MKUU wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro,
amewaonya baadhi ya watu wanaohamasishana kupitia mitandao mbalimbali ya
kijamii kuhusu kufanya maandamano bila kufuata utaratibu uliopo na kwamba
kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
IGP Sirro amesema hayo leo Februari 26 Mjini Bariadi Mkoani Simiyu mara baada ya
kuzungumza na Viongozi na Askari wa Jeshi la Polisi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu
wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja
mkoani humo.
Amesema upo utaratibu wa kufuata maandamano unaoanisha
maandamano halali na yasiyo halali akabainisha kuwa maandamano yasiyo halali yanaashiria
uvunjifu wa amani na kutenda uhalifu, hivyo ikiwa maandamano yataashiria kutenda
uhalifu na kwa kuwa jeshi la polisi lipo kuzuia uhalifu litahakikisha maandamano hayo hayafanyiki.
“Maandamano ambayo si halali njia yake ni
kuyadhibiti na uwezo wa kudhibiti tunao, wananchi wanataka maendeleo hawataki
usumbufu wale wanaotaka usumbufu watapambana na Jeshi la polisi; jambo la msingi nawaeleza wafuate utaratibu
watoe taarifa sisi hatuna tatizo lakini wakitaka kufanya kwa vurugu wasije
wakailaumu Serikali” alisema IGP Sirro.
“Naona kwenye mitandao wanasema lakini
niwaambie tu kwamba kuvunja sheria ni rahisi lakini madhara yake huwa ni mabaya
sana, nawaomba wazazi waendelee kuwapa malezi bora na wawasaidie watoto wao wasijiingize katika matukio ya kuvunja sheria”
alisisitiza
Aidha, IGP Sirro amewataka askari wa Jeshi la Polisi kote nchini kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kufuata misingi ya sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi wanaowahudumia.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Jeshi la Polisi
Mkoani humo limechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu
yaliyokuwepo katika miaka kadhaa iliyopita ambayo ni pamoja na mauaji ya watu
wenye Ualbino, Vikongwe na ukataji wa mapanga.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro akizungumza
na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati alipokuwa katika Ziara yake ya
siku moja Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro akisaini
Kitabu cha Wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake
ya siku moja Mkoani humo(kulia), Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro akifanya mazoezi ya utayari na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Simiyu wakati alipokuwa katika Ziara yake ya siku
moja Mkoani Simiyu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro(wa tatu
kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
Mkoa wa Simiyu, wakati wa Zaira yake mkoani humo, (wa kwanza kushoto), Mkuu wa
Wilya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga.
Kutoka kushoto Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka, IGP Simon Sirro na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jmanne Sagini
wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa ziara ya IGP Sirro mkoani Simiyu.