Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony J. Mtaka amepiga
marufuku tabia ya askari na watendaji wengine wa
mwekezaji MWIBA Holdings Limited wa
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao wilayani Meatu, ya kuwakamata
wananchi na kuwafanyia mahojiano katika Ofisi zao , na kuwataka kufuata sheria na
kukitumia kituo cha polisi cha Makao kufanya mahojiano.
Mkuu wa Mkoa aliyasema hayo
jana alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Makao kata ya Mwangudo wilayani
Meatu katika mkutano wa hadhara, mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wananchi
hao dhidi ya Mwekezaji MWIBA Holdings Limited, ikiwemo unyanyasaji wa wananchi,
kukiukwa kwa makubaliano ya mikataba ya utwaaji ardhi na mkataba wa uanzishwaji
wa Lanchi.
Akiwasilisha malalamiko
yake kwa Mkuu wa Mkoa mmoja wa wananchi wanaodaiwa kupigwa na kufanyiwa vitendo vya
unyanyasaji katika ofisi za MWIBA Holdings
Limited, Bibi. Asteria Godson mkazi wa kijiji cha Makao alisema, alichukuliwa
nyumbani kwake na kupelekwa katika moja ya ofisi za mwekezaji huyo ambako
alipigwa na kusababishiwa maumivu makali na kuvunjika mkono wa kulia ambao hadi
sasa hata baada ya kupata matibabu, bado hauwezi kufanya kazi sawasawa.
“Mimi nilikuwa nimelala
ndani kwangu wakaingia watu ambao sikuweza kuwatambua wakitaka niwaeleze mahali
alipo mume wangu, nikawaambia mume wangu hayupo wakaanza kunipiga, walinipiga
baadae wakanichukua mpaka ofisi za MWIBA huko nako walinipiga na kunifanyia
vitendo vingi vya unyanyasaji. Kutokana na kile kipigo sasa hivi mkono wangu
mmoja haufanyi kazi”alisema Asteria.
Akipokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa, Afisa Uhusiano wa MWIBA Holdings Limited Bwana
Msafiri Clarenes alisema wamekubali na watatekeleza kama
ilivyoelekezwa, ambapo alimuomba Mkuu wa Mkoa atoe maelekezo kwa wananchi wa Mako kuacha
kuchungia mifugo katika eneo la uwekezaji.
Katika kukabiliana na
tatizo la eneo la malisho ya mifugo, Mtaka alisema Serikali iliweka mpango wa
matumizi bora ya ardhi ambao unaeleza kuwa litatengwa eneo maalum kwa ajili ya
machungo ambalo litatumika kipindi ambacho majani yatakuwa yamepungua kuanzia
mwezi Julai hadi mvua zitakapoanza kunyesha.
Akitoa ufafanuzi juu ya
eneo la kulishia mifugo Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Bwana
Emmanuel Lugamila alisema, eneo hilo lipo ndani ya Jumuiya ya Hifadhi ya
Wanyamapori (WMA) Makao na linatarajiwa kuwekewa alama za kudumu mwezi
Juni,2016 ili wananchi waweze kulitambua.
Wakati huo huo Mkuu wa
Mkoa amewaasa wananchi kuachana na tabia ya kupangisha mifugo ambayo ni maarufu
katika Maeneo hayo kama LUBAGA, kwa kuwa ni chanzo cha migogoro kati ya
wafugaji, badala yake viongozi wa vijiji wawatambue watu wenye mifugo katika
maeneo yao na kuepuka kwenda katika maeneo ambayo hawaruhusiwi kuchungia.
Wananchi wa kijiji cha Makao wamekuwa na Mgogoro wa kimkataba na Mwekezaji MWIBA Holdings Limited ambao unaendelea kutafutiwa suluhu kwa mujibu wa sheria.