Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga
amesema Serikali wilayani humo itaendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa
katika fursa za kiuchumi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na
utegemezi.
Kiswaga ameyasema hayo wakati wa ziara ya Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe.
Stella Ikupa Wilayani Bariadi, ambayo ililenga kujionea utekelezaji wa mradi wa
kitalu nyumba na masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu.
Amesema katika mradi wa kitalu nyumba ambao
utahusisha vijana 100 atahakikisha vijana wenye ulemavu wanashirikishwa kupata
elimu ya ujenzi wa kitalu nyumba na kilimo cha kisasa chenye tija kupitia mradi
huo ili waweze kujiajiri na kujipatia kipato.
Aidha, katika mradi wa ushonaji unaotarajiwa kuanza
kutekelezwa hivi karibuni katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi atakahikisha sehemu ya washiriki katika miradi
huo ni watu wenye ulemavu.
“Tunatarajia kuanza mradi wa ushonaji hapa Bariadi
Mjini na tayari tuna vyerehani 50 kwa
hiyo tutahakikisha watu wenye ulemavu wamejumuishwa ili nao wanufaike na
mradi huu ambao utawasaidia wananchi kupata kipato na Halmashauri kupata chanzo
cha mapato pia” alisema Kiswaga.
Kwa upande wao watu wenye ulemavu pamoja na kuishukuru
serikali kwa kushughulikia changamoto
zinazowakabili wameomba Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia
kwa watu wenye ulemavu na kuongeza walimu wa elimu maalum.
Vile vile wameomba watu wenye ulemavu wapewe
kipaumbele katika suala la ajira na mafunzo mbalimbali yakiwepo ya Jeshi la
Kujenga Taifa ili nao wawe sehemu ya kutegemewa katika jamii badala ya kuwa
tegemezi.
“Tunaishukuru Serikali kutusaidia kutatua changamoto
mbalimbali lakini tunaendelea kuiomba iboreshe mazingira ya kujifunzia kwa
watoto wenye ulemavu kwa kuongeza madarasa na wataalam wa lugha ya alama, ili
nao wapate haki yao ya msingi ya elimu bora”alisema Alex Benedicto Makamu Mwenyekiti
wa Chama cha Wasiosikia
Akijibu baadhi ya changamoto za watu wenye ulemavu, Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe.
Stella Ikupa amesema Serikali imeendelea kuajiri watu wenye ulemavu katika kada
mbalimbali huku akitoa wito kwa Halmashauri kuweka mikakati ya kutafuta
wataalam wa lugha ya alama ili waweze kuwasaidia walemavu wasiosikia
kuwasiliana.
Kuhusu miundombinu Mhe. Ikupa ametoa wito kwa
taasisi zinazoendelea kujenga majengo zizingatie ujenzi wa miundombinu rafiki
kwa watu wenye ulemavu na kwa upande wa majengo ya zamani taasisi zione namna
ya kufanya marekebisho madogo ili ziweze kufikika kirahisi na watu enye ulemavu
katika kupata huduma.
Naibu Waziri Stella Ikupa akiwa wilayani Bariadi
amezungumza na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu pamoja na kutembelea
mradi wa Kitalu nyumba ili kujionea utekelezaji.
MWISHO
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa akipokelewa na baadhi ya
viongozi wa Wilaya ya Bariadi kuelekea kwenye kikao kuzungumza na viongozi hao
na watu wenye ulemavu Mjini Bariadi, wakati akiwa katika ziara yake ya
kikazi Wilayani humo, Feburuari 2019.
Kiongozi wa Chama cha Watu wenye ulemavu wa kusikia,
Alex Benson akichangia hoja katika kikao
cha Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye
Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu Mjini
Bariadi, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani humo, Feburuari 2019.
Katibu wa SHIVYAWATA Wilaya ya Bariadi, Zizi Kubilu akiwasilisha
taarifa ya walemavu kwa Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella
Ikupa na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu Mjini Bariadi, wakati akiwa
katika ziara yake ya kikazi Wilayani
humo, Feburuari 2019.
Mkalimani wa lugha ya alama(mbele kulia)
akiwatafsiria baadhi ya watu wenye ulemavu wa kusikia hotuba ya Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella
Ikupa, wakati akizungumza na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu
Mjini Bariadi, alipokuwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani humo, Feburuari 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga
akiwasilisha taarifa ya Wilaya kuhusu watu wenye ulemavu kwa Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella
Ikupa, wakati akiwa katika ziara yake ya
kikazi Wilayani humo, Feburuari 2019.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa(aliyepo kwenye gari)
akizungumza na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu wilayani Meatu baada ya kutembelea Kitalu nyumba kilichopo Nyakabindi
, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi
Wilayani Bariadi, Feburuari 2019.
Baadhi ya viongozi na watu wenye ulemavu Wilaya ya Bariadi
wakipewa maelezo juu kilimo kinavyofanyika katika Kitalu nyumba kilichopo Nyakabindi
Baadhi ya wakuu wa idara halmashauri ya Wilaya ya
Bariadi na Mji wa Bariadi wakifuatilia kikao cha Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa(hayupo
pichani ) na viongozi wa Serikali na watu wenye ulemavu wilayani Bariadi, wakati
akiwa katika ziara yake ya kikazi
Wilayani Bariadi, Feburuari 2019
0 comments:
Post a Comment