Saturday, June 24, 2017

NSSF YAKABIDHI HUNDI YA SHILINGI BILIONI 1.5 UPANUZI WA KIWANDA CHA CHAKI SIMIYU


Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umekabidhi hundi ya shilingi bilioni 1.5 kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu,  fedha ambazo ni  mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha Chaki Wilayani humo na kuongeza uzalishaji.
Hundi hiyo imekabidhiwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof.Godius Kahyarara wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof.Godius Kahyarara amepongeza Mkoa wa Simiyu kwa kutekeleza Sera ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kwa vitendo  na kuwataka viongozi wa mkoa huo kutokatishwa tamaa.
Amesema NSSF kama Shirika la Umma linatekeleza sera na maelekezo ya Serikali na wametoa mkopo huo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ili wafanye upanuzi wa kiwanda cha chaki na kuongeza uzalshaji kwa kuwa suala la Viwanda ni la kipaumbele.
Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na  watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amesema kiwanda cha Chaki Maswa kimebeba ujumbe na dhana ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli ya kushikamanisha Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya watu kwa sababu kinatumia malighafi ya hapa nchini.
Aidha, amesema kiwanda hiki kitawanufaisha Watanzania hususani vijana wa Mkoa wa Simiyu ambao watafanya kazi moja moja katika kiwanda na wale wataohusika katika uchimbaji wa malighafi ambayo inapatikana maeneo mengine  hapa nchini.
Asilimia 56 ya nguvukazi hapa Tanzania ni vijana na vijana wengi bado hawana ajira lakini kiwanda hiki kitasaidia, kwa kuwa sehemu ya hiyo asilimia 56 wataajiriwa katika kiwanda na wengine watapata ajira huko mkoani Singida ambako malighafi ya kutengenezea chaki inapatikana” amesema.
Mhe.Mhagama ameongeza kuwa kiwanda kitatatua tatizo la upatikanaji wa chaki hapa nchini,kitaokoa fedha kwa kuwa chaki zitauzwa kwa bei nafuu na kitaongeza mapato ya fedha za kigeni kwa kuwa chaki zitakazozalishwa zitauzwa katika soko la nje ya nchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amesema Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imeonesha mfano katika kutekeleza agizo la Rais wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli la kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa kujenga kiwanda hicho kikubwa, ambapo amesema kufikia mwaka 2020 Halmashauri za Mkoa wa Simiyu zitakuwa mfano kwa kuwa na miradi yake zenyewe .
     “Kama Halmashauri zinakopa mabilioni kujenga stendi, masoko kwa nini zisikope kujenga viwanda, zikatumia malighafi ya hapa nchini  zikaajiri Watanzania wakapata kipato na nchi yetu ikanufaika; Halmashauri za Mkoa wa Simiyu zitaajiri na kwenye miaka mitano ya Mhe.Rais tutatoa mfano wa kuwa Halmashauri zenye miradi yake” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Mhe.Riziki Pembe Juma amesema Zanzibar ni wadau wakubwa wa Chaki zinazotengenezwa Maswa(Maswa Chalks), hivyo ameomba ushirikiano ulioanzishwa kati ya Zanzibar na Simiyu udumu ili kufikia malengo katika kukuza kiwango cha elimu na utekelezaji wa Sera ya Viwanda.

Kiwanda cha kutengeneza chaki Wilayani Maswa kwa sasa kinazalisha katoni zaidi ya 180 kwa siku na chaki hizo zinatumika katika shule zilizopo katika maeneo tofauti hapa nchini,  ikiwa ni pamoja na mikoa yote za Zanzibar na baadhi ya mikoa ya Tanzania bara ikiwemo Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita na Tabora.
Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama(kulia) akimkabidhi hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt.Fredrick Sagamiko.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof.Godius Kahyarara(kushoto) akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa, (kulia) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu(wa tatu kushoto), viongozi wa Wilaya ya Maswa wakimkabidhi Meneja wa Benki ya Azania( wa pili kulia) Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki wilayani humo ili aendelee na taratibu za kibenki.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kahyarara(kulia)  wakiteta jambo wakati wa hafya ya makabidhiano ya hundi  ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Wilayani Maswa.
Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu, Mhe.Jenista Mhagama(wa tatu kulia), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi (wa pili kulia) katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa, wilaya ya Maswa na Vijana wa Maswa Family wanaofanya kazi katika kiwanda cha chaki.
Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akipokea taarifa ya Upembuzi yakinifu wa panuzi wa kiwanda cha chaki cha Maswa kutoka kwa mtalaam wa Taasisi ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii(ESRF), Deodatus Sagamiko.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Mhe.Riziki Pembe Juma akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa hafla ya makabidhiano ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.
Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama( wa pili kushoto) akiangalia kikundi cha ngoma mara mara baada ya kuwasilisi wilayani Maswa, kwa ajili ya makabidhiano ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.
Msanii Elizabeth Maliganya (kulia) na baadhi ya waimbaji wa Kwaya ya Kanisa la AICT Bariadi (wenye sare za vitenge) wakicheza na viongozi mbalimbali mara baada ya makabidhiano ya hundi  ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama(wa tano kulia), Waziri wa Elimu Zanzibar (mwenye ushungi mwekundu), mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa sita kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Maswa na wadau wengine wa maendeleo baada ya makabidhiaono ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama katika picha ya pamoja na viongoziwa mkoa na wakuu wa idara wa Halmasahuri ya Wilaya ya Maswa baada ya makabidhiaono ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.
Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Mbunge wa Maswa Mashariki, mhe.Stanslaus Nyongo mara baada ya kuwasili wilayani Maswa, kwa ajili ya makabidhiano ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akitoa salamau za mkoa wakati wa hafla ya makabidhiano ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 iliyotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.
Baadhi ya viongozi katika Mkoa wa Simiyu wakifuatilia masuala mbalimbali katika hafla ya makabidhiano ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.

Baadhi ya viongozi katika Mkoa wa Simiyu wakifuatilia masuala mbalimbali katika hafla ya makabidhiano ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.
Waziri wa Nchi Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kahyarara(mara baada ya kuwasili wilayani Maswa, kwa ajili ya makabidhiano ya Hundi ya shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na NSSF kama mkopo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha chaki Maswa.


TAARIFA YA RUFAA YA VYETI FEKI KUTOLEWA JUNI 30

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro   amesema taarifa ya rufaa ya watumishi waliobainika kuwa na vyeti feki itatolewa Juni 30, mwaka huu.

Dkt Ndumbaro ameyasema hayo leo wakati alipozungumza na viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya, ambao ni wasimamizi wa Watumishi wa Umma Mkoani Simiyu katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi nchini.

Amesema katika zoezi la uhakiki la awamu ya kwanza Watumishi zaidi ya 9000 walibainika kuwa na vyeti feki ambapo kati yao ni asilimia kumi tu (10%) ndiyo waliokata rufaa.

“ Taarifa itawasilishwa tarehe 30 mwezi huu na baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya rufaa hizo  maelekezo yatatolewa namna ya kuhitimisha ajira za watu wenye vyeti feki” amesema

Aidha , amesema baada ya taarifa ya rufaa kuwasilishwa Serikali itatangaza vibali vya nafasi za ajira kwa watumishi watakaojaza nafasi zitakazoachwa wazi na zile zilizotengwa.

Wakati huo huo Katibu Mkuu huyo amewataka viongozi wasisite kuwachukulia hatua watumishi wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma na kuwapongeza wanaofanya kazi kwa bidii ili kuwapa motisha.

“Kusiwe na masuala ya kuhamisha watumishi wanaosumbua, kama mtu anasumbua malizana naye pale pale fuata taratibu mfungulie mashtaka,  ili tujenge utumishi wa Umma wenye uadilifu na weledi, lakini pia wale wanaofanya kazi vizuri wapongezeni mkiwaacha mtawakatisha tamaa” alisema.

Kuhusu suala la Watumishi kupandishwa vyeo Dkt.Ndumbaro amesema lifanyike kama motisha kwa watumishi wanaofanya kazi vizuri kwa kuzingatia ufanisi katika utendaji wa kazi,bajeti, masharti mengine ya upandaji vyeo kwa watumishi likiwepo la kufanya kazi kazi kwa muda usiopungua miaka mitatu katika cheo kimoja.

Katika hatua nyingine Dkt. Ndumbaro amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuwasimamia Maafisa Utumishi wanaosimamia mfumo wa mshahara wa LAWSON kuhakikisha wanaunganisha taarifa za mfumo huo na takwimu za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA kwa ufasaha na kuwakumbusha watumishi kuangalia taarifa zao ili wazihakiki ikiwa ziko sahihi na halali.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Watumishi wa Umma mkoani Simiyu, Katibu Tawala Mkoa ameahidi kutekeleza na  kuhakikisha watendaji wengine wanatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu ili Utumishi wa Umma ufanyike katika maadili, ufanisi na weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg.Mariano Mwanyigu ameshauri Serikali iangalie kwa upya umri wa kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, kwa mujibu wa sheria miaka 60 na kuona uwezekano wa kupunguza miaka ili kutoa nafasi kwa vijana wengi walio nje ya mfumo kupata ajira.

Kikao hicho ambacho pia kimetumika kutoa taarifa, maagizo na maelekezo mbalimbali kimewashirikisha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri na Maafisa Utumishi wanaoshughulikia Mfumo wa mshahara wa  LAWSON.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro  akizungumza na baadhi ya Watumishi wa Mkoa wa Simiyu mjini Bariadi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumisi nchini.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini akizungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro  aweze kuzungumza na baadhi ya watumishi wa Umma(viongozi) mkoani humo.
Baadhi ya viongozi na watumishi wa Umma ngazi ya Wilaya na Mkoa wakisikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro katika kikao kilichofanyika Mjini Bariadi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa umma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Ndg.Mariano Mwanyigu akitoa maoni wakati wa kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Watumishi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa umma.
Mkuu wa Idara ya Utawala ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Diocle Rutema akitoa maoni wakati wa kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Watumishi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani Halmashauri ya Wilaya ya Itilima akitoa maoni yake wakati wa kikao kilichofanyika Mjini Bariadi kati ya Watumishi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti ya Mkoa, Wakurugenzi na Makatibu Tawala Wilaya mara baada ya kufanya kikao na watumishi mjini Bariadi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Meatu na Itilima mara baada ya kufanya kikao na watumishi mjini Bariadi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Busega na Mji wa Bariadi mara baada ya kufanya kikao na watumishi mjini Bariadi.

Wednesday, June 14, 2017

BARAZA LA UWEZESHAJI LATOA TUZO KWA MKOA WA SIMIYU KWA KUTEKELEZA SERA YA VIWANDA

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limetambua mchango wa Mkoa wa Simiyu katika  Utekelezaji wa Sera ya Viwanda na kutoa Tuzo ya kikombe na Cheti.

Tuzo hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji lililofanyika Mjini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka amesema Tuzo hizi ni  hamasa kwa Viongozi na wananchi wa Simiyu kuongeza jitihada zaidi katika Utekelezaji wa Sera ya Viwanda kuelekea kwenye Uchumi wa Kati.

Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “WILAYA MOJA BIDHAA MOJA” ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha kutengeneza Chaki kilichopo wilayani Maswa na Kiwanda cha kusindika Maziwa wilayani Meatu, ambapo upembuzi yakinifu unaendelea kwa ajili ya upanuzi wa viwanda hivi ili kuongeza uzalishaji.

Aidha, upembuzi yakinifu utafanyika katika Halmashauri nyingine kwa ajili ya kuanzisha viwanda mbalimbali kikiwemo kiwanda cha sabuni za maji, za unga na mche wilayani Itilima, Kiwanda cha kutengeneza Tomato Sauce na Chill Sauce Wilaya ya Busega na kiwanda cha kusaga nafaka  na kupaki unga Bariadi Mjini.

Vingine ni kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kitakacojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Kiwanda cha kutengeneza vifungashio kitakachojengwa Wilayani Maswa.


Pamoja na viwanda hivyo, Serikali imekusudia kujenga Kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba,  ambacho kitasaidia Taifa kuokoa fedha zilizokuwa zikitumika kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kulia) na Katibu Tawala Mkoa,Ndg.Jumanne Sagini(kushoto) wakiwa na tuzo za Kikombe na cheti ambazo zimetolewa kwa Mkoa wa Simiyu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji kutambua utekelezaji wa Sera ya Viwanda kwa mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) akikabidhiwa Tuzo ya Kikombe kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ambayo ilitolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji kutambua utekelezaji wa Sera ya Viwanda kwa mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(aliyeshika kikombe) katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama(wa tatu kulia) na baadhi ya Viongozi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Thursday, June 8, 2017

LIFE MINISTRY YATOA MSAADA WA VIFAA TIBA HOSPITALI TEULE YA MKOA SIMIYU

Shirika la Kidini la Madhebu ya Kikristo la Life Ministry limetoa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 40 kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Mjini Bariadi.

Akipokea vifaa tiba  hivyo Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.  Anthony  Mtaka ameishukuru Life Ministry kwa msaada huo na kuwahakikishia kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi katika hospitali hiyo.

Aidha, amesema Serikali iko tayari kushirikiana na madhehebu ya dini katika  kuhakikisha kuwa afya za wananchi zinakuwa salama, hivyo akawahakikishia kuwa  milango iko wazi kwa taasisi nyingine za dini zinazotaka kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya.

Mtaka ameongeza kuwa ili Madaktari na wauguzi waweze kutekeleza majukumu yao vizuri ni lazima wawezeshwe vifaa, hivyo msaada huo utawatia moyo na kuongeza ari ya kufanya kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Life Ministry hapa nchini, Dismas Shekalaghe amesema vifaa hivyo vimetolewa kama sehemu ya kuisaidia jamii ambavyo vitawawezesha madaktari na wauguzi kuwahudumia wananchi.

Shekalaghe ameongeza kuwa wao wanaamini kuwa ili mtu aweze kumtumikia Mungu  ni lazima awe na afya njema, hivyo kupitia msaada huo wa vifaa wagonjwa watahudumiwa na kurudi katika hali zao kawaida na kuendelea kumtumikia Mungu na kufanya shughuli za maendeleo.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Dkt.Fredrick Mlekwa akitoa shukrani kwa Life Ministry amesema, msaada huo umefika katika wakati muafaka ambapo amesisitiza kuwa uongozi wa Hospitali umefarijika kupata vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Tumefarijika sana kupata msaada huu na walengwa ambao ni wananchi watapata huduma bora  kupitia vifaa hivi, naomba nitoe wito kwa Mashirika mengine  ya madhehebu ya dini  kuendelea kutusaidia kwa kuwa Hospitali hii inawahudumia watu wenye mahitaji mbalimbali” alisema Dkt.Mlekwa.

Baadhi ya Vifaa vilivyotolewa na Life Minisry ni pamoja na viti vya kubebea wagonjwa(wheel chairs), vifaa vya viungo bandia, vifaa vya huduma za meno, vifaa vya vinavyotumika katika upasuaji, bandeji na mabomba ya sindano.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.  Anthony  Mtaka(katikati), Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Mkoa, Dkt. Fredrick Mlekwa(kushoto) wakipokea baadhi ya vifaa vilivyotolewa  Life Ministry kutoka kwa Mkurugenzi wa Shirika hilo la dini, Bw. Dismas Shekalaghe(Kulia)

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.  Anthony  Mtaka(katikati), Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Mkoa, Dkt. Fredrick Mlekwa(kushoto) wakikabidhiwa viti vya kubebea wagonjwa na Mkurugenzi wa Life Ministry Bw. Dismas Shekalaghe (kulia).  ambavyo ni miongoni mwa vifaa vilivyotolewa  Shirika hilo la Kikristo kwa Hospitali Teule  ya Mkoa wa Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.  Anthony  Mtaka akizungumza na wachungaji wa madhehebu ya Kikristo wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na Shirika la Kikristo la Life Ministry kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, mjini Bariadi

Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule  ya  Mkoa wa Simiyu, Dkt.Fredrick Mlekwa akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na Shirika la Kikristo la Life Ministry kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, mjini Bariadi.
Mkurugenzi wa Life Ministry hapa nchini, Dismas Shekalaghe(wa pili kulia) wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na Shirika hilo la Kikristo kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, mjini Bariadi.
Baadhi ya Viti vya kubebea wagonjwa(wheel chairs) vilivyotolewa na Shirika la Madhehebu ya Kikristo la Life Ministry kwa Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, mjini Bariadi.

Kumbukumbu za Blogu

Powered by Blogger.
Subscribe Via Email

Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)

Your email address is safe with us!