Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa
amewashauri Vijana nchini, kuondokana na dhana ya kuwa shughuli za kilimo ni za
Wazee na badala yake watumie vitalu nyumba kujifunza kilimo chenye tija na
hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi.
Ikupa ametoa ushauri
huo wilayani Maswa wakati alipowatembelea Vijana katika kitalu nyumba
katika kata ya Binza akiwa katika ziara yake wilayani humo Mkoani
Simiyu Februari 25, 2019.
IKUPA amesema Vijana
wanapaswa kuachana na dhana potofu kuwa kilimo ni shughuli
inayopaswa kufanywa na Wazee, badala yake watumie fursa za mafunzo ya kilimo na
wakawe mabalozi ndani ya jamii kuwa kilimo kinaweza kuwapatia ajira na kipato.
“ Kilimo kinaweza kuwatoa vijana kutoka
mahali fulani kikawapeleka mahali pengine tena wakawa na uwezo mzuri kifedha
kuliko hata wale walioajiriwa katika kazi za maofisini, niwashauri vijana
muione fursa kupitia vitalu nyumba ondoeni dhana kwamba eti kilimo ni kazi ya
wazee si kweli” alisema.
Ameongeza kuwa vijana wanayo nafasi ya
kupata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
na Halmashauri zao hivyo wachangamkie fursa hiyo kupata mikopo itakayowawezesha
kuendeleza shughuli zao za uzalishaji ikiwemo kilimo kupitia vitalu nyumba.
Katika hatua nyingine Mhe. Ikupa amesema
ni vema Halmashauri zikazingatia masuala ya watu wenye ulemavu katika mipango
ya bajeti zao ili ziweze kusaidia katika utatuzi wa baadhi ya changamoto za
watu wenye ulemavu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwatumia
wakalimani wa lugha ya alama ili waweze kusaidia mawasiliano kati ya walemavu
wa kusikia na makundi mbalimbali ya watu ikiwemo viongozi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt.
Seif Shekalaghe amekiri kupokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Naibu
Waziri Ikupa na kumhakikishia kuwa watu wenye ulemavu watalindwa,
watashirikishwa katika fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa Kitalu
nyumba.
Nao baadhi ya vijana wanaojihusisha na
utekelzaji wa mradi wa Kitalu nyumba katika Kata ya Sola wameishukuru Serikali
na kuomba ipanue wigo wa kuwafikia vijana kupitia mradi huu ili vijana wengi
waweze kufikiwa mpaka ngazi ya Kata.
“ Mimi ninaishukuru Serikali yetu kwa
kutuletea mradi wa kitalu nyumba, tumeshajifunza namna ya kutengeneza vitalu
nyumba, kilimo bora chenye tija kupitia mradi huu, tunaomba mradi upelekwe
mpaka ngazi ya kata ili vijana wengi waweze kunufaika zaidi” alisema
Rachel Paulo mkazi wa Sola Maswa.
Naibu Waziri Ikupa,
anaendelea na ziara yake Mkoani Simiyu ambayo itahitimishwa tarehe 27 Februari
2019, akiwa wilayani Maswa Naibu waziri ametembelea kitalu nyumba kilichopo
Sola na kuzungumza na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu.
MWISHO
Baadhi ya Viongozi wilayani Maswa na wananchi wa Kata ya Sola
wakisikiliza Naibu waziri Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa (hayupo pichani),
wakati akizungumza nao mara baada ya kutembelea na kuona utekelezaji wa Mradi
wa kitalu nyumba katika Kata ya Sola Wilayani Maswa, Februari, 25, 2019.
Mkuu
wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe akimkaribisha Naibu waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa mara baada ya kuwasili
wilayani humo ka ajili ya ziara ya kikazi Februari 25, 2019.
Baadhi
ya viongozi, watendaji na watu wenye ulemavu wakimsikiliza Naibu waziri Ofisi
ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa (hayupo pichani) mara
baada ya kuwasili wilayani humo ka ajili ya ziara ya kikazi Februari 25, 2019.
Mwakilishi
wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo akizungumza na baadhi ya viongozi, watendaji na
watu wenye ulemavu wilayani Maswa wakati wa Ziara yake ya kikazi Februari 25,
2019.
Naibu
waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa akizungumza jambo na Mkuu
wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe wakati wa Ziara yake ya kikazi
wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Februari 25, 2019.
0 comments:
Post a Comment