Sunday, July 30, 2017

SIMIYU YAJIPANGA KUTENGENEZA AJIRA KUPITIA SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO

Mkoa wa Simiyu umejipanga kurasimisha kazi za sanaa, utamaduni na baadhi ya michezo ili kutengeneza ajira kwa wananchi  ambazo zitasaidia kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu Tamasha la “Simiyu Jambo Festival” litakalohusisha mashindano ya mbio za baiskeli na ngoma za asili ambalo litafanyika Agosti 06, 2017 Mjini Bariadi.

Amesema Mkoa wake umekusudia kuandaa utaratibu wa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuona namna ambayo kazi za sanaa,utamaduni na michezo zinazofanyika katika mkoa wa Simiyu zinaweza kufanywa kibiashara na zikawanufaisha wananchi.

Ameongeza kuwa vikundi vya sanaa na utamaduni vya Mkoa wa Simiyu vitapewa mafunzo ya namna ya kufanya kazi zao kitaalam katika viwango vinavyotakiwa, ili kazi ziweze kuuzika ndani na nje ya mkoa hususani kipindi ambacho watalii wengi wanakuja hapa nchini kwa kuwa mkoa huo unapakana na mikoa yenye hoteli nyingi za kitalii.

“Simiyu ni mkoa unaopakana na mikoa yenye Hoteli za kitalii, tungehitaji tufike mahali ambapo kazi za utamaduni na sanaa ndani ya mkoa wetu zinafanywa kibiashara;wakati watalii wanapotembelea hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwenda kwenye  hoteli za kitalii wasiishie kupiga picha, tungehitahi vikundi vyetu vya sanaa na utamaduni viuze kazi zao huko” amesema Mtaka

.Aidha, Mtaka amefafanua kuwa katika kufanikisha hayo Mkoa umeanza na mchezo wa  Mbio za baiskeli kupitia Mashindano yatakayofanyika Agosti 06, mwaka huu ambapo Mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Tulia Ackson.

 Amesema vijana wengi wa Mkoa huo wanafanya vizuri katika mchezo huo hivyo watafanyiwa utaratibu wa kupewa mafunzo ya kuwaimarisha zaidi katika mchezo huo, ili Mkoa ufikie hatua ya kutoa wawakilishi katika nchi kwenye mashindano makubwa ya mbio za baiskeli kama ya Jumuiya ya Madola na Olimpiki.

“Tuko kwenye kutambua vipaji vya watu na tunajaribu kuona kila mwananchi aliyeko ndani ya mkoa wa Simiyu kile ambacho amejaliwa na Mwenyezi Mungu kinamsaidia kujipatia kipato chake.Tunafanya yote haya kwenye Mkoa kwa kuwa tunaamini Kipaji cha mtu ni biashara na kipaji ni ajira” amesema Mtaka.


 Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama cha baiskeli Mkoa wa Simiyu Joseph Paul amesema kuwa chama chake kinaiwashukuru kampuni ya Jambo Food Product kwa kudhamini mashindano hayo ya Mbio za baiskeli ambayo yatahusisha makundi matatu; kilometa 200 kwa wanaume, Kilometa 80 wanawake na Kilometa Tano kwa watu wenye Ulemavu.


Paul amesisitiza kuwa chama chake kimejipanga vilivyo na zaidi ya washiriki  150 wamethibitisha kushiriki mashindano hayo kutoka katika mikoa ya Simiyu,Geita,Mwanza, Shinyanga na Arusha


Naye Meneja wa Masoko wa Kampuni ya Jambo Food  Product Anthony Paul,amesema Kampuni hiyo ambayo ni wadhamini wakuu wa Mashindano hayo wamejipanga kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo Pikipiki itakayotolewa kwa mshindi wa Kwanza (wanaume) na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 8 zitashindaniwa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka akiiendesha pikipiki itakayotolewa na Kampuni ya Jambo Food  Product kama zawadi ya mshindi wa kwanza wanaume katika Mashindano ya baiskeli yatakayofanyika Agosti 06 mwaka huu Mjini Bariadi, wengine ni baadhi ya washiriki wa mashindano hayo


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kushoto)akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)ofisini kwake kuhusu Simiyu Jambo Festival itakayohusisha mashindano ya Mbio za Baiskeli na burudani ya ngoma za asili yatakayofanyika Agosti 06 mwaka huu mjini Bariadi, (kushoto ) Mwenyekiti wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Joseph Paul.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Jambo Food  Product Anthony Paul (wa pili kushoto)akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu zawadi zitakazotolewa na kamunu hiyo kwa washindi wa mashindano ya baiskeli yatakayofanyika Agosti 06, 2017 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka (mwenye pikipiki) akiwa katika picha ya pamoja na baadh ya washiriki wa mashindano ya mbio za Baiskeli kutoka mkoani humo ambayo yatafanyika Agosti 06, 2017 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na wadau wa michezo wakimsikiliza mkuu wa Mkoa wa Simiyu akizungumza na waandishi wa Habari juu ya “Simiyu Jambo Festival” tamasha litakalohusisha Mashindano ya Baiskeli na burudani ya wagika , wagalu na ngoma za asili Agosti 06, 2017.
Manju wa Kundi la Wagika, Sadam Chulichuli(katikati) akiwaeleza waandishi wa habari juu ya ushiriki wao katika Tamasha la “Simiyu Jambo Festival” litakalohusisha mashindano ya Baiskeli na Burudani kutoka kwa wagika, wagalu na ngoma nyingine za asili.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kushoto)akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)ofisini kwake kuhusu Simiyu Jambo Festival itakayohusisha mashindano ya Mbio za Baiskeli na burudani ya ngoma za asili yatakayofanyika Agosti 06 mwaka huu mjini Bariadi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka mwenye kipeperushi(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Baiskeli, Viongozi wa Wagika na Wagalu  na baadhi ya wadau wa michezo na utamaduni mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Mashindano ya baiskeli yatakayofanyika Agosti 06, 2017.


Friday, July 28, 2017

SIMIYU YAJIPANGA KIMKAKATI KUWASAIDIA WAFUGAJI KUFUGA KISASA

Serikali Mkoani Simiyu imejipanga  kuweka mkakati maalum utakaowasaidia wafugaji mkoani humo kutoka kwenye ufugaji wa kuhama hama na kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika kikao maalum cha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wafugaji, wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya mkoa  kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini Bariadi.

Mtaka amesema Mkoa wake umedhamiria kuwatambua wafugaji na maeneo yao na kutoa elimu juu ya upimaji wa maeneo hayo ili yatumiwe kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhama hama kufuata maji na malisho katika mikoa mingine.

“Hatuwezi kuwa Serikali ambayo ina majibu mepesi kwenye mambo ya msingi, lazima tupate majawabu ya wafugaji ndani ya mkoa wetu, tufike mahali ambapo mfugaji kutoka mkoa wa Simiyu hatapigwa faini kwenye mikoa mingine kwa sababu ya kutafuta maji na malisho”amesema Mtaka.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali kupitia Wataalam wa Kilimo na Mifugo watatoa elimu kwa Wafugaji watakaorasimisha maeneo yao, ili wayatumie kupata malisho ya mifugo na kuweka miundombinu muhimu ya mifugo kama vile malambo, majosho na visima katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji na malisho ya mifugo.

Ameongeza kuwa, Mkoa unaandaa utaratibu ambapo shule za Serikali zitakapokuwa zinafungwa, Idara ya Kilimo na Mifugo itatumia madarasa hayo kutoa elimu ya ufugaji na kilimo bora kwa wananchi.

Sanjali na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema zoezi la kupima maeneo ya wafugaji na kuweka miundombinu muhimu ya mifugo litakapokamilika Serikali imepanga kuweka mizani katika minada yote mkoani humo ili wafugaji wasidanganywe na kuibiwa wanapouza mifugo yao.

Kwa upande wake Padre John Kasembo ambaye ni Mwezeshaji na Mshauri katika Masuala ya Uongozi, Ujasiriamali na  Maendeleo ametoa wito kwa Wafugaji wa Mkoa wa Simiyu kukubali kufanya ufugaji wenye tija na waungane na Viongozi katika mipango inayoandaliwa kwa ajili ya kufikia ufugaji bora kwa manufaa yao.

Padre Kasembo amesema ili wafugaji wafuge kisasa wanapaswa kuwa na maeneo, miundombinu ya kisasa, malisho na kufuata sheria na taratibu, hivyo akawaasa wakubali kubadilika katika namna ya kufikiri, kutenda, kuweka vipaumbele na kushughulikia changamoto ili wapate matokeo chanya.

Daktari wa Mifugo wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Gamitwe Mahaza amesema Wafugaji wengi pia ni Wakulima, hivyo ni vema wakatumia masalia ya mazao kwa ajili ya malisho badala ya kuyaacha mashambani yakaharibika; akasisitiza juu ya urasimishaji wa maeneo yao ili miundombinu kama visima iwekwe kusaidia ukuaji wa malisho ya asili na upandaji wa malisho ya kisasa.

Naye Mtaalam wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC), Mhandisi George Mulamula ameeleza kuwa upimaji katika maeneo ya wafugaji unaweza kufanyika kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo zinazotumia mifumo ya TEHAMA , kama vile matumizi ya satelite na ndege zisizotumia rubani (drones) ambazo zitasaidia zoezi hilo kufanyika kwa  usahihi mkubwa na haraka.

Pia Mhandisi Mulamula amesema kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wafugaji wataweza kupata mafunzo na taarifa mbalimbali za mifugo kupitia simu zao za mikononi, kujua bei na soko la mifugo na kutambua mifugo yao hivyo kupunguza wizi wa mifugo.

Viongozi wa Wafugaji na Wafugaji kwa pamoja wameshukuru Uongozi wa Mkoa kuona umuhimu wa kushughulikia changamoto zao ambapo wamesema kwa kuwa wana maeneo ambayo hayajapimwa wameiomba Serikali kupitia Idara ya Ardhi kupima maeneo hayo na Idara ya Mifugo iendelee kutoa elimu ya ufugaji bora.

“Tunaushukuru sana uongozi wa Mkoa kwa kuliona hili, mimi naomba maeneo yetu yapimwe na sisi wafugaji tuelimishwe kufuga kisasa, wafugaji wengi tuna maeneo ila ng’ombe tumewapeleka mikoa mingine kwa sababu hatujui tunayatumiaje maeneo yetu, wataalam watuelimishe namna ya kuyatumia” amesema Yohana Mnyumba, Mfugaji kutoka Wilaya ya Bariadi.

Mkoa wa Simiyu ni moja ya Mikoa inayoongoza kwa kuwa na mifugo mingi hapa nchini, hali inayopelekea baadhi ya Wafugaji kuhamia maeneo mengine ili kutafuta malisho, hivyo Serikali imedhamiria kuona wafugaji Mkoani humo wanaondokana na ufugaji wa mazoea na kuingia kwenye ufugaji wa kisasa wenye tija
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu(hawapo pichani) katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mtaalam wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTEC), Mhandisi George Mulamula akiwaonesha na viongozi wa Serikali,viongozi wa dini, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu, na wadau wengine wa mifugo baadhi ramani za maeneo yaliyopimwa kwa kutumia ndege zisiondeshwa na rubani katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi.
Padre John Kasembo ambaye ni Mwezeshaji na Mshauri katika Masuala ya Uongozi,Ujasiriamali na  Maendeleo akizungumza na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wafugaji,wataalam mbalimbali na wadau wengine wa mifugo kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu, katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya viongozi wa Serikali, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi, kujadili juu ya mkakati wa ufugaji bora
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki.
Diwani wa Kata ya Budui Wilaya ya Bariadi, Mhe.Yohana Mnyumba ambaye pia ni mfugaji , akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki
Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Dkt.Titus Kamani akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki
Baadhi ya viongozi wa dini, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi, kujadili juu ya mkakati wa ufugaji bora
Diwani kutoka Wilaya ya Maswa, Mhe.Steven Dwese akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki.Wednesday, July 26, 2017

IGP SIRRO: MAKAMANDA WA POLISI MIKOA WATABAKI KWENYE VITUO VYAO UHALIFU UKIPUNGUA

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Generali Simon Sirro amesema Makamanda wa Polisi wa Mikoa wataendelea kubaki katika vituo vyao vya kazi endapo watatimiza wajibu wao na kupunguza uhalifu katika mikoa yao.

IGP Sirro ameyasema hayo wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu katika mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kamaliza mazungumzo yake na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu

IGP Sirro amesema Makamanda wa Polisi Mikoa wanapaswa kutimiza wajibu wao  katika kujali na kusimamia suala la Ulinzi na Usalama katika mikoa yao ili wananchi wakae kwa amani na mali zao ziwe salama.

“ Moja ya lengo la ziara yangu ni kuwakumbusha askari wa jeshi la polisi uwajibikaji na kuwajibika ni pamoja na kulinda watu na mali zao,  makamanda wa polisi mikoa nimewaambia kamanda ataendelea kukaa kwenye mkoa ule kama uhalifu utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa” amesema Sirro

Inspekta Sirro amesema ziara yake pia imelenga kuwakumbusha askari majukumu yao katika kuhakikisha wanawajibika kutimiza kiapo chao na kutenda haki ili wananchi waendelee kuliamini Jeshi la Polisi.

Kiongozi huyo pia ameelekeza viongozi wa jeshi la polisi wasiwanyime haki ya  dhamana watu wenye makosa ya kawaida ambayo yana  dhamana isipokuwa kwa makosa makubwa yakiwepo ya mauaji, kughushi na mengine yanayohitaji upelelezi.

Kuhusu suala la kuwepo kwa mahusiano mabaya kati ya baadhi ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Waandishi wa habari, Inspekta Sirro amefafanua kuwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa watimize wajibu wao kama watumishi wa Umma kwa kuwajali waandishi kama wanavyowajali wateja wengine kwa kufuata sheria na akawataka waandishi wa habari wafuate sheria, kanuni na taratibu pasipo kuvuka mipaka.

Akakimkaribisha Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini, katika Mkoa wa Simiyu Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka amemshukuru Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Boniventure Mshongi na Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa namna wanavyoshirikiana katika suala la ulinzi na usalama.

Aidha, amemuomba Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini kuona uwezekano wa kusaidia kujenga majengo ya Ofisi na nyumba za makazi kwa ajili ya  Askari wa Jeshi la Polisi mkoani humo.


Inspekta Simon Sirro amewasili Mkoani Simiyu akitokea Mkoani Mara akiwa katika ziara yake ya kikazi ambapo pamoja na kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu, Wakuu wa Wilaya ambao pni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya,  pia  amezungumza na viongozi na askari wa Jeshi la Polisi mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara yake ya kikazi Mkoani Simiyu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro (kulia) akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Simiyu(hawapo pichani) wakati wa ziara yake mkoani humo, (kushoto) Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kulia) akifuaahia jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro mara baada ya kumaliza mahojiano na waandishi wa habari wakati wa ziara yake mkoani Simiyu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu  mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara ya kikazi mkoani Simiyu.
Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Simiyu za Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro(hayupo pichani) katika kikao alichofanya akiwa ziarani mkoani humo.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro (kulia) na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo wakati wa ziara yake mkoani humo.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro (kulia) akizungumza na Kamati ya Ulizi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake mkoani humo,(baadhi ya wajumbe hawapo pichani).
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro (hayupo pichani) na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo wakati wa ziara yake mkoani humo.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro akisalimiana na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimaliwatu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Chele Ndaki mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji,katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt.Gamitwe Mahaza (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.
Kaimu Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Simiyu(kulia) akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ndg.Simon Maganga(kulia) akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kamaliza mazungumzo yake na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Afisa Ardhi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bibi.Grace Mgombera (kulia)akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.

Monday, July 24, 2017

RC MTAKA: SIMIYU INAHITAJI USHIRIKA IMARA, WA KISASA KUELEKEA UCHUMI WA KATI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka  amesema Mkoa huo unahitaji ushirika imara na wa kisasa unaolenga kuwafikisha wananchi katika Uchumi wa kati.

Mtaka amesema  hayo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa wa Simiyu uliofanyika katika Ukumbi wa kanisa Katoliki Mjini Bariadi, tukio ambalo limeshirikisha viongozi Serikali na watalaam mbalimbali ngazi ya Mkoa na Wilaya, viongozi wa vyama vya ushirika, Tume ya maendeleo ya Ushirika  na wadau  mbalimbali wa ushirika.

" Sisi kama mkoa tuko tayari  kwa yale ambayo  ninyi wenzetu wa Tume ya Ushirika mnadhani kupitia hayo tutakuwa na ushirika imara na utakaoendeshwa kisasa, tuko tayari hata kwa kuwatoa watu wetu kujifunza katika vyama  vya ushirika vilivyofanikiwa;ushirika wa Tanzania ukiamua Uchumi wa kati inawezekana"

Aidha, Mtaka amesema  wananchi wakielimishwa na kukubali kuungana katika vyama ushirika wanaweza kuondokana na Umaskini,  hivyo amesisitiza uwepo wa ushirika imara wenye matokeo chanya katika maeneo muhimu ya uzalishaji, ili hata mikoa mingine ijifunze Simiyu

"Mwalimu Nyerere amewahi kusema namna pekee ya watu maskini kujikomboa ni kuungana, niwasihi wanaushirika kuunganisha nguvu katika ushirika, matajiri wanaungana kuunda makampuni yanayoweza kukopa, yakashtaki na kushtakiwa ninyi unganeni kwenye vyama vya ushirika kujenga uchumi " amesema Mtaka.

Aidha, Mtaka amesema  Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) imekubali kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu kwa kuviwezesha vyama vya ushirika na  vikundi vilivyosajiliwa kisheria kwa kuwajengea uwezo wanachama na kuwapa mikopo kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali, hivyo vyama vya ushirika vinapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

Akizungumzia mchango wa ushirika katika utekelezaji wa Kauli Mbiu ya Mkoa"Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja" Mkuu huyo wa Mkoa amesema vyama vya ushirika ndivyo vyenye wazalishaji wa malighafi ya viwanda, hivyo jukwaa la ushirika litumiwe vizuri katika kuweka mikakati ya kuimarisha vyama vya ushirika na Viongozi wa Serikali wako tayari kuonesha ushirikiano.

Katika hatua nyingine Mtaka amesema mkoa unaandaa andiko linalolenga kuwakusanya wakulima na wanaushirika wote pamoja, ambapo watatumia vyumba vya madarasa katika Shule za Serikali wanafunzi watakapokuwa likizo kupewa mafunzo ya ushirika na kilimo na Wataalam wa Halmashauri, Mkoa na Chuo Kikuu cha Ushirika, ili kuimarisha ushirika na kuongeza tija katika kilimo na mifugo.

Sanjali na hilo Mtaka amesisitiza kuwa mkoa wa Simiyu ndio unaoongoza kwa kulima pamba hapa nchini, hivyo ni vema kukawa na ushirika wenye kuleta majawabu kwa changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba kuondoa kero kwa wakulima na kuongeza ubora katika uzalishaji.

Kwa Upande wake Kaimu Naibu Mrajis kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Ndg.Collins Nyakunga amemshukuru Mkuu  wa Mkoa wa Simiyu kwa kuonesha nia ya kuimarisha ushirika katika mkoa huo na kuona kuwa kupitia ushirika wananchi wanyonge wanaweza kutatua matatizo yao ya kiuchumi na Kijamii.

Nyakunga amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika itaandaa namna ambayo itautoa ushirika katika uendeshaji wa kizamani uendeshwe kisasa, tafiti zitafanyika kupitia Chuo Kikuu cha Ushirika kuona namna ya kuongeza bei, thamani ya zao la pamba na ushirika mkoani Simiyu kuimarika.

Naye Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Ndg Mathias Shineneko amesema Mkoa huo umejiwekea mkakati wa kuakikisha vyama vya ushirika vinajielekeza katika kuweka taratibu za kuongeza  na kuimarisha mitaji, hisa na akiba ili kujiimarisha kiuchumi.

Wakati huo huo Ezekiel Ganji kutoka Chama cha Msingi Sola wilayani  Maswa ameiomba Serikali kuwashirikisha wakulima wa pamba katika maamuzi ya kupanga bei badala ya kupangwa na makampuni yanayonunua pamba na kusisitiza kuwa katika ukaguzi wa vyama vya ushirika Serikali  iangalie uwezo wa vyama hivyo na kupunguza tozo za ukaguzi  kwa kuwa vyama vingi havina uwezo mzuri kifedha
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wadau wa Ushirika wa Mkoa huo(hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi, (kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akiteta jambo na Kaimu Naibu Mrajis kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Ndg.Collins Nyakunga wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la mkoa wa Simiyu, Mjini Bariadi

Baadhi ya Wadau wa Ushirika Mkoa wa Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa mara baada ya uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wadau wa Ushirika Mkoa wa Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa mara baada ya uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wadau wa Ushirika  wa mkoa huo (hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Afisa Ushirika Mkuu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Sehemu ya Uhamasishaji na utaratibu, Veneranda Mgoba akiwasilisha mada ya Usimamizi na Udhibiti Vyama vya Ushirika kwa wadau wa Ushirika wa Mkoa huo(hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.
Mwanasheria kutoka Tume ya Maendeleo ya ushirika Kitengo cha Sheria, Donald Deogratius  akiwasilisha mada ya Sheria ya Ushirika kwa wadau wa Ushirika wa Mkoa huo(hawapo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Jukwaa la Ushirika la Mkoa huo Mjini Bariadi.

Sunday, July 16, 2017

BENKI YA KILIMO KUFANYA KAZI NA MKOA WA SIMIYU

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) imeuhakikishia uongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa itafanya kazi kwa karibu katika kutoa fursa ya  mikopo itakayowasaidia wakulima mkoani humo kulima kilimo chenye tija..

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka  pamoja na Wakurugenzi na Wataalam kilimo na umwagiliaji, ushirika na mifugo kutoka Halmashauri zote za Simiyu,Kaimu Mkurugenzi wa Banki hiyo Francis Assenga amesema  wapo tayari kukopesha na kufanya kazi na Mkoa wa Simiyu kutokana na utayari wao na uwepo wa mwongozo elekezi wa shughuli za kilimo zilizofanyiwa utafiti.

Amesema Benki hiyo ambayo ina lengo la  kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania imeridhia kutoa mikopo katika miradi ya kilimo kwa wakulima, vikundi vilivyosajiliwa, vyama vya ushirika na kupitia Benki na taasisi nyingine za kifedha ambazo zinaweza kuwakopesha wakulima, ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wakulima mkoani humo.

Ameongeza kuwa ili kufanikisha azma ya Mkoa wa Simiyu ya kukifanya kilimo kuwa ni biashara na kukuza uchumi wa wakulima wake , Benki ya TADB itasaidia kutoa mikopo itakayoambatana na  mafunzo ya kuwajengea uwezo wakopaji hususani wanawake na vijana.

Ameeleza kuwa  benki yake imekwisha tenga kiasi cha shilingi milioni 650 kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo na Bil 42 za mkopo kwa wanawake na vijana, hivyo amezisisitiza Halmashauri za Mkoa wa Simiyu kuwahamasisha vikundi vya wakulima vilivyosajiliwa kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo yenye riba ndogo na masharti nafuu.

 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu uko tayari kufanya kazi na Benki ya TADB kupitia vikundi vya uzalishaji, Halmashauri na Miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani humo, ikiwa ni pamoja na miradi ya umwagiliaji ya Mwamanyili Wilayani Busega  ulio katika hatua ya upembuzi yakinifu na Mwasubuya wilayani Bariadi ambao uko katika hatua ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

“Tungehitaji kuwa Mkoa ambao kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tungetengeneza namna ambayo ingewasaidia wakulima na ikasaidia mikoa mingine kuja kuona maendeleo ya kilimo  ambayo ni matokeo ya Serikali kuwekeza katika Benki ya Kilimo” amesema Mtaka.
"Sisi kama Mkoa tumejipanga ,tumetoa Elimu ya utayari na namna ya utekelezaji wa shughuli zote kwa wataalam wetu pamoja na wananchi na isitoshe tayari tumeshafanya utafiti na kuandaa mwongozo wa uwekezaji ndani ya mkoa, hivyo tunawakaribisha kuwekeza” Amesema Mtaka

Aidha Mtaka ameongeza kuwa Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha chaki na maziwa na miradi mingine minne ya viwanda iko katika upembuzi yakinifu, hivyo benki inaweza kuwekeza katika miradi hii kwa kuwawezesha wakulima na wafugaji kuzalisha malighafi ya Viwanda hivyo au kuwa mdau katika viwanda hivyo.

 Naye Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB Augustino Matutu Chacha  amesema wamefurahishwa na utayari wa Mkoa wa Simiyu juu ya kuwawezesha wakulima na Benki hiyo iko tayari kutoa mikopo pia kwa wakulima wa zao la pamba ambao wanazalisha zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini ili izalishwe kwa wingi zaidi na katika ubora wa hali ya juu.


Chacha amesema wataalam wa kilimo wa Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na wataalam wa benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) watakutana ili kuona namna watakavyofanya kazi kwa pamoja ili mikopo itakayotolewa iweze kuwa wa manufaa kwa wakulima na nchi kwa ujumla.

 Aidha amewaeleza Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwa, Halmashauri zinaweza kupatiwa mikopo ili ziweze kuendesha miradi ya kilimo itakayoweza kuwa  vyanzo vipya vya mapato kwa Halmashauri zao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB), Francis Assenga akizungumza na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na wataalam wa Kilimo, ushirika na Mifugo (hawapo pichani) Mjini Bariadi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya uongozi wa Mkoa huo, wataalam wa kilimo, mifugo na ushirika na Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania.
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo, Augustino Matutu Chacha wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB), akizungumza na Uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na wataalam wa Kilimo, ushirika na Mifugo (hawapo pichani) Mjini Bariadi.
Mkuu wa Idara ya kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Juma Chacha akichangia katika kikao kilichofanyika katika uongozi wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wataalam wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB).
Mkuu wa Idara ya  Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Wilbert Siogopi akichangia katika kikao kilichofanyika kati ya Uongozi wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB) Mjini Bariadi.
Baadhi ya Wataalam wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB).
Baadhi ya Wataalam wakifuatilia masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiwasilishwa katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania(TADB).

Friday, July 14, 2017

VIJIJI 347 KUPATA UMEME WA REA AWAMU YA TATU MKOANI SIMIYU

Jumla ya Vijiji 347 Mkoani Simiyu vinatarajia kupata Umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya Tatu ambao utatekelezwa katika kipindi cha miezi 24 kuanzia mwezi Julai 2017.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu na utambulisho wa Mkandarasi wa mradi katika Kijiji cha Nangale, Kata ya Ndolelezi Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.

“Mradi wa REA awamu ya tatu utapeleka Umeme katika vijiji vyote vya Mkoa wa Simiyu hilo la kwanza, pili mradi huu utapeleka Umeme katika vitongoji vyote hata vijiji ambavyo vilipelekewa Umeme lakini baadhi ya vitongoji vyake bado havina, katika awamu hii navyo vinapelekewa” amesema Kalemani. 

Ameongeza kuwa Umeme wa REA awamu ya tatu pamoja na kuwanufaisha wananchi katika makazi yao kwenye vijiji vyote 347 vilivyosalia pia utapelekwa katika Taasisi za Umma zikiwepo shule, vituo vya kutolea huduma za afya, visima na mitambo ya miradi ya maji pamoja na nyumba za ibada( makanisa na misikiti).

Aidha, Dkt.Kalemani amewataka wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuutumia umeme huo kibiashara hususani katika shughuli za uzalishaji ambazo zitawaongezea kipato badala ya kuutumia kwa ajili ya kuwasha taa majumbani tu.

Ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Simyu  kwa kasi nzuri ya utekelezaji wa Sera ya Viwanda ambapo amebainisha kuwa utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya Tatu mkoani humo utasaidia kuwezesha shughuli za viwanda kufanyika vizuri hali itakayowawezesha wananchi kukuza uchumi kwa kuwa mazao yao yataongezewa thamani kupitia viwanda hivyo.

Wakati huo huo Dkt.Kalemani amesema Serikali ina mkakati wa kujenga vituo viwili vya kupozea umeme Mkoani Simiyu, ambapo kimoja kitajengwa Mjini Bariadi na kingine katika Mji wa Lalago wilayani Maswa na kuwahakikishia wananchi kuwa mkoa huo utapata umeme wa kutosha ambao utatumika pia katika viwanda.

Akimkabidhi Mkandarasi wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu ambaye ni Kampuni ya JV White City International kwa Wananchi wa Mkoa wa Simiyu, Dkt.Kalemani amemtaka  kuhakisha kuwa anatekeleza mradi  ndani ya muda uliopangwa (miezi 24), akiwatumia wakandarasi wasaidizi wenye sifa kutoka ndani ya mkoa na kuwapa ujira wao kama inavyotakiwa pamoja na  kununua vifaa vyote zikiwemo nguzo na transifoma hapa nchini.

Amemtaka Meneja wa TANESCO Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Rehema Mashinji kusimamia na kuhakikisha kuwa wakandarasi watakaowaunganishia wananchi Umeme ni wale walioidhinishwa na shirika hilo ili kuepuka Vishoka ambao watawaongezea wananchi gharama zisizo za lazima.

Amesema Serikali ina mpango wa kujenga Ofisi za TANESCO kila Wilaya na kuweka vituo vya kuhudumia wateja katika kila kata na tarafa ambapo yataanzishwa madawati ya huduma kwa wateja.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameomba Shirika la Umeme TANESCO  kuona namna ya kuweka nguvu katika Mkoa huo ili ujitosheleze kwa umeme wa uhakika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya viwanda inayoendelea kutekelezwa chini ya Kauli Mbiu ya Mkoa ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja”

Mtaka ameongeza kuwa Mkoa huo umejipanga kufanya mapinduzi kupitia teknolojia ambapo utatengeneza mpango mkakati wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT Strategy),kujenga  ICT Hub ya mkoa na vituo vya mawasiliano katika baadhi ya shule, ili wanafunzi wa madarasa ya mitihani waweze kupata unafuu wa kufundishwa kupitia teknolojia hususani kwenye masomo ya sayansi, hivyo akasisitiza umeme kupelekwa katika shule na Taasisi nyingine za Umma.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu kupitia CCM, Mhe.Leah Komanya ametoa Rai kwa TANESCO kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili wajue taratibu zote za kuunganishiwa umeme ikiwa ni pamoja kufahamu gharama ambayo ni shilingi elfu 27,000/= ili wasidanganywe na kutumia gharama kubwa kinyume na mpango wa Serikali.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mradi huo Mkazi wa Kijiji cha Nangale Bw.Mathias Mabula Mageni ameishukuru Serikali kuwafikishia umeme kupitia REA ambapo amesema utawasaidia katika kukuza uchumi kwa kuwa watautumia katika shughuli mbalimbali zitakazowaingizia kipato kama vile kuchomelea vyuma, kuanzisha mashine za kusaga na kukoboa nafaka, kuanzisha saluni za kike na za kiume pamoja na viwanda vidogo.


Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu unatekelezwa na Mkandarasi JV White City International Contractors  ambalo ni Kampuni ya Kitanzania kwa kushirikiana na Guangdong Jianneng Electronic Power Engineering Co. Ltd.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani akizindua Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilayani Itilima (kushoto) Mkuu wa mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani (mwenye suti nyeusi katikati) akikata utepe kabla ya kuzindua Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima
 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani akizungumza na wannachi wa Wilaya ya Itilima wakati wa Uzinduzi waMradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu  Mkoani Simiyu uliofanyika  katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Medard Kalemani akiwaonesha wananchi Kifaa kiitwacho UMETA(Umeme Tayari) ambacho hutumika kuleta nishati ya umeme katika nyumba ambazo haziwezi husukwa nyaya wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu  Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akitoa salamu za Mkoa wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima Mkoani humo.
 Mbunge wa Viti Maalum  Mkoa wa Simiyu kupitia CCM, Mhe.Esther Midimu akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Itilima wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Mbunge wa Itilima, Mhe.Njalu Silanga akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Itilima wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu  Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilayani Itilima.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu kupitia CCM, Mhe.Leah Komanya akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Itilima wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu  Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani( wa tatu kulia) akicheza wimbo maalum wa Kisukuma pamoja na viongozi wa mkoa wa Simiyu wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt. Medard Kalemani( wa tatu kushoto) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu(kushoto) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dkt.Titus Kamani wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani( wa pili kulia) pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Simiyu wakicheza kuelekea kuwatuza wasanii waliokuwa wakitoa burudani (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mh.Anthony Mtaka (kushoto) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Dkt.Titus Kamani akizungumza na wananchi wa Itilima wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akiteta jambo na Mbunge wa Itilima Mhe.Njalu Silanga wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofamyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima, (kushoto) ni Mbunge wa Maswa Magharibi, Mhe.Mashimba Ndaki.
Mmoja wa Wazee 10 waliopewa kifaa cha Umeme kiitwacho UMETA katika Kata ya Ndolelezi Wilayani Itilima na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani akitoa shukrani wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu uliofanyika katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Itilima wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani(hayupo pichani) wakati wa wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Kikundi cha Kwaya kutoka wilayani Itilima wakitumbuiza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani Simiyu katika Kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.
Msanii Elizabeth Maliganya (mwenye kipaza sauti katikati) akicheza wimbo wa Kisukuma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.Dkt.Medard Kalemani(kushoto) pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu kufurahia uzinduzi wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA)Awamu ya Tatu Mkoani humo katika kijiji cha Nangale wilaya ya Itilima.


Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!