Friday, July 28, 2017

SIMIYU YAJIPANGA KIMKAKATI KUWASAIDIA WAFUGAJI KUFUGA KISASA

Serikali Mkoani Simiyu imejipanga  kuweka mkakati maalum utakaowasaidia wafugaji mkoani humo kutoka kwenye ufugaji wa kuhama hama na kufanya ufugaji wa kisasa wenye tija.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika kikao maalum cha viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wafugaji, wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya mkoa  kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini Bariadi.

Mtaka amesema Mkoa wake umedhamiria kuwatambua wafugaji na maeneo yao na kutoa elimu juu ya upimaji wa maeneo hayo ili yatumiwe kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhama hama kufuata maji na malisho katika mikoa mingine.

“Hatuwezi kuwa Serikali ambayo ina majibu mepesi kwenye mambo ya msingi, lazima tupate majawabu ya wafugaji ndani ya mkoa wetu, tufike mahali ambapo mfugaji kutoka mkoa wa Simiyu hatapigwa faini kwenye mikoa mingine kwa sababu ya kutafuta maji na malisho”amesema Mtaka.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali kupitia Wataalam wa Kilimo na Mifugo watatoa elimu kwa Wafugaji watakaorasimisha maeneo yao, ili wayatumie kupata malisho ya mifugo na kuweka miundombinu muhimu ya mifugo kama vile malambo, majosho na visima katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji na malisho ya mifugo.

Ameongeza kuwa, Mkoa unaandaa utaratibu ambapo shule za Serikali zitakapokuwa zinafungwa, Idara ya Kilimo na Mifugo itatumia madarasa hayo kutoa elimu ya ufugaji na kilimo bora kwa wananchi.

Sanjali na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema zoezi la kupima maeneo ya wafugaji na kuweka miundombinu muhimu ya mifugo litakapokamilika Serikali imepanga kuweka mizani katika minada yote mkoani humo ili wafugaji wasidanganywe na kuibiwa wanapouza mifugo yao.

Kwa upande wake Padre John Kasembo ambaye ni Mwezeshaji na Mshauri katika Masuala ya Uongozi, Ujasiriamali na  Maendeleo ametoa wito kwa Wafugaji wa Mkoa wa Simiyu kukubali kufanya ufugaji wenye tija na waungane na Viongozi katika mipango inayoandaliwa kwa ajili ya kufikia ufugaji bora kwa manufaa yao.

Padre Kasembo amesema ili wafugaji wafuge kisasa wanapaswa kuwa na maeneo, miundombinu ya kisasa, malisho na kufuata sheria na taratibu, hivyo akawaasa wakubali kubadilika katika namna ya kufikiri, kutenda, kuweka vipaumbele na kushughulikia changamoto ili wapate matokeo chanya.

Daktari wa Mifugo wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Gamitwe Mahaza amesema Wafugaji wengi pia ni Wakulima, hivyo ni vema wakatumia masalia ya mazao kwa ajili ya malisho badala ya kuyaacha mashambani yakaharibika; akasisitiza juu ya urasimishaji wa maeneo yao ili miundombinu kama visima iwekwe kusaidia ukuaji wa malisho ya asili na upandaji wa malisho ya kisasa.

Naye Mtaalam wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC), Mhandisi George Mulamula ameeleza kuwa upimaji katika maeneo ya wafugaji unaweza kufanyika kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo zinazotumia mifumo ya TEHAMA , kama vile matumizi ya satelite na ndege zisizotumia rubani (drones) ambazo zitasaidia zoezi hilo kufanyika kwa  usahihi mkubwa na haraka.

Pia Mhandisi Mulamula amesema kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wafugaji wataweza kupata mafunzo na taarifa mbalimbali za mifugo kupitia simu zao za mikononi, kujua bei na soko la mifugo na kutambua mifugo yao hivyo kupunguza wizi wa mifugo.

Viongozi wa Wafugaji na Wafugaji kwa pamoja wameshukuru Uongozi wa Mkoa kuona umuhimu wa kushughulikia changamoto zao ambapo wamesema kwa kuwa wana maeneo ambayo hayajapimwa wameiomba Serikali kupitia Idara ya Ardhi kupima maeneo hayo na Idara ya Mifugo iendelee kutoa elimu ya ufugaji bora.

“Tunaushukuru sana uongozi wa Mkoa kwa kuliona hili, mimi naomba maeneo yetu yapimwe na sisi wafugaji tuelimishwe kufuga kisasa, wafugaji wengi tuna maeneo ila ng’ombe tumewapeleka mikoa mingine kwa sababu hatujui tunayatumiaje maeneo yetu, wataalam watuelimishe namna ya kuyatumia” amesema Yohana Mnyumba, Mfugaji kutoka Wilaya ya Bariadi.

Mkoa wa Simiyu ni moja ya Mikoa inayoongoza kwa kuwa na mifugo mingi hapa nchini, hali inayopelekea baadhi ya Wafugaji kuhamia maeneo mengine ili kutafuta malisho, hivyo Serikali imedhamiria kuona wafugaji Mkoani humo wanaondokana na ufugaji wa mazoea na kuingia kwenye ufugaji wa kisasa wenye tija
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu(hawapo pichani) katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi.
Mtaalam wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTEC), Mhandisi George Mulamula akiwaonesha na viongozi wa Serikali,viongozi wa dini, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu, na wadau wengine wa mifugo baadhi ramani za maeneo yaliyopimwa kwa kutumia ndege zisiondeshwa na rubani katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi.
Padre John Kasembo ambaye ni Mwezeshaji na Mshauri katika Masuala ya Uongozi,Ujasiriamali na  Maendeleo akizungumza na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, wafugaji,wataalam mbalimbali na wadau wengine wa mifugo kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu, katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi.
Baadhi ya viongozi wa Serikali, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi, kujadili juu ya mkakati wa ufugaji bora
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki.
Diwani wa Kata ya Budui Wilaya ya Bariadi, Mhe.Yohana Mnyumba ambaye pia ni mfugaji , akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki
Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Dkt.Titus Kamani akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki
Baadhi ya viongozi wa dini, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani na nje ya Simiyu wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika kikao maalum kilichofanyika Mjini Bariadi, kujadili juu ya mkakati wa ufugaji bora
Diwani kutoka Wilaya ya Maswa, Mhe.Steven Dwese akichangia jambo katika kikao maalum cha kujadili mkakati wa ufugaji bora Mkoani Simiyu, kilichofanyika Mjini Bariadi katika Ukumbi wa kanisa Katoliki.



0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!