Mkoa wa Simiyu umeweka historia ya Mchezo wa Mpira wa Miguu baina ya
wachungaji na waganga wa jadi ikiwa ni makubaliano ya kutoa ujumbe wa kupinga
mauaji ya watu wenye Ualbino na vikongwe kwa kupiga maarufuku Ramli Chonganishi
ambazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa mauaji hayo.
Mchezo huo kati ya wachungaji na waganga wa jadi umefanyika siku moja kabla ya kufanyika burudani kubwa ya
utamaduni wa asili almaarufu Mbina ambayo hufanyika kila mwaka Mei 31,baada ya
wakulima kumaliza msimu wa kilimo .
Pande zote mbili kwa pamoja zilikubaliana
kuwa utaratibu wa kufanya vikao na
michezo utakuwa endelevu na utafanyika kila mwaka kwa kuzunguka katika wilaya
zote ili kuhakikisha mauji ya watu wenye ualbino na vikongwe yanakomeshwa
kabisa.
Askofu
wa K.K.K.T Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt.Emmanuel Makala amesema
Kanisa liko tayari kukemea kwa wazi mauaji ya watu wenye ualbino na linaunga
mkono juhudi za Serikali za kulinda amani na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Naye Mtemi Charles Balele Doto ambaye ni Katibu wa Umoja wa Watemi Kabila
la Wasukuma amesema waganga wa jadi kazi yao ni kutoa huduma za tiba asili kwa
watu na siyo kufanya ramli chonganishi zinazopelekea mauji ya watu wenye
ualbino, akawataka wanaofanya hivyo waache mara moja kwa kuwa ni wababaishaji
na wanadhallisha ya huduma ya tiba asili.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kukamilika,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Mhe.Anthony Mtaka amewapongeza kwa uamuzi huo ambao unatoa Taswira mpya kwa
mkoa wa Simiyu wa kuondokana na dhana iliyokuwepo ya mauaji na kuwa
mkoa wa kimaendeleo na kuagiza michezo mbalimbali kufanyika kila mwezi ili
kuendeleza vipaji vya mbalimbali vya wanamichezo.
Aidha, amesema Mkoa huo una agenda ya “Wilaya Moja, Bidhaa Moja, Kiwanda
Kimoja ama ununue au ukodishe Simiyu, Watanzania Tupende vya kwetu”hivyo
akawataka wananchi kuchangamkia fursa hizo kwa maendeleo yao na kuachana na
imani potofu kuwa Viungo vya Mtu mwenye ualbino vitawapa utajiri.
“Simiyu tunajenga viwanda utajiri wako wewe usiue albino utajiri wako lima
pamba uuze kwenye kiwanda cha nguo, jiandae kuwa wakala, soma vizuri uwe
mfanyakazi, jiandae kuzalisha malighafi ya Viwanda vya Rais wetu Mhe.Dkt. John
Pombe Magufuli” alisema.
“Tarehe 09 Mwezi Juni tunapokea hundi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya
ujenzi wa kiwanda cha chaki Maswa, Tarehe 12 Juni tunaanza upembuzi yakinifu wa
viwanda vyetu viwili; upanuzi wa kiwanda cha maziwa Meatu na kiwanda cha
kusindika nyanya na pilipili ili tutengeneze tomato sauce na chili sauce.
Bariadi tutajenga kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba, Itilima
tutajenga kiwanda cha kutengeneza sabuni zote hizi ni fursa” alisema
Mtaka ameongeza kuwa wazazi wote walio na watoto wenye ulemavu wa aina
yoyote wasiwafiche wawatoe kwa Serikali imewatengenezea mazingira mazuri ikiwa
ni pamoja na kulinda haki zao.
Wakati huo huo amewataka wananchi kuvitumia vituo vya kutolea huduma za
Afya kwanza kila wanapohitaji matibabu badala ya kukimbilia kwa Waganga wa jadi
hali inayopelekea wengi wao kuchelewa kupata
huduma wanapoteza maisha na kuingia katika ramli chonganishi kwa kuamini
kuwa wamerogwa.
Katika Mtanange huo uliofanyika katika uwanja wa Halmashauri ya Mji Bariadi Waganga
wa kienyeji walikubali kichapo cha Magoli mawili kwa nunge(sifuri) kutoka kwa watumishi
wa Mungu(Wachungaji).