Na Stella Kalinga
(Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu)
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe. Anthony J. Mtaka amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani humo
kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha Maafisa kilimo wa Vijiji,Kata na Wilaya
kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Mtaka ametoa agizo hilo
wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi na Maafisa Kilimo katika kikao
kilichofanyika Mjini Bariadi ambacho kilihudhuriwa na Wakuu wa wilaya,Wenyeviti
wa Halmashauri,Wakurugenzi na Makatibu Tawala Wilaya kutoka katika wilaya zote tano za mkoa huo.
Mtaka amesema Maafisa
Kilimo wanapaswa kuwezeshwa kwa kupewa vyombo vya usafiri kama pikipiki na
magari pamoja na mafuta, ili waweze kuwafikia wakulima katika maeneo yao kwa
ajili ya kuwapa ushauri wa kitaalam kila wanapowahitaji katika kuendeleza
kilimo bora na chenye tija.
“Mwaka huu kilimo kwa
mkoa wetu ni kipaumbele cha pili na Halmashauri
za Mkoa huu zinategemea kilimo kwa takribani asilimia 90 ya mapato yake ya
ndani, ipo haja kuwawezesha maafisa
kilimo kwa kuwa wana mchango kubwa katika mapato ya Halmashauri. Ningependa
kuona mwaka 2016/2017 hadhi ya Maafisa Kilimo inapanda, Wakurugenzi muwathamini
hawa wataalam ndiyo wanaowasaidia kupata hayo mapato katika pamba, choroko,
dengu, mpunga na mazao mengine”, alisema Mtaka.
Aidha, kufuatia
makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania
na India yaliyofanywa hivi karibuni kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wa India juu ya biashara
ya mazao ya jamii ya mikunde kama choroko, dengu na mbaazi takribani tani
milioni sita, Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu unayo fursa kubwa ya kuzalisha mazao haya kwa takribani asilimia 60
kama ilivyo katika zao la pamba, kwa kuwa kuna ardhi yenye rutuba na wananchi
wanalima mazao hayo.
Katika kufikia azma
hiyo, Mtaka amewataka Maafisa kilimo kutumia muda huu kufanya tafiti katika
vituo mbalimbali vya utafiti juu ya
mbegu bora, kabla ya msimu wa mazao ya mikunde haujaanza ili wakati utakapofika
uzalishaji wa mazao hayo ufanyike kitaalam na kuongeza uzalishaji kuliko ilivyo
sasa.
Wakati huo huo Mtaka
amewaagiza viongozi na Maafisa Kilimo kutoka katika wilaya zote kuwa na
mashamba ya mifano ambayo yatatumika kama mashamba darasa kwa wananchi ili
wananchi wajifunze kutoka kwao kwa kuwaonesha kuwa maelezo wanayoyatoa
yanatekelezeka.
Kwa upande wake Katibu
Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji katika Sekretarieti ya
Mkoa wa Simiyu, Bw. Joseph Nandrie ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Simiyu
kulima mazao yanayostahimili ukame kama mihogo na mtama ili kukabiliana na baa
la njaa.
Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akikiri kupokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa amewataka
Maafisa Kilimo kuandaa mipango kazi kwa ajili ya utekelezaji wa maelekezo
yaliyotolewa na kuyawasilisha kwa viongozi wao wa wilaya ili yaanze
kutekelezwa.
Jumla ya Maafisa kilimo
203 kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Busega, Itilima, Maswa ,
Meatu na Halmashauri ya Mji Bariadi
wameshiriki katika kikao hiki ambacho kililenga kutoa mwelekeo wa Sekta ya
Kilimo kama kipaumbele cha Pili Mkoani Simiyu kwa mwaka 2016/2017.