Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu nayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa ametoa
wito kwa wadau kuendelea kutoa msaada wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu
kwa kuwa hili ni hitaji endelevu kwa watu hao.
Mhe. Ikupa ameyasema hayo jana Februari 27, 2019
wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Serikali wilayani Busega mkoani
Simiyu wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Amewashukuru
viongozi wa Wilaya ya Busega kwa namna inavyowasaidia watu wenye ulemavu katika
kuwapatia vifaa saidizi huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya
jitihada za kuwatafutia na kuwapatia watu wenye ulemavu vifaa hivyo kwa kadri
vitakavyopatikana.
“Napenda
kuwashukuru viongozi wa Busega kwa namna wanavyowasaidia watu wenye ulemavu
kupata vifaa saidizi kama fimbo nyeupe kwa wasioona, baiskeli na viungo bandia
kwa walemavu wa viungo, mafuta kwa wenye ualbino, lakini niwaombe wadau
waendelee kuwasaidia kwa kuwa hili ni hitaji endelevu katika kuishi kwao.” alisema
Mhe. Ikupa.
Katika hatua
nyingine Mhe. Naibu Waziri amesisitiza Kamati za watu wenye ulemavu kupewa
miongozo ya namna ya kuziendesha kamati hizo, ili ziweze kutimiza majukumu yake
ipasavyo na kuzitaka kutoa taarifa kuhusu fursa na masuala mbalimbali
yanayowahusu walemavu katika maeneo yao.
Vile vile Mhe.
Ikupa amesema Serikali inatarajia kuanzisha mfuko wa watu wenye ulemavu ambao
utakuwa ukishughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja
na kutoa ruzuku kwa vyama vya walemavu.
Akitoa taarifa Mkuu
wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera, amesema Serikali wilayani imetoa baiskeli
17 kwa watu wenye ulemavu wa viungo, zaidi ya fimbo nyeupe 50 kwa wasioona,
mafuta kwa watu wenye ualbino na Halmashauri imeandaa mpango maalum wa Mfuko wa
Bima ya Afya(CHF) iliyoboreshwa kwa ajili ya huduma za afya kwa walemavu.
Kwa upande wao
watu wenye ulemavu wameiomba Serikali na wadau kuendelea kuwapa msaada wa vifaa
saidizi , kupewa elimu ya kuunda vikundi na kuandaa maandiko ya miradi na kutoa
semina elekezi kwa kamati za watu wenye ulemavu.
“Mahitaji ya
walemavu bado ni makubwa tunaomba wadau mbalimbali waendelee kutukumbuka kutupa
msaada wa vifaa saidizi kama fimbo nyeupe kwa wasioona, viungo bandia na
baiskeli kwa walemavu wa viungo lakini na mafuta kwa wenzetu wenye ualbino”
alisema Katibu wa SHIVYAWATA Wilaya ya
Busega, Makasi Egonjo.
“Tunaishukuru Serikali
kwa kutusaidia kwenye mahitaji yetu mengi lakini tunaendelea kuomba wasichoke
kutusaidia, tunaomba maafisa ustawi wa jamii wawafikie watu wenye ulemavu mpaka
waliopo vijijini ili tuwe na elimu kuhusu mambo yanayotuhusu na fursa za mikopo
na ujasiriamali” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona, John Daniel
Naye Mwakilishi
wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amemhakikishia Naiba waziri Ikupa kuwa Mkoa wa
Simiyu utaendelea kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa katika ziara yake
na kuhakikisha walemavu wanashirikishwa na kufikiwa katika fursa mbalimbali.
Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa amehitimisha
ziara yake ya siku tatu mkoani Simiyu Febrauari 27, 2019 ambapo alipata nafasi
ya kuzungumza na viongozi wa serikali,
watu wenye ulemavu na kukagua mradi wa kitalu nyumba katika Halmashauri zote
sita za Mkoa wa Simiyu.
MWISHO
Katibu
wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
ulemavu (SHIVYAWTA) Wilaya ya Busega, Makasi Egonjo akiwasilisha taarifa ya
watu wenye ulemavu kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati wa ziara yake Wilayani
humo Februari 27, 2019
Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, akizungumza
na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu
wilayani Busega, wakati wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019.
Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, akizungumza
jambo na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu wilayani Busega, wakati wa ziara yake
Wilayani humo Februari 27, 2019.
Mkuu wa Wilaya ya
Busega, Mhe. Tano Mwera akiwasilisha taarifa ya wilaya kwa Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa, wakati
wa ziara yake Wilayani humo Februari 27, 2019.
Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa akiwaaga
baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali pamoja na watu wenye ulemavu
wilayani Busega(baadhi hawapo pichani) mara baada ya kukamilisha ziara yake
wilayani humo, Februari 27, 2019
Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe. Stella Ikupa(wa pili
kushoto) alipotembelea Ofisi za CCM Wilaya, wakati wa ziara yake ya kikazi
wilayani humo, Februari 27, 2019.
Baadhi ya viongozi na
watendaji wa serikali pamoja na watu wenye ulemavu wilayani Busega wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia walemavu, Mhe.
Stella Ikupa, wakati alipotembelea Kitalu nyumba katika ziara yake wilayani
humo Februari 27, 2019.