Sunday, July 30, 2017

SIMIYU YAJIPANGA KUTENGENEZA AJIRA KUPITIA SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO

Mkoa wa Simiyu umejipanga kurasimisha kazi za sanaa, utamaduni na baadhi ya michezo ili kutengeneza ajira kwa wananchi  ambazo zitasaidia kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu Tamasha la “Simiyu Jambo Festival” litakalohusisha mashindano ya mbio za baiskeli na ngoma za asili ambalo litafanyika Agosti 06, 2017 Mjini Bariadi.

Amesema Mkoa wake umekusudia kuandaa utaratibu wa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuona namna ambayo kazi za sanaa,utamaduni na michezo zinazofanyika katika mkoa wa Simiyu zinaweza kufanywa kibiashara na zikawanufaisha wananchi.

Ameongeza kuwa vikundi vya sanaa na utamaduni vya Mkoa wa Simiyu vitapewa mafunzo ya namna ya kufanya kazi zao kitaalam katika viwango vinavyotakiwa, ili kazi ziweze kuuzika ndani na nje ya mkoa hususani kipindi ambacho watalii wengi wanakuja hapa nchini kwa kuwa mkoa huo unapakana na mikoa yenye hoteli nyingi za kitalii.

“Simiyu ni mkoa unaopakana na mikoa yenye Hoteli za kitalii, tungehitaji tufike mahali ambapo kazi za utamaduni na sanaa ndani ya mkoa wetu zinafanywa kibiashara;wakati watalii wanapotembelea hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwenda kwenye  hoteli za kitalii wasiishie kupiga picha, tungehitahi vikundi vyetu vya sanaa na utamaduni viuze kazi zao huko” amesema Mtaka

.Aidha, Mtaka amefafanua kuwa katika kufanikisha hayo Mkoa umeanza na mchezo wa  Mbio za baiskeli kupitia Mashindano yatakayofanyika Agosti 06, mwaka huu ambapo Mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Tulia Ackson.

 Amesema vijana wengi wa Mkoa huo wanafanya vizuri katika mchezo huo hivyo watafanyiwa utaratibu wa kupewa mafunzo ya kuwaimarisha zaidi katika mchezo huo, ili Mkoa ufikie hatua ya kutoa wawakilishi katika nchi kwenye mashindano makubwa ya mbio za baiskeli kama ya Jumuiya ya Madola na Olimpiki.

“Tuko kwenye kutambua vipaji vya watu na tunajaribu kuona kila mwananchi aliyeko ndani ya mkoa wa Simiyu kile ambacho amejaliwa na Mwenyezi Mungu kinamsaidia kujipatia kipato chake.Tunafanya yote haya kwenye Mkoa kwa kuwa tunaamini Kipaji cha mtu ni biashara na kipaji ni ajira” amesema Mtaka.


 Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama cha baiskeli Mkoa wa Simiyu Joseph Paul amesema kuwa chama chake kinaiwashukuru kampuni ya Jambo Food Product kwa kudhamini mashindano hayo ya Mbio za baiskeli ambayo yatahusisha makundi matatu; kilometa 200 kwa wanaume, Kilometa 80 wanawake na Kilometa Tano kwa watu wenye Ulemavu.


Paul amesisitiza kuwa chama chake kimejipanga vilivyo na zaidi ya washiriki  150 wamethibitisha kushiriki mashindano hayo kutoka katika mikoa ya Simiyu,Geita,Mwanza, Shinyanga na Arusha


Naye Meneja wa Masoko wa Kampuni ya Jambo Food  Product Anthony Paul,amesema Kampuni hiyo ambayo ni wadhamini wakuu wa Mashindano hayo wamejipanga kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo Pikipiki itakayotolewa kwa mshindi wa Kwanza (wanaume) na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 8 zitashindaniwa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka akiiendesha pikipiki itakayotolewa na Kampuni ya Jambo Food  Product kama zawadi ya mshindi wa kwanza wanaume katika Mashindano ya baiskeli yatakayofanyika Agosti 06 mwaka huu Mjini Bariadi, wengine ni baadhi ya washiriki wa mashindano hayo


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kushoto)akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)ofisini kwake kuhusu Simiyu Jambo Festival itakayohusisha mashindano ya Mbio za Baiskeli na burudani ya ngoma za asili yatakayofanyika Agosti 06 mwaka huu mjini Bariadi, (kushoto ) Mwenyekiti wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Joseph Paul.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Jambo Food  Product Anthony Paul (wa pili kushoto)akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu zawadi zitakazotolewa na kamunu hiyo kwa washindi wa mashindano ya baiskeli yatakayofanyika Agosti 06, 2017 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka (mwenye pikipiki) akiwa katika picha ya pamoja na baadh ya washiriki wa mashindano ya mbio za Baiskeli kutoka mkoani humo ambayo yatafanyika Agosti 06, 2017 Mjini Bariadi.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na wadau wa michezo wakimsikiliza mkuu wa Mkoa wa Simiyu akizungumza na waandishi wa Habari juu ya “Simiyu Jambo Festival” tamasha litakalohusisha Mashindano ya Baiskeli na burudani ya wagika , wagalu na ngoma za asili Agosti 06, 2017.
Manju wa Kundi la Wagika, Sadam Chulichuli(katikati) akiwaeleza waandishi wa habari juu ya ushiriki wao katika Tamasha la “Simiyu Jambo Festival” litakalohusisha mashindano ya Baiskeli na Burudani kutoka kwa wagika, wagalu na ngoma nyingine za asili.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa pili kushoto)akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)ofisini kwake kuhusu Simiyu Jambo Festival itakayohusisha mashindano ya Mbio za Baiskeli na burudani ya ngoma za asili yatakayofanyika Agosti 06 mwaka huu mjini Bariadi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka mwenye kipeperushi(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Baiskeli, Viongozi wa Wagika na Wagalu  na baadhi ya wadau wa michezo na utamaduni mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya Mashindano ya baiskeli yatakayofanyika Agosti 06, 2017.


0 comments:

Post a Comment

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!