Na Stella Kalinga
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein
amesema Serikali imejipanga kukusanya na kutumia Mapato na rasiliamali zake kwa maendeleo ya wananchi ili kupunguza na hatimaye
kuondokana na kupewa misaada ya wahisani.
Rais
Shein amesema hayo leo wakati alipowahutubia na wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Taifa kwa
ujumla kwenye maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, mwl. Julius
K. Nyerere na Wiki ya vijana, yaliyofanyika kitaifa Mkoani Simiyu.
Rais
Shein amesema Serikali haiko tayari kukubali misaada ya baadhi ya wahisani ambao
wamekuwa wakitoa na kuambatanisha na masharti yasiyotekelezeka ambayo yapo wa ajili ya kuharibu mipango ya maendeleo.
Aidha,
Rais Shein amesema ili kufikia azma hiyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimejidhatiti kuimarisha
uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kubana mianya yote ya rushwa na upotevu wa
mapato na fedha zitakazookolewa zitaelekezwa katika shughuli za kiuchumi na
huduma za jamii.
Sanjali
na hilo Mhe. Dkt. Shein ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia
uchumi wa nchi na kupambana na watu wenye tamaa na lengo la kuhujumu uchumi.
Dkt.
Shein amesema juhudi hizo za Serikali zina nia ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi
na kijamii ambapo alizitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) na Bodi ya Mapato
Zanzibar kuwajibika ipasavyo katika ukusanyaji wa mapato.
“Tumeanza
kuwawajibisha watumishi wasio waadilifu wapo waliotangazwa na ambao
hawajatangazwa, bado tunaendelea kuwachunguza wengine “alisema Rais Shein.
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye ulemavu
, Mhe. Jenista Mhagama amesema Mwenge wa
uhuru mwaka 2016 umebaini ubadhilifu na udanganyifu katika miradi ya maendeleo katika
Halmashauri saba nchini, hivyo akaelekeza hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria
kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma zichukuliwe kwa watakaobainika kuwa
chanzo cha ubadhilifu huo.
Katika
kutekeleza Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, mwaka 2016, “Vijana ni nguvu
kazi ya Taifa; Washirikishwe na kuwezeshwa” Mhe.Mhagama amesema mikoa ya Simiyu,
Njombe,Mwanza, Ruvuma, Mbeya na Mtwara imetekeleza agizo la Serikali la
kuhakikisha vijana wote nchini wanawezeshwa kwa kuwapa mitaji na kuwajengea
uwezo wa kuendesha miradi mbalimbali.
Akitoa
salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa wake umedhamiria
kuwawezesha vijana kujiairi kwa kutumia fursa zilizopo ikiwemo kuanzisha
viwanda vidogo vidogo kwa kila wilaya chini ya Kauli Mbiu “Wilaya moja bidhaa
moja”, ambapo hadi sasa Wilaya ya Maswa ina kiwanda cha kuzalisha chaki na
Meatu kiwanda cha kusindika maziwa.
Maadhimisho
ya Kilele cha Mbio za Mbio za Mwenge wa
Uhuru na Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa mwaka 2016 yalitanguliwa na Ibada
ya Kumuombea Hayati Baba wa Taifa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Yohana Mjini Bariadi, ambapo Askofu wa Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu amewaasa Watanzania kumuenzi
Baba wa Taifa kwa kupinga rushwa, ubaguzi
na kudumisha amani na utulivu nchini.
Jumla
ya Miradi 1,342 yenye thamani ya
shilingi bilioni 498.8 imewekewa mawe ya Msingi
na mingine kuzinduliwa na Mwenge wa uhuru mwaka 2016 na kuanza kutoa
huduma kwa wananchi, Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2017 zitazinduliwa katika
Mkoa wa Katavi na kuhitimishwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi