisema Ofisi yake itatafuta wataalam wa ufugaji wa samaki kutoka chuo cha Ukiriguru cha jijini Mwanza ambao watafanya tathmini na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kufanikisha lengo hilo.
“Hatuwezi kuendelea kutegemea samaki kutoka sehemu nyingine wakati tuna mabwawa katika mkoa wetu ambayo yanafaa kabisa kwa ufugaji wa samaki na kuwaongezea fursa ya ajira vijana wetu,” alisema Mtaka.
Baadhi ya viongozi walioshiriki kikao hicho walisema watamuunga mkono Mkuu huyo wa mkoa kwa kuwahamasisha vijana kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mradi huo.

Sunday, March 27, 2016

RC SIMIYU AAGIZA MENEJA MAMLAKA YA MAJI ACHUNGUZWE

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony J. Mtaka ameviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kumkamata na kumchunguza Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Wilayani Maswa (MAUWASA) Mhandisi. Lema Jeremia.
Mtaka ametoa agizo hilo kufuatia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Rosemary Kirigini kuwa Meneja huyo anatuhumiwa kushindwa kusimamia Mamlaka hiyo na kutoa taarifa za uongo kuhusu mwenendo mzima wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chujio la maji, katika Bwawa la New Sola lililopo katika Kijiji cha Zanzui kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Aidha, Bi.Rosemary Kirigini amesema Meneja huyo anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa  utekelezaji wa mradi huo ulikuwa ukifanyika bila uwepo wa Bodi ya Mamlaka ya Maji. “Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa maneno ya Mwenyekiti wa Bodi, anasema bodi hii imeanza kazi hivi karibuni kwa maana hiyo haikuwepo, mimi nasema  akamatwe na afikishwe mahakamani” alisema Kirigini.
Mtaka amesema pamoja na mradi wa ujenzi wa chujio, Mamlaka hiyo imekuwa ikisambaza maji kwa wananchi bila kuweka dawa, hali ambayo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama kuhara na kipindupindu.
“Unakusanya fedha kutoka kwa wananchi kila mwezi, lakini unawapatia maji yasiyo na dawa  na unaona hilo ni jambo la kawaida tu. Unakusanya shilingi milioni 20 kwa mwezi kutokana na kuwauzia maji wananchi ambao ni wateja wa mamlaka yako , lakini unashindwa kutoa shilingi milioni 1.7  kununua dawa kwa ajili ya kutibu maji, kwa nini usishukuliwe hatua?”, alihoji Mtaka.
Wakati huo huo Mhe. Mtaka amefuta maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji kilichopangwa kufanyika  kimkoa wilayani Meatu na ameelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kufanikisha maadhimisho hayo zitumike kununua madawati.
“Nimefuta maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji kwa sababu hatuwezi tukawa tunafanya sherehe  kuadhimisha wiki ya maji wakati watu wanakunywa maji ya tope” alisema Mtaka.


Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!