Wakuu wa
Idara wametakiwa kuzingatia ushauri wa Wakaguzi wa Ndani wa kujibu hoja inavyotakiwa
ili Halmashauri zao zisipate hati zenye masahaka au hati chafu..
Hayo
yalisemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne A.Sagini wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa fedha, mipango na bajeti, uwekezaji,
uimarishaji ukusanyaji wa mapato, taratibu za ukaguzi wa ndani na manunuzi ya
umma kwa wahasibu, wakaguzi wa ndani, maafisa ugavi na maafisa mipango wa
Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri
ya wilaya ya Meatu.
Mbali
kuzisaidia Halmashauri kutopata hati za
mashaka au chafu kutoka kwa mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) taarifa
za mkaguzi wa ndani zinasaidia menejimenti kutambua kasoro za mfumo wa
usimamizi wa fedha ndani ya taasisi na kuziondoa kwa kuzingatia sheria na
kanuni za umma.
“Mkaguzi wa
Ndani ni Jicho la Afisa Masuuli kumwezesha kujua kama matumizi ya fedha za Umma
yanafuata taratibu na miongozo ya usimamizi wa fedha za Umma iliyopo na
anawakumbusha wakuu wa Idara na Vitengo kujibu Hoja za Mkaguzi wa Ndani ya siku
saba kama sheria inavyotaka, ” , alisema Sagini
Sagini
alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga katika umuhimu wa usimamizi wa rasilimali
fedha ikiwa kama kiungo cha kuwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi, ambapo
wataongeza utambuzi, namna ya kuanzisha wazo la uwekezaji na namna ya kupata
fedha za miradi katika kufanya uwekekezaji katika sekta ya umma.
Kwa upande
wake Thomas Magambo ambaye ni mtaalamu mshauri wa mradi wa PFMRP IV Mkoa wa
Mara na Simiyu amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuboresha mfumo wa manunuzi
ya umma, ukusanyaji mapato na uwekezaji ndani ya halmashauri ili kuongeza
ukusanyaji mapato na kuwezesha kupata hati safi.
Naye Donatus Wegina, Katibu Tawala Msaidizi wa
Mipango na Uratibu katika Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, alisema kuwa mafunzo
hayo yamefanyika ili kuwajengea uwezo wasimamizi wa fedha za ndani, ukaguzi wa
ndani, manunuzi, mipango na bajeti ili mipango inayoandaliwa iweze kusaidia Halmashauri
kupata hati safi na kuhakikisha kuwa fedha za Umma zinatumika kwa kufuata miongozo
na taratibu za kibajeti kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Katika ukaguzi
uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa hesabu za
mwaka 2014/2015 Halmashauri za Itilima, Bariadi Mji na Busega zimepata hati
safi wakati huo Halmashauri za Meatu, Maswa na Bariadi vijini zimepata
hati zenye mashaka.